Tuesday, July 15, 2014

BAGAMOYO; JIMBO TAJIRI LENYE WANANCHI MASKINI

Makala: Hashim Aziz
Kilometa 75, Kaskazini mwa Jiji la Dar es Salaam, ndipo unapopatikana mji mkongwe na wa kihistoria wa Bagamoyo ambao ni miongoni mwa miji yenye vivutio vya kipekee duniani, ulioanzishwa karne ya 18, ukiwa pembezoni mwa Bahari ya Hindi.

Historia inaonesha kuwa Bagamoyo iliyopo mkoa wa Pwani ndiyo kilikuwa kituo kikuu cha biashara ya watumwa na bandari ya kwanza katika mwambao wa Afrika Mashariki, achilia mbali  magofu ya kale, makaburi ya karne nyingi zilizopita, msikiti wa kwanza na kanisa la kwanza Afrika Mashariki pamoja na njia za watumwa (caravans).

Mwishoni mwa wiki iliyopita, Gazeti la Uwazi lilisaga lami mpaka Bagamoyo, lengo kubwa likiwa ni kuangalia jinsi wakazi wa eneo hilo wanavyonufaika na utajiri mkubwa wa kihistoria unaowavutia watalii wengi kutoka sehemu mbalimbali duniani, ahadi za mbunge na jinsi anavyozitekeleza pamoja na matatizo ya wananchi.
Uwazi lilijipenyeza mpaka kwenye Kata za Dunda, Magomeni, Yombo, Kiromo, Zinga, Kerege na Vigwaza zinazounda jimbo hilo linaloongozwa na Mheshimiwa Shukuru Kawambwa (CCM) ambaye pia ni Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi na kubaini mambo mbalimbali.
MATATIZO YA WANANCHI
 Katika ziara yake, Gazeti la Uwazi lilibaini matatizo yakiwemo ukosefu wa madawati, vyumba vya madarasa na vifaa vya kujifunzia katika baadhi ya shule. Uvuvi haramu ni tatizo lingine linalotishia afya ya wananchi wa jimbo hilo nauhai wa viumbe vya baharini ambapo wavuvi hutumia ‘kokoro’ na wakati mwingine baruti.
Kukosekana kwa uwazi wa mapato ya utalii katika Kijiji cha Kaole na Ngome Kongwe kwenye magofu ya kale, ukosefu wa masoko ya uhakika ya mazao ya wakulima yakiwemo mpunga na matunda, mgogoro wa ardhi katika Vijiji vya Buma na Mataya na ukosefu wa huduma bora za afya ni miongoni mwa matatizo mengine yanayowasumbua wakazi wa Bagamoyo.
MAPATO YA UTALII
Uwazi lilichanja mbuga mpaka kwenye Kijiji cha Utalii cha Kaole na kufanikiwa kuzungumza na mkuu wa kituo hicho, Siyawezi Hungo ambaye alifafanua kwamba kwa kawaida, kituo chake hupokea wageni wengi katika miezi ya Julai mpaka Desemba ambapo kwa wastani, watalii 4466 huingia kila mwezi.
“Watalii kutoka nje hulipa shilingi 20,000 kwa watu wazima na 10,000 kwa watoto chini ya miaka 16, kwa wazawa hulipa shilingi 1,000 na watoto ni shilingi 500. Fedha zote zinazopatikana, huwa tunazikabidhi kwa idara ya mambo ya kale ambayo yenyewe ndiyo inayojua namna zinavyotumika,” alisema mama Siyawezi.
MAELEZO YA MBUNGE
Uwazi lilisaga lami hadi kwenye ofisi ya mheshimiwa Kawambwa ambapo lilipokelewa na katibu wa mbunge huyo, Magreth Masenga aliyekuwa na haya ya kuzungumza:
“Kwenye elimu, mbunge amejenga shule tatu, chenji ya rada imenunua vitabu kwa wingi kwenye shule karibu zote za hapa jimboni, shule nyingi zimeingiziwa umeme na wanafunzi wanaokaa chini ni wachache sana, tena kwenye baadhi ya shule.
“Kwenye afya, mbunge amewezesha kujengwa kwa chumba cha kisasa cha upasuaji katika Hospitali ya Wilaya ya Bagamoyo na kupatikana kwa vitanda ingawa suala la manesi na madawa bado ni tatizo. Pia zahanati zote zimepatiwa umeme wa solar kwa msaada wa Shirika la Jewish Heart for Africa (JHFA).
“Wananchi hawana kabisa tatizo la maji, mbunge amechimba visima zaidi ya 200 na mradi wa Ruvu Chini pia unatusaidia. Katika kilimo, kuna ‘scheme’ kubwa za umwagiliaji katika Vijiji vya Chaulo na Jaika na pia ameshughulikia migogoro ya ardhi.
“Kuhusu uvuvi haramu,mbunge ametoa mafunzo maalum kwa wavuvi pamoja na kuwapa vifaa vya kisasa zikiwemo boti za uvuvi. Pia amewapa ajira vijana wengi kwa kuwakopesha bodaboda na kuwapa mafunzo ya ujasiriamali wanawake wengi.
“Kuhusu mapato ya utalii, fedha huwa zinaingizwa kwenye mapato ya halmashauri na ndizo zinazojenga barabara za mitaa, si unaona hapa Bagamoyo barabara nyingi ni za lami, pia matumizi mengine ya fedha hizo nafikiri utayapata ukienda halmashauri.
“Kwenye michezo kuna mashindano ya Kawambwa Cup ambayo yanawapa ajira vijana wengi, kimsingi mheshimiwa anajitahidi sana kuwatumikia wananchi na kuwakwamua kutoka kwenye umaskini. Pia anawasomesha wanafunzi wengi sana hapa jimboni, wananchi ni mashahidi wa jinsi anavyowatumikia,” alihitimisha Masenga.


 

No comments:

Post a Comment

THE DARKEST HOURS (SAA ZA GIZA TOTORO)- 1

Mtunzi: Hashim Aziz (Hashpower) 0719401968 “Ngo! Ngo! Ngo! Fungua!” “Nanii?” “Fungua!” “Jitambulishe kwanza, wewe nani?” “Nimese...