Saturday, September 4, 2010

Big Brother Africa: Watanzania wanaielewa au wanashabikia tu?

• Mtanzania aliyeko Nzega anaelewa maana yake?
• Ni muhimu kweli katika jamii?
JE, umewahi kulisikia shindano linalojulikana kwa maneno ya “Big Brother Africa”? Kama umewahi kulisikia na kulifuatilia linavyorushwa katika vituo mbalimbali vya televisheni, umewahi kusita na kujiuliza lina maana gani?
Kwa tafsiri nyepesi, maneno “Big Brother Africa” yanamaanisha “Kaka Mkubwa Afrika” kwa Kiswahili.
Kwa kifupi, Big Brother Africa ni mashindano yaliyoanzishwa kwa mara ya kwanza nchini Afrika Kusini na kampuni ya Endemol yenye makazi yake nchini Uholanzi. Shindano la kwanza la aina hiyo lilianza Jumapili ya 25 Mei, 2003 likijumuisha nchi 12 za Afrika – ikiwemo Tanzania – ambapo lilirushwa kwa televisheni na kuonekana moja kwa moja (live) katika nchi 42.

Tangu mwaka huo, Big Brother Africa imefanyika mara tano – ikiwemo hii ya sasa ambayo inajumuisha nyota kadhaa waliowahi kung’ara katika mashindano manne yaliyopita. Nyota hao ni wale ambao hawakushinda au hawakushika nafasi ya kwanza ya mashindano hayo.
Mashindano ya sasa yanaitwa Big Brother All Stars.
Ikumbukwe kwamba Tanzania imekuwa ikishiriki mashindano hayo ambapo Mtanzania, Richard Dyle Bezuidenhout, alishinda mashindano ya pili yaliyoanza tarehe 5 Agosti, 2007!
Kama ilivyo kawaida, Watanzania wengi waliojikuta wakiangalia televisheni siku ya tarehe 11 Novemba, 2007, usiku, ni dhahiri walishangilia walipogundua kwamba kuna Mtanzania mwenzao alikuwa ameshinda mpambano “fulani” uliokuwa ukitazamwa na mamilioni ya watu barani Afrika na sehemu kadhaa duniani.
Kwa wengi, furaha yao ilikuwa ni hiyo tu! Hawakujali wala kujua nini kilikuwa kimefanyika hadi kijana Richard akaibuka mshindi!
Lakini, je, kwa wanaoifahamu na wanaoishabikia Big Brother Africa, wanaweza kuwaeleza Watanzania wengine wasiofahamu, asili (essence) na maana (significance) ya mashindano hayo?
Kwa ufahamisho – hususani kwa wale ambao wanayafahamu kidogo na wasioyafahamu kabisa -- ni kwamba, mashindano hayo hujumuisha washindani vijana wa kike na kiume ambao huishi katika jengo au makazi ya pamoja, kwa siku zipatazo 100, wakifanya mambo yote kwa pamoja kama vile kula, kulala, kunywa, kucheza na kadhalika.
Kufanya mambo yote pamoja kunamaanisha “pamoja” kweli! Yaani kuchanganyika pamoja -- wanaume na wanawake -- tangu bafuni hadi kitandani.
Kama ni kulala pamoja kunamaanisha ni kulala katika ukumbi au chumba kimoja, kitanda kimoja na kujifunika shuka moja!
Kwa mfano, kuoga pamoja kuna maana hiyohiyo kwa mwanamke na mwanamme! Kwa maneno mepesi zaid ni kuvua nguo wote na mkaoga pamoja!
Kwa wasiowahi kuyaona mashindano hayo yakirushwa kwa televisheni wanadhani maneno haya ni uzushi, lakini kwa wale ambao wamewahi kuyaona na wanayafuatilia haya ya sasa ya Big Brother All Stars, wanayaelewa yale wanayoyasoma katika safu hii.
Kitu cha ajabu na cha kuvutia katika Big Brother Africa ni kwamba kila uchochoro wa makazi hayo yanakofanyika mashindano hayo, kuna kamera zinazochukua picha za moja kwa moja za washiriki kutoka mahali popote walipo na kuzirusha angani kwa watazamaji duniani!
Kamera hizo huchukua picha tangu kitandani, bafuni, jikoni, na popote pengine!
Hata hivyo, pamoja na yote hayo ambayo hufanyika katika jengo hilo kwa siku zote hizo, kitu cha kuvutia zaidi ni kwamba mshindi wa kwanza hupata kitita kikubwa cha fedha. Richard aliposhinda alipata kitita cha dola za Marekani ambazo ni sawa na kiasi cha sh. 1,000,000 na zaidi za Kitanzania!
Ni jambo la kufurahisha.
Lakini, kwa jumuia ya Afrika, hususani Tanzania, maudhui hasa ya mashindano hayo ni nini? Kuna wale wanaodai kwamba yanapima uvumilivu wa vijana. Je, ni uvumilivu gani anaotakiwa kupimwa mwanamke na mwanamme ambapo tangu asubuhi wanaamka wakala, wakacheza na kulala kwa pamoja kwa siku zipatazo 100?
Uvumilivu gani huo usioweza kupimwa nje ya jengo hilo lililojaa kina aina ya vituko visivyokuwa na mafunzo yoyote kwa vijana wengine wanaoyafuatilia mashindano hayo katika vituo vya televisheni?
Kwa kifupi: Je, kuna chochote cha kujifunza kwa watu wengine – wakiwemo watoto na wazee – kutoka Big Brother Africa? Kama kipo ni kipi?
Mwandishi wa makala hii hapingani na mashindano hayo, lakini anataka kufahamu hasa mashindano hayo yana lengo gani kwa jamii, hususani kwa mamilioni ya watu maskini waliozagaa barani Afrika?
Au, je, mashindano hayo yanahusu ulimwengu wa wasomi na matajiri tu? Yaani watu wanaoweza kuzungumza Kiingereza tu?
Tatizo liko hapo!
Je, ni rahisi kumweleza Mtanzania wa kawaida, mfano shangazi zetu na baba zetu walioko vijijini Nzega au Nachingwea, wakaielewa – na kuikubali -- Big Brother Africa?
Tunakielewa kweli kinachofanyika Big Brother Africa au tunashabikia tu ili tusionekane “washamba”?

No comments:

Post a Comment

THE DARKEST HOURS (SAA ZA GIZA TOTORO)- 1

Mtunzi: Hashim Aziz (Hashpower) 0719401968 “Ngo! Ngo! Ngo! Fungua!” “Nanii?” “Fungua!” “Jitambulishe kwanza, wewe nani?” “Nimese...