Sunday, August 15, 2010

USILIE TENA GENEVIV - SIMULIZI ZA MAJONZI

Geneviv ni binti mdogo ambaye amezaliwa katika familia yenye maisha mazuri sana.Mungu amemjaalia kuwa na sura nzuri yenye mvuto.Bahati mbaya kuzaliwa kwake akiwa na sura nzuri na urembo usio na kifani kunamfanya apate mateso makubwa sana kutoka kwa wanaume ambao kila mmoja akiwemo hata baba yake wanamtumia kimapenzi na baadae kumuacha akipata mateso makubwa mno.

Uzuri ambao Mungu alimjaalia unageuka kuwa sumu kali ambayo inammaliza taratibu mpaka anakaribia kupoteza uhai wake, akiwa katika hatua za mwisho kabisa za uhai wake.Ni mateso,maumivu, machozi,majeraha mtimani na kilio ndivyo vinavyotawala maisha yake.Anaichukia dunia,anawachukia wanaume…hawezi kulipa kisasi,anachoweza kufanya ni kutoa machozi muda wote,analia lakini hakuna anayemsikia! Anapokaribia kukata pumzi anasikia sauti ikimfariji…Shed no more tears Geneviv!

Ungana nami ufahamu mkasa mzima



SEHEMU YA KWANZA
Ilikuwa ni alfajiri tulivu,miale ya jua ikianza kuchomoza kwa mbali kuashiria mwanzo wa siku mpya,siku ya jumatatu.Milio ya ndege wa angani waliokuwa wakiimba na kurukaruka kutoka tawi moja hadi tawi jingine juu ya miti waliufanya mwanzo wa siku uwe wakuvutia sana.Jua lilikuwa likizidi kuchomoza huku nuru yake ikilifukuzia mbali giza la alfajiri.

Wakati kukizidi kupambazuka,upande wa pili alikuwepo binti mdogo aliyekuwa amejilaza chini ya mti mkubwa,mahali ambapo yamekuwa makazi yake kwa muda mrefu sasa,akishinda kutwa nzima akiwa amejilaza chini kivulini na giza likiingia alikuwa akilala na kujifunika kipande cha gunia palepale mpaka asubuhi.Mwili wake wote ulikuwa umejawa na vidonda vilivyokuwa vinatoa usaha na kumsababishia maumivu makali kupita kiasi.

Harufu kali ya majeraha yaliyokuwa yakiendelea kuuozesha mwili wake na harufu ya haja kubwa aliyokuwa anajisaidia hapo hapo, vilipafanya pale chini ya mti panuke mithili ya mzoga wa mnyama aliyejifia.

Binti yule mdogo hakuwa na msaada wowote,hakuweza hata kuinuka kutoka pale chini alipokuwa amelala…alichoweza ilikuwa ni kufumba na kufumbua macho na kufukuza nzi waliokuwa wakivizonga vidonda vyake.Alishakata tamaa ya kuishi na alionekana kama anayengojea pumzi yake ya mwisho ikatike aondokane na mateso makali yaliyokuwa yanamuandama.Kwake maisha yalipoteza maana kabisa,aliichukia dunia na vyote vilivyomo ndani yake.Mara kwa mara alikuwa akimkufuru Muumba wake kwa kumsababishia mateso makali kiasi kile kwani aliamini anateseka kwa sababu Mungu alimuumba akiwa mrembo kupita kiasi.

Aliamini anapata mateso makali kiasi kile kwa sababu ya uzuri wake aliopendelewa na Mungu,na huo ndio ulikuwa ukweli.Miaka michache tu aliyoishi duniani ilikuwa ni kama karne nzima kwani alipitia mateso makubwa sana ambayo kama angepata nafasi ya kuusimulia ulimwengu hakika kila mtu angemwonea huruma na kudondosha machozi.Aliendelea kuwaza akiwa amelala pale chini huku macho yake yakilitazama jua lililokuwa linazidi kuchomoza na kuanza kuwa kali.

Dunia aliiona kama shimo la hewa na zaidi aliwachukia wanaume.Aliapa kuwa kama angepata nafasi ya kulipa kisasi,angewateketeza wanaume wote duniani.Aliamini wanaume ni mashetani kwa waliyomfanyia na akazidi kukufuru dini kwa kumlaumu Mungu kwa kuwaumba wanaume.
“ I hate the world,I hate men…”
alijisemea Geneviv pale chini alipolala kwa sauti ya kunong’ona.

Kumbukumbu zake zilimrudisha nyuma alipokuwa bado mdogo.
Aliyakumbuka maisha ya furaha aliyoishi na familia yake kabla mambo hayajaanza kubadilika.Alishindwa kuyazuia machozi ambayo yalianza kuuloanisha uso wake mchanga uliochakazwa na mateso… soo many tears…hakika alitia huruma.

Geneviv alikuwa ni mtoto wa kipekee kwenye familia ya mzee Manuel Rwakatare na Bi. Patricia mahiza.Alizaliwa kwenye familia yenye uwezo mkubwa kifedha, baba yake akiwa ni Afisa utumishi katika wizara ya Madini na nishati huku mama yake akiwa Katibu Muhtasi katika ofisi ya waziri mkuu wa Nchini Blaziniar.Tangu anazaliwa maisha yalikuwa mazuri kupita kiasi huku wazazi wake wakijitahidi kumpatia kila alichokihitaji.

Waliishi kama wako peponi huku pesa kwao ikiwa sio tatizo.
Uzuri aliojaaliwa Geneviv ulianza kuonekana tangu akiwa mdogo hali ambayo ilizidi kuwaongezea fahari mzee Rwakatare na mkewe.Kila aliyemuona mtoto Geneviv alishindwa kujizuia kumsifia.Sura yake iliyokuwa na mchanganyiko safi wa baba na mama ulizidi kumfanya aonekane kama malaika…

“you have beared a very cute angel sir,congrats!”
(umezaa mtoto mzuri sana mzee,hongera sana)
Hiyo ilikuwa ni kauli kutoka kwa mmoja kati ya wafanyakazi wenzake mzee Rwakatare akimsifia kwa kuzaa mtoto mzuri kiasi kile.
Bi Patricia naye alikuwa akipokea sifa kila alipopita na mwanae hali iliyozidi kumpa kichwa na kumfanya ajione kama mama wa malaika.

”Atawasumbua sana vijana wa kiume akikua huyu,kama wewe ulivyonisumbua kipindi nakutafuta darling…”
Mzee Rwakatare alimtania mkewe wakati wakipata chakula cha jioni na mtoto wao Geneviv.Bi Patricia alitabasamu huku akimbusu mumewe shavuni.
Siku zikawa zinasonga kwa kasi huku Geneviv akizidi kukua na kupendeza zaidi, urembo wake ukizidi kujionyesha dhahiri hali iliyomfanya aonekane tishio mbele ya kila aliyemtazama.

Alipotimiza miaka saba wazazi wake wakaona bora wamuanzishe shule.Akatafutiwa shule nzuri yenye hadhi ya kimataifa, st Benard Blaziniar academy,shule iliyokuwa ikisifika kwa kutoa elimu bora kwa nadharia na vitendo.Baada ya taratibu zote kukamilika Geneviv akaanza shule.Aliahidi kwa wazazi wake kuwa atasoma kwa bidii mpaka afike chuo kikuu.

“I want to be a doctor daddy! I want to heal the world…”
(Nataka kuwa daktari baba,nataka kuuponya ulimwengu)
Geneviv alikuwa akimwambia baba yake asubuhi wakiwa ndani ya gari lao akimpeleka shule.

“Sure! Go for it and you can be what you you want to be”
(Hakika utakuwa kama unavyotaka kuwa ukijipangia malengo vizuri na kuyatekeleza)

Mzee Rwakatare alikuwa akimtia ujasiri bintiye kuwa anaweza kuwa daktari ikiwa atajiwekea malengo madhubuti ya kusoma kwa bidii.
“Let education be your only heritage daughter coz when everything has gone the future still remain dark”
(Ikazanie sana elimu ndio iwe urithi pekee maishani mwako, vitu vyote vitakapopita, maarifa yatabaki kuwa mwanga pekee wa maisha yako)

Baada ya kumfikisha shule,Geneviv alipokelewa na mwalimu na kuelekezwa utaratibu wa Shule.Ilikuwa ni furaha isiyo kifani kwa Geneviv kuanza shule.Alikuwa amechoka kufungiwa ndani kila siku,akaona huo ndio muda muafaka wa kuanza kufurahi na wenzake.Alijiwekea nadhiri ya kusoma kwa kadri ya uwezo wake wote ili azidi kuwafurahisha wazazi wake na kutimiza ndoto yake.

Baada ya siku chache tu tangu Geneviv ajiunge na Shule ya st Bernard Blaziniar, wanafunzi karibu wote na walimu walishamfahamu kutokana na uzuri aliojaaliwa.Wengine wakambatiza jina na kuanza kumuita “Cute Angel”. Usingepata shida kumtafuta kwani kila kona ya shule alifahamika. Akapata marafiki wengi huku wavulana anaosoma nao Grade one (darasa la kwanza) wakijigonga kila mmoja akitaka awe mchumba wake.

“Geneviv njoo tudimbedimbe mi niwe baba wewe uwe mama” aliongea mwanafunzi mmoja aliyeitwa Kim darasani na kusababisha darasa zima licheke.
Ukiacha uzuri na shani alivyokuwa navyo Geneviv,pia alitokea kuwa mwelewa “Bright” darasani hali ilyomfanya azidi kuwa kivutio kwa walimu wake na wanafunzi.
Kadri siku zilivyokuwa zinaenda mbele umaarufu wa Geneviv ukawa unaongezeka.

Nyumbani nako hali ilizidi kuwa shwari huku baba yake mzee Manuel Rwakatare na mkewe bi Patricia wakizidi kuonyeshana mapenzi motomoto. Amani na upendo vikazidi kutawala ndani ya familia ya mzee Rwakatare hali iliyozidi kumpa furaha Geneviv.Akawa anazidi kukua vizuri kimwili, kiakili na kiroho, kwani alifundishwa pia kumcha Mungu.

****

Katika kipindi hiki chote, baba yake alikuwa bado ni mfanyakazi wa wizara ya madini na nishati huku akipokea mshahara mnono na marupurupu yaliyomfanya aweze kuyamudu maisha ya familia yake kwa kiwango cha juu kabisa.Alianzisha vitega uchumi vingi nchini Blaziniar na katika nchi jirani ya Tanzania.Pamoja na kwamba alipata mshahara mkubwa na mke wake naye alikuwa akipokea mshahara mnono, bado siri ya utajiri wao uliokuwa unazidi kukua kila ilipoitwa leo haikufahamika.Kwa makadirio ya haraka ilitosha kusema kwamba mafanikio makubwa aliyokuwa nayo mzee Manuel Rwakatare yalizidi kipato chake halisi.

Mambo yakaanza kubadilika ofisini kwake mara baada ya Raisi mpya, mhe. James Kahungo “the JK”, kuingia ikulu ya Blaziniar.Raisi huyu mpya mwana mageuzi halisi aliwataka watumishi wote wa wizara zote nyeti kuorodhesha mali walizokuwa wanazimiliki na kueleza namna walivyozipata.

Tofauti na maraisi wengine ambao nao walikuwa wakitoa mkwara kama huo bila kusimamia utekelezaji, James kahungo alionyesha kudhamiria kiuhakika kuwapunguza wahujumu nchi.Miezi mitatu tu tangu aingie madarakani,watumishi zaidi ya mia tatu walisimamishwa kazi kwa kosa la ubadhirifu na kujilimbikizia mali kinyume na sheria ya nchi ya Blaziniar.

Kivumbi kikahamia kwenye wizara ya Madini na Nishati ambako uozo mkubwa ulifichuliwa wa hujuma nzito zilizokuwa zikifanyika.Mzee manuel Rwakatare, baba yake Geneviv naye akawa miongoni mwa waliokumbwa na Ufagio wa chuma.Alisimamishwa kazi baada ya kugundulika kuwa ameingiza hasara ya mamilioni ya pesa kwenye ofisi yake.Mahakama ikaamuru mali zake zote isipokuwa nyumba aliyokuwa anaishi zitaifishwe ili kufidia deni alilokuwa anadaiwa.

Ilikuwa vigumu sana kwa mzee Manuel Rwakatare kukabiliana na hali halisi.Alishazoea kucheza na mamiloni ya pesa,leo ghafla anafukuzwa kazi na mali zake zote kufilisiwa! hakutaka kuamini haraka kuwa ni kweli yamemkuta. Akaanza kuhangaika kwa waganga kutafuta ni nani aliyemloga bila mafanikio…akaanza pia kwenda kuroga usiku na mchana ili arudishwe kazini lakini wapi! Mwisho akajikuta akiishiwa mbinu. Mkewe bi Patricia akawa anajitahidi kumfariji mumewe na kumtuliza kwa maneno matamu lakini hgakufanikiwa.

“Mume wangu yote tumwachie mungu, mshahara wangu utatosha kutufanya tuishi vizuri na mwanetu atasoma bila shida, wewe kinachokuumiza ni nini? Calm down please my Huz, everything gonna be alright”
Bi patricia alikuwa akimbembeleza mumewe usiku baada ya kuona hali ya mumewe inazidi kuwa mbaya, chakula hali wala usingizi hapati.Pamoja na kujaribu kumfariji usiku kucha kila siku, bado haikusaidia kitu.Mzee Rwakatare alikuwa amekata tamaa kabisa…kila kitu kilipoteza maana kwake.Akaona njia bora ya kutoa mawazo na mfadhaiko ni kunywa pombe! Akaanza kidogokidogo kunywa pombe,kumbe ndio alikuwa anaongeza matatizo.

Maisha yakaanza kubadilika kwa kasi ya ajabu, kutoka kwenye umilionea hadi kwenye ufukara. Akiba ya Pesa zilizokuwa zimesalia akawa anazitumia kunywea pombe…”From Hero to Zero”

ndivyo wambea wa mitaani walivyoanza kumuita na kumbeza baada ya habari kuzagaa karibu kila kona ya nchi juu ya kufukuzwa kwake kazi.Ni katika kipindi hiki Geneviv alikuwa akijiandaa kufanya mtihani wa mwisho wa kuhitimu elimu ya msingi. Hakufahamu mara moja ni nini kimemtokea baba yake kwani muda mwingi alikuwa yuko shule akijiandaa na mitihani.
“Mama mbona dadii siku hizi haendi kazini?”
Geneviv aliuliza swali ambalo lilikuwa kama msumari wa moto kwa Bi Patricia. Ilibidi atumie uongo kumridhisha Geneviv kuficha aibu ya mumewe.
“Dadii yuko likizo mwanangu,ameamua kupumzika nyumbani”

Geneviv hakuridhika na jibu hilo lakini kwa jinsi alivyozisoma hisia za mama yake kwa haraka akajua lazima kuna kitu ambacho mama yake anamficha.Akauliza swali lingine ambalo nalo lilikuwa gumu…

“Lakini mbona siku hizi anachelewa sana kurudi nyumbani na akija anakuwa ananuka pombe…kwani ameanza lini kunywa Pombe? Mwalimu shuleni ametufundisha kuwa kunywa pombe ni vibaya na ni tabia hatarishi,sasa mbona baba ameanza kunywa?”
Geneviv alikuwa akiendelea kumshambulia mama yake kwa maswali mfululizo ambayo yote Bi. Patricia alishindwa kuyajibu.

“Basi mngoje akirudi umuulize mwenyewe maana mimi nashindwa kuyajibu.”

Alijitetea Bi Patricia na kabla hata hajamalizia ,wote walisikia mlango ukigongwa kwa nguvu,wakajua baba mwenye nyumba karudi.Geneviv akanyanyuka na kukimbilia mlangoni kwenda kumfungulia baba yake.
Tofauti na alivyozoea kumuona,mzee Rwakatare alikuwa tofauti kabisa,hali iliyomfanya Geneviv arudi nyuma kwa hofu…
“Whats wrong with you daddy?”
Aliuliza Geneviv kwa sauti iliyokuwa ikitetemeka kwa hofu.Mzee Rwakatare alikuwa amelewa kupita kiasi ,akishindwa hata kutembea vizuri kiasi cha kujiegemeza kwenye mlango kama mgonjwa,ile Geneviv anafungua tu mlango,mzee Rwakatare alidondokea kwa ndani na kuanguka sakafuni kama gunia …Puuh!

“Daddy! Are you sick? Mama njoo umuone daddy…”

alipaza sauti kwa nguvu Geneviv na kuanza kukimbilia ndani alikomuacha mama yake.Alikuwa ameshtuka kupita kiasi akidhani baba yake amepatwa na jambo baya.Hakujua kuwa Starehe ya pombe ndiyo iliyomfanya awe vile.
Hata kabla ya kumuona,Bi Patricia alishajua kilichomsibu mumuwe.Alichokifanya ni kumtuliza mwanae Geneviv ambaye alionekana kuchanganyikiwa,akampeleka chumbani kwake na kumsihi alale mpaka asubuhi na kumhakikishia kuwa baba yake hakuwa na tatizo lolote.Kweli Geneviv alikubali kulala kwa shingo upande huku maswali mengi yasiyo na majibu yakipishana kichwani mwake.

Baada ya kuhakikisha Geneviv ametulia Bi Patricia alirudi mlangoni na kumkuta mumewe akiwa bado palepale chini akikoroma kutokana na kuzidiwa na pombe.Kwa upole alimuinua na kumpeleka chumbani kwao.Alimvua nguo na kumpeleka bafuni ili angalau azinduke baada ya kuoga maji ya baridi.Kweli alifanikiwa kwani baada ya kummwagia maji mengi ya baridi Fahamu zilimrudia na pombe zikamuisha kichwani.Baada ya kumuogesha vizuri,Bi Patricia alimshika mkono mumewe na kumpeleka chumbani ambapo alimlaza vizuri na kumuacha apumzike.

Alipohakikisha kuwa kila kitu kimetulia Bi Patricia alienda chumbani kwa mwanae Geneviv.Alimkuta akiwa bado hajalala.Alikuwa amejikunja kitandani huku ameukumbatia mto wake.Aligundua namna mwanae alivyopatwa na mshtuko kwa kumuona baba yake katika hali ile.Akaamua kumfariji na kumfanya asahau kila kitu.Alianza kumfanyia utani kama walivyozoea kufanyiana kila siku na baada ya muda mfupi Geneviv alikuwa tayari ameshasahau yote yaliyotokea,wakawa wanacheka kwa furaha.

Kelele za vicheko zilimshtua mzee Rwakatare ambaye aliamka na kuanza upya kuvaa nguo.Japokuwa pombe ilikuwa imepungua lakini bado akili yake ilikuwa haijatulia.Alifikiri mkewe na mwanae wanamcheka yeye kwa sababu amelewa sana,kumbe haikuwa hivyo.Akajikuta hasira zikianza kumpanda na mara akainuka na kuanza kufoka kwa sauti. Bi Patricia aliposikia mumewe anafoka alitoka haraka na kumucha Geneviv akijiandaa kulala.Akawa anatembea kwa haraka kuelekea chumbani kwao, kabla hata hajafika akamuona mumewe akitoka kwa jazba chumbani.Wakakutana mlangoni…

”Mnachekacheka nini na mwanao? mnanicheka mimi sio? Sasa leo mtanijua!”
Aliongea kwa ukali mno mzee Rwakatare, akimfokea mkewe kama mtoto mdogo.Bi patricia alibaki ameduwaa akimshangaa mumewe.Tangu waoane karibu miaka kumi na tano iliyopita hakuwahi kumuona mumewe akiwa katika hali kama ile. Bila hata kusubiri mkewe ajitetee mzee Rwakatare akaanza Kurusha ngumi na mateke kama anapigana na mwanaume mwenzake.Mkewe akaamua kukimbilia chumbani bila ya kupiga kelele hata kidogo akihofia mwanae Geneviv angejifunza kitu kibaya.


Alipoingia chumbani alitaka kuwahi kujifungia kwa ndani lakini Mzee Rwakatare akamuwahi na kuusukuma mlango kwa nguvu.Akaingia na kuufunga mlango kwa ndani.Kilichoendelea humo ikawa ni kipigo mtindo mmoja.Bi Patricia alijitahidi kujitetea lakini wapi…baadae akaanguka chini na kupoteza fahamu baada ya kuzidiwa na maumivu huku damu nyingi zikimtoka puani na mdomoni.Baada ya kuona mkewe amedondoka na kupoteza fahamu,mzee Rwakatare akatoka na kuufunga mlango kwa nje.Akahamia kwenye chumba anacholala mwanae.

Kitendo cha Geneviv kumuona baba yake akiingia chumbani mwake kilimfanya moyo umlipuke kwa hofu.Alishasikia ugomvi uliokuwa unaendelea chumbani kwa wazazi wake, akajua sasa ni zamu yake.Tangu aanze kuwa na akili hakuwahi kupigwa hata kibao na baba yake,akabaki akisubiri aone kitakachomtokea.

Mzee Rwakatare baada ya kumuona mwanae akiwa amejawa na hofu kiasi kile,anajikuta nguvu zikimuishia na kuanza kumuomba msamaha mwanae.Geneviv alishindwa kuelewa nini lengo la baba yake na akabaki akimkodolea macho huku akishindwa kuificha hofu yake.Mzee Rwakatare akawa mpole ghafla na akasogea na kukaa karibu na geneviv juu ya kitanda chake.

Bado Geneviv akawa anatetemeka mwili mzima kiasi cha kufanya kijasho chembamba kimtoke na kuiloanisha Night dress ndogo aliyokuwa ameivaa.Dakika kama tatu zikapita huku wakiwa bado wanatazamana,mwishoni Geneviv alishindwa kujizuia na kumuuliza baba yake kwa sauti ya kutetemeka,

“Where is my mum,Why do you act like this to us?
(Mama yangu yuko wapi,kwanini unatufanyia hivi)

Kwa mara ya kwanza Mzee Rwakatare akaligundua kosa alilolifanya,akajikuta akikosa jibu la kumpa mwanae…akiwa bado anajikanyaga, Geneviv alimsukuma kwa nguvu na kukimbilia chumbani aliko mama yake,alipofika mlangoni akakuta mlango umefungwa kwa funguo, akawa anagonga kwa nguvu akimtaka mama yake amfungulie…akiwa bado anagonga,akaona kitu chini ya mlango ambacho kinamshtua mno.Aliona michirizi mikubwa ya damu ikichuruzika kupitia chini ya mlango kutoka ndani ya chumba alimo mama yake.Nguvu zikamuishia na taratibu akakaa chini na kuzigusa zile damu akiwa bado haamini.
“Dady, did you kill my mother? I hate you… “

Geneviv aliongea kwa sauti kubwa na kuanza kupiga kelele za kuomba msaada kwa majirani.Mzee Rwakatare akiwa amechanganyikiwa akatokea mlango wa nyuma na kutokomea gizani akielekea kusikojulikana.Geneviv akazidi kupiga mayowe yaliyowaamsha majirani ambao ndani ya muda mfupi walikusanyika kutaka kujua kumetokea nini.

Geneviv akisaidiana na majirani waliuvunja mlango na kufanikiwa kuingia chumbani ambako walimkuta mama yake akiwa amelala chini huku damu nyingi zikimtoka puani na mdomoni.Uso mzima ulikuwa umevimba kiasi cha kutotambulika…Geneviv akajikuta mwili wote ukimlegea akiwa haamini alichokiona, ghafla na yeye akaanguka na kupoteza fahamu.

****
Bi patricia alikuja kurudiwa na fahamu baada ya siku mbili.Alipofumbua macho tu,sauti ya kwanza kuisikia ilikuwa ni ya mwanae Geneviv aliyekuwa amekaa pembeni yake akilia huku akisali kwa sauti ya chini, ndani ya wodi ya upasuaji ya hospitali ya Planet Health Aid.

Kumbukumbu za matukio yote yaliyompata zilikuwa zimepotea kutokana na majeraha makubwa aliyokuwa ameyapata sehemu za kichwani na kifuani.
“Hapa ni wapi?” Aliuliza Bi Patricia huku akizishangaa dripu za maji na dawa zilizokuwa zinatiririka kuingia mishipani mwake.Kitendo cha kufumbua macho na kuuliza hapo ni wapi kilimshtua Geneviv aliyekuwa amezama kwenye kilio na Sala ya kumuombea mama yake.

“She is awake, Nurse Please come quick, my mother is back into her counciousness”

Aliongea Geneviv kwa sauti kubwa huku akiwa na furaha na akakimbia mpaka kwenye chumba cha nesi aliyekuwa anamhudumia mama yake.Sekunde chache baadae Geneviv alirudi akiwa ameongozana na nesi. Bi Patricia alikuwa bado akijaribu kukumbuka ni nini kilichomtokea mpaka akawa hapo.
Geneviv akawa anamshukuru Mungu kwa kumrejeshea fahamu mama yake huku machozi yakizidi kumiminika kwenye mashavu yake laini.Nesi alimtumliza Geneviv kwa kumwambia kuwa mgonjwa anahitaji kupumzika zaidi kwani alipata majeraha makubwa hivyo kelele zingemuongezea maumivu.Geneviv alielewa haraka na akatulia kimya akimtazama mama yake usoni alikokuwa amefungwa bandeji kubwa.

“Pole mum, My dad is a devil,I hate him…”
Aliongea Geneviv huku akimpiga busu mama yake.Hapo Bi Patricia akaanza kukumbuka yaliyomtokea mpaka akawa hpo hospitalini.Aliumia sana moyoni mwake, na kilichomuumiza haikuwa majeraha na maumivu aliyoyapata, aliumizwa zaidi na Geneviv ambaye aliyashuhudia yote na kujifunza kitu kibaya akilini mwake.
“Don’t cry for me Geneviv, im okay and everything is fine, Pray God for your daddy, don’t hate him.”
Aliongea Bi Patricia kwa taabu akimsihi binti yake kuchukulia kawaida yote yaliyotokea na kuzidi kumwomba Mungu kwani yeye ndiye mweza wa yote.
Bi Patricia aliendelea kutibiwa kwa siku kadhaa na hali yake ilipokuwa nzuri akaruhusiwa kurudi nyumbani.

Kwa siku zote alizokuwa Hospitalini, mumewe hakuwahi kuja hata mara moja kumjulia hali yake.Msaidizi mkubwa akawa ni mwanae pekee Geneviv ambaye ilibidi aache kwenda shule kwa takribani wiki mbili akimhudumia mama yake.Kipindi ambacho Geneviv alikuwa haendi shule, wenzake ndio walikuwa katika maandalizi ya mwisho kabla ya kufanya mtihani wa mwisho wa kumalizia elimu ya msingi
.
Aliendelea kumuomba Mungu amsimamie katika wakati mgumu aliokuwa nao.Kwa kipindi chote hicho Mzee Manuel Rwakatare alikuwa hafahamiki yuko wapi kwani hata nyumbani kwake alikuwa hakanyagi.
“Mum why cant we report dad on police station for the pain he has caused you?”
(mama kwanini usimshitaki baba polisi kwa maumivu aliyokusababishia?)
Aliuliza Geneviv wakati akimpoozea mama yake uji.Pamoja na maumivu aliyosababishiwa na mumewe,Bi Patricia bado alikuwa anampenda na alishamsamehe kwa yote yaliyotokea.

“Mwanangu Geneviv,matatizo ya kifamilia humalizwa na wanafamilia wenyewe kwa msaada wa Mungu baba wa Mbinguni,kwenda polisi ni kuongeza matatizo kwani hawatatusaidia chochote.Mungu anatufundisha kuwapenda wanaotufanyia mabaya, kusamehe
na kusahau kama yeye anavyotusamehe dhambi zetu,nakuomba usimchukie baba yako,msamehe kwani ni shetani ndio anamtumia kwa sasa,jifunze kusamehe…”

Bi Patricia alikuwa akimpa darasa zito binti yake kwani alionekana kuanza kumchukia baba yake.Wakiwa bado wanaendelea na mazungumzo yao, walisikia mlango ukigongwa kwa nguvu.Wakajua “Simba mtu amerudi”. Geneviv akainuka na kwenda kufungua mlango.Alikuwa ni baba yake,mzee Rwakatare.Japokuwa ilikuwa ni asubuhi,alionekana ameshalewa kama mtu aliyelala kwenye kilabu cha pombe.Bila hata salamu, mzee Rwakatare aliingia mpaka ndani alikomkuta mkewe akinywa uji alioandaliwa na mwanae.

“Karibu mume wangu,habari za asubuhi!” alimpokea kwa moyo mkunjufu mumewe.Mzee Rwakatare hakujibu kitu, akaanza kufoka.Safari hii alikuja na hoja mpya akimtuhumu mkewe kuwa anatembea na bosi wake na ndio maaana wakaandaa njama za kumfukuzisha kazi. Bi patricia hakujibu kitu akawa anamtazama mumewe usoni kwa huruma.
Geneviv alikuwa amesimama mlangoni akishuhudia yote yaliyokuwa yakiendelea. Ghafla mzee Rwakatare alimvamia mkewe pale alipokuwa amelala akiuguza majeraha yake ya kupigwa ambayo yalikuwa bado hayajapona.
“Si naongea na wewe? Mbona hunijibu…kiburi sio?”

Kabla hata Bi Patricia hajajibu lolote, alishtukia akipigwa kibao kizito usoni, damu zikaanza kumtoka masikioni,puani na mdomoni.
Geneviv alishindwa kuvumilia kitendo kile alichokiona.kwa nguvu zake zote akaibeba stuli iliyokuwa mbele yake na kuinyanyua juu, kisha akaishusha kwa nguvu kichwani kwa baba yake.Ilitua kisawasawa utosini na kumfanya mzee Rwakatare apige yowe kubwa kisha akadondoka chini na kutulia kimya…alipoteza fahamu.

“Umefanya nini Geneviv, si nilikwambia usilipe ubaya kwa ubaya?” aliongea Bi patricia huku akijikongoja kuamka kitandani na kumuinamia mumewe pale chini huku akijifuta damu zilizokuwa zinavuja baada ya kupigwa kibao na mumewe.
Geneviv alibaki akimshangaa mama yake, Pamoja na maumivu yote aliyokuwa anapewa na mumewe bado alikuwa akimtetea!
“No mum,no mum, it pain my heart, cant tolerate to see this…im walking away”
Aliongea Geneviv na kuanza kukimbia kuelekea nje akiwa haelewi anakokwenda. Hakukusudia kumuumiza baba yake,lakini pia hakuweza kuvumilia kuona mateso aliyokuwa anayapata mama yake.

Hakukumbuka hata kuvaa viatu,akatoka hivyohivyo huku akikimbia kama aliyerukwa na akili.Alikimbia umbali mrefu sana mpaka akaanza kuhisi mwili wote ukiishiwa nguvu.Akatafuta mti wenye kivuli na kujitupa chini huku machozi yakimtoka kama chemchemi.Taratibu usingizi ukaanza kumpitia…

****
Mzee Rwakatare alikuja kushtuka baada ya masaa manne tangu alipopoteza fahamu kwa kupigwa na kitu kizito kichwani. Alijikuta amelala chumbani kwake huku mkewe Bi Patricia akimpepelea kwa kanga yake na kiyoyozi alichokisogeza karibu kabisa na kitanda.
“Pole mume wangu, nisamehe kwani mimi ndio chanzo cha yote”
Alikuwa akiongea Bi Patricia kwa sauti ya chini huku machozi yakimtoka. Mzee Rwakatare alifumbua macho akiwa hakumbuki kilichomtokea, alichokihisi ni maumivu makali sehemu ya utosini.
“What happened to me!” Alihoji mzee Rwakatare kwa sauti ya chini,mkewe hakumjibu kitu, akabaki akimtazama usoni kwa huruma.Baada ya muda kumbukumbu zikaanza kumrudia upya.Alikumbuka kila kitu kuanzia siku ya kwanza alipompiga na kumjeruhi vibaya mkewe na kisha kumtelekeza chumbani akiwa amepoteza fahamu.Alikumbuka alivyoshinda kwenye baa za pombe kwa wiki mbili mfululizo huku akiwa hajui mkewe anaendeleaje ingawa alisikia kuwa alikuwa amelazwa.Alikumbuka pia jinsi alivyoingia kwa vurugu asubuhi hiyo na kuanza kumpiga upya mkewe japokuwa alijua kabisa kuwa bado hajapona.Kumbukumbu zake ziliishia hapo…

“What happened to me?....” alirudia swali lake lilelile lakini Bi Patricia hakumjibu kitu zaidi ya kuendelea kububujikwa na machozi.Kilichomshangaza Mzee Rwakatare ni kule kuzinduka na kujikuta yuko mikononi mwa mkewe.kwa matukio aliyokuwa anamfanyia aliamini isingekuwa rahisi kwa mkewe kuendelea kumpenda na kumjali kiasi kile.Alipomtazama tena usoni,aligundua mkewe alikuwa na makovu makubwa ambayo ni yeye ndiye aliyemsababishia.Alijikuta dhamira yake ikimshtaki kwa uovu aliomfanyia mkewe waliyetoka naye mbali kimaisha.

“Patricia…”
Bi Patricia alishtuka kumsikia mumewe akilitaja jina lake kwani tangu wampate mtoto wao Geneviv, mumewe aliacha kabisa kumuita jina lake…akitumia zaidi mama Geneviv au My Darling!
“Abee mume wangu!” aliitikia Bi Patricia kwa adabu huku akijifuta machozi.
“Naomba nisamehe mke wangu.Najua nimeuumiza sana moyo wako Darling, Najua nimekufanya ulie sana mke wangu…I know…I know! But please 4give me…I will never hurt you again.”

Mzee Rwakatare alishindwa kuyazuia machozi yasimtoke.Alimvuta mkewe na kumkumbatia kwa nguvu.Bi Patricia hakujibu kitu zaidi ya kumwambia kuwa yote alimwachia Mungu na alishamsamehe kwa sababu anampenda.

“Mwanangu Geneviv yuko wapi? Hebu mwite nimuombe msamaha sababu najua yeye ndiye aliyeumia zaidi”.
“Ngoja nimuangalie chumbani kwake…Aliinuka Bi Patricia kwa kujikongoja na kuelekea chumbani kwa Geneviv.Alishajua kuwa hayupo ila alitaka tu kwenda kuhakikisha.”

****
“Oyaa washkaji eeeh…huyu si ndo yule Cute Angel Geneviv wa sculi kwetu?”
“Ndo mwenyewe mwana! Halafu mi nilikuwa namtamani siku kibao useme ndio alikuwa ananimwaga kila nikimuaproch!”
“Hata mimi nilikuwa namlia taiming siku kibao ila nilikuwa namgwaya si unajua mtoto mwenyewe alivyo juu!”
“Leo kajilengesha kwenye 18 zetu…ful kujisevia”

Hayo yalikuwa ni mazungumzo ya vijana wanne waliokuwa wametoka porini kuvuta bangi baada ya kutoroka shule.Walimkuta Geneviv akiwa amelala chini ya mti kutokana na uchovu wa kukimbia juani akitoroka kwao baada ya kumjeruhi baba yake kwa kumpiga na stuli mpaka akapoteza fahamu wakati akimpiga mama yake.

Akiwa usingizini alisikia sauti za watu wakichekelea kwa furaha.Aliposhtuka alikuta vijana wapatao wanne wamemzunguka na kabla hata hajakaa sawa alijikuta akivamiwa mwilini na kubanwa pale chini kiasi cha kushindwa hata kufurukuta.Mmoja alimziba mdomo huku wengine wakimvua nguo.Kufumba na kufumbua nguo alizokuwa amezivaa zilichanwachanwa na kumuacha akiwa mtupu.Akajua kilichokuwa kinataka kutokea.

Hakuna kitu alichokuwa anakiogopa maishani mwake kama kubakwa.Tangu awe mkubwa hakuwahi kumjua mwanaume hata siku moja na aliapa kujitunza mpaka atakapokuja kuolewa.Hakuwa tayari kuamini kuwa usichana aliokuwa akiutunza kama yai ndio ulikuwa unatolewa kwa aibu na maumivu makubwa namna ile.Alijitahidi kufurukuta lakini wapi,akataka kupiga mayowe ya kuomba msaada lakini hakuweza…akashuhudia kijana wa kwanza akifungua zipu yake na kumuinamia pale chini.Hakuwa na cha kufanya zaidi ya kufumba macho huku akiuma meno.Kilichofuatia ikawa ni maumivu makali kupita kiasi ambayo hakuwahi kuyapata maishani mwake.

Baada ya yule wa kwanza kumaliza, alishuhudia wa pili akijiandaa…akajua huo ndio ulikuwa mwisho wake.Alijikaza mpaka naye akamaliza, akashuhudia watatu naye akijiandaa…akajikuta fahamu zikimtoka polepole kutokana na maumivu makali aliyokuwa anayapata.

Wale vijana waliendelea kumfanyia ushetani ule Geneviv kwa zamu zamu mpaka wote wanne walipotosheka baada ya kurudia karibu mara tatu tatu.Wakamuacha akiwa amepoteza fahamu wakitokomea kusikojulikana.

Geneviv alikuja kushtuka baada ya kuhisi baridi kali ikimpiga.Aliposhtuka akajikuta yuko palepale chini ya mti, huku nguo zake zikiwa zimechanwachanwa.Alitaka kuinuka,maumivu makali yakamrudisha chini.Akawa anajaribu kukumbuka kilichomtokea,akapeleka mkono wake kwenye ikulu yake changa,kulikuwa kumeharibiwa vibaya mno…ndipo hapo kumbukumbu zilipomrudia,alikuwa amebakwa.Alibaki amepigwa na bumbuwazi akitamani hiyo iwe ndoto lakini haikuwa hivyo,ukweli ukabaki kuwa palepale,alibakwa.

Alijaribu tena kuinuka,lakini safari hii alisikia maumivu makali kupita kiasi.Akajilaza chali huku akilia kilio cha kuomboleza.Alijikuta akimchukia mno baba yake mzee Rwakatare kwani bila yeye asingepatwa na tukio baya namna ile.
“I hate my daddy! I hate men, they are Devils”
***********

Baada ya kumkosa chumbani kwake, Bi Patricia alirudi na kumpa mumewe taarifa.
“Atakuwa ameenda wapi? Maskini malaika wangu…”
Aliongea mzee Rwakatare akijifanya kumsikitikia mwanae.Kwa kifupi,zile tofauti zilizokuwepo baina ya Bi Patricia na mumewe zilionekana kama zimekwisha kabisa na sasa wote wakawa wanamfikiria binti yao Geneviv.

Muda ulizidi kwenda bila ya Geneviv kurudi nyumbani.Hawakujua yuko wapi na amepatwa na nini.
“Ningekuwa na nguvu ningeenda kumuulizia kwa wenzake,mwanangu hana tabia ya kuchelewa kurudi nyumbani namna hii! Sijui kapatwa na balaa gani maskini”

aliongea Bi Patricia kwa masikitiko baada ya kuanza kuhisi kuwa huenda mwanae amepatwa na jambo baya baada ya usiku kuzidi kuingia.Mwili wake wote ulikuwa bado una maumivu kutokana na kipigo cha mumewe kiasi cha kumfanya ashindwe hata kutoka nje kwenda kumtafuta mwanae.Saa ya ukutani iliyokuwa mle chumbani ilionyesha kuwa ni tayari saa nne za usiku.
Wasiwasi ulizidi kuwaingia kiasi cha kila mtu kubaki kimya akiwaza kivyake.

“kwani alivyoondoka aliaga anakwenda wapi?”
Mzee Rwakatare aliuliza swali la kijinga kiasi cha kumkumbusha mkewe yaliyotokea asubuhi ya siku ile na kumfanya Geneviv atoroke pale nyumbani bila kuaga.
“Si ujinga wako uliokuwa unaufanya asubuhi,unafikiri mwanao bado mtoto sio, namtaka mwanangu! Amka kamtafute mwanangu…!”
Bi Patricia alianza kucharuka na kumshinikiza mumewe aende kumtafuta Geneviv.Mzee Rwakatare naye hakuweza kutoka nje kwani bado alikuwa na maumivu sehemu ya kichwani baada ya kupigwa na stuli asubuhi.Wakabaki kulaumiana wenyewe kwa wenyewe.Mzee Rwakatare alijihisi kushtakiwa na dhamira yake sana,kwani ukweli aliujua kuwa yeye ndio chanzo cha matatizo na hata kama mwanae angepatwa na jambo baya,basi yeye ndiye aliyemsababishia.Alijikuta akisononeka sana moyoni hasa baada ya kumuona mkewe akizidi kulia kwa kuomboleza.
“Mke wangu jikaze jamani,unavyolia anamchulia mwanetu,atapatwa na matatizo bure,yote tumwachie Mungu”

Mzee Rwakatare alijifanya kuongea kwa busara.Bi Patricia hakuamini kusikia maneno kama yale kutoka kwa mumewe.Ilibidi ainue macho na kumtazama usoni kwa mshangao,alihisi mumewe anamkejeli kwani tangu aachishwe kazi hakuwahi kulitaja jina la Mungu kutoka kinywani mwake zaidi ya matusi ambayo sasa alishaanza kuyazoea.

Waliendelea kutazamana kwa muda mrefu huku kila mmoja akiwa kimya.Masaa yalizidi kuyoyoma na hatimaye saa ya ukutani ikawa inasoma saa sita za usiku. Bi patricia alishindwa kujikaza na akawa anaendelea kulia kwa kilio cha kwikwi.Pia alikuwa akisali kimoyomoyo akimuomba Mungu wake amnusuru mwanae Geneviv.
****
Manyunyu ya mvua yalianza kudondoka huku wingu zito likitanda angani kuashiria mvua kubwa inataka kunyesha.Geneviv alizinduka kutoka usingizini baada ya kuona ameanza kuloana.Aliposhtuka mwili wake ulikuwa ukitetemeka kwa baridi kali ya usiku huku akiwa hajajifunika kitu chochote zaidi ya nguo alizokuwa amezivaa ambazo nazo zilikuwa zimechanwachanwa. Alijaribu tena kuinuka kutoka pale chini na safari hii alifanikiwa kusimama kwani maumivu yalikuwa yamepungua kidogo.Alijaribu kuinua mguu na kupiga hatua lakini akajikuta akishindwa kutembea.
“I must die hard, I need to move out of this place”
(lazima nife kigumu,nahitaji kuondoka mahali hapa)

Alijiambia Geneviv kimoyomoyo wakati akijikaza na kuanza kupiga hatua fupifupi kuelekea barabarani ambako aliamini anaweza kupata msaada.Japokuwa alikuwa akisikia maumivu makali alijitahidi kujikongoja kiupande-upande na akawa anajongea taratibu kuelekea upande iliko barabara. Manyunyu ya mvua yalikuwa yakiongezeka na kuanza kuuloanisha mwili wake mchanga.Kadri manyunyu yalivyokuwa yanaongezeka na kumloanisha ndivyo Geneviv alivyozidi kupata nguvu ya kutembea na kuongeza mwendo. Baada ya kitambo kirefu akawa amefika barabarani.

Hakutaka kupoteza muda zaidi,akaanza kuifuata barabara akiwa haelewi anakoelekea. Hakutamani tena kurudi nyumbani kwao kwani chuki dhidi ya baba yake ilizidi kukua na kumfanya amchukie kama shetani. Akiwa bado anazidi kusonga mbele akielekea asikokujua,aliona mwanga wa taa za gari likija kutokea mbele yake.Hakujua ni gari gani na lilikuwa likielekea wapi ila akapiga moyo konde na kuamua kulisimamisha.

“Haroo afande hebu simamisha ‘Defender’ ,naona kama kuna rimutu rinasimamisha gari,sijui ni rinani na rimetokea wapi usiku wote huu Mura!”

aliongea Koplo Marugu kwa Kiswahili kibovu akimuamuru dereva wake kusimamisha gari.Walikuwa wako katika doria ya usiku pamoja na askari wengine watatu waliokuwa wamekaa nyuma ya gari.

Geneviv aliendelea kulipungia lile gari mikono kwa nguvu zake zote na taratibu akaanza kuliona likipunguza mwendo na kusimama karibu yake.
Liliposimama Geneviv akagundua kuwa lilikuwa ni gari la polisi,alishusha pumzi ndefu na kumshukuru Mungu wake kwani aliamini angekuwa salama mikononi mwa wanausalama wale.Hakutaka kuwaambia ukweli wa kilichomtokea kwani alijisikia vibaya kueleza kuwa amebakwa kwani alihisi ni aibu kubwa kwake.Akaamua kutunga uongo…

Baada ya lile gari kusimama,askari walishuka na kuanza kumhoji ametoka wapi na anakwenda wapi usiku wote ule,ukizingatia yeye ni mtoto wa kike na hapo alipo ni porini.
“Tulikuwa tumetoka shambani na dada,tukavamiwa na watu walioanza kutupiga mpaka wakanichania nguo.Dada alikimbia na kuniacha peke yangu huku.”

Geneviv aliongea uongo mtakatifu huku akitoa machozi na kuwafanya wale askari waamini alichokuwa anakisema.Bila hata kumhoji maswali mengi,walimpakia ndani ya Defender na kuanza kurudi naye mjini ambapo alielezwa kuwa atapewa sehemu ya kulala mpaka asubuhi ambapo ataandikisha maelezo yake kituoni ili watuhumiwa waanze kusakwa.Hakuna hata mmoja aliyehisi kuwa maelezo ya Geneviv ni uongo.

Gari likawashwa na kuanza kurudi mjini.Muda mfupi baadae tayari walikuwa wameshafika kituo kikuu cha polisi cha Blaziniar ambapo Geneviv alikabidhiwa kwa askari wawili wa kiume waliokuwa zamu na wale polisi wengine wakaendelea na doria. Wale askari walimpokea Geneviv na kumuweka kaunta,huku wakijifanya kumuonea huruma. Walimuonyesha sehemu ya kukaa na wao wakaendelea na shughuli zao.

“Haloo afande haka kabinti ni kazuri mno,hebu kaangalie vizuri”
wale askari walikuwa wakinong’onezana kwa sauti ya chini na mara wote wakaanza kumtolea macho Geneviv ambaye alikuwa ameanza kusinzia pale alipokaa na hakuwa na habari kama wale askari wanamtazama kwa macho ya husda.

“Aisee kweli bwana,unajua nilikuwa sijakaangalia vizuri…halafu unajua mke wangu alisafiri wiki ya pili sasa…natamani niwe fataki japo kidogo tu!”

Waliendelea kunong’ona wale askari na wakajikuta wakicheka kwa pamoja na kugongesheana mikono.Kelele za vicheko zilimshtua Geneviv aliyekuwa anasinzia kwenye kiti alichokuwa amekalia.
Mmoja kati ya wale askari aliinuka na kumfuata pale alipokuwa amekaa na kumshika begani.

“Binti naona umechoka sana, pole! amka basi nikakuonyeshe sehemu ya kulala,usiwe na wasiwasi hapa uko mikononi mwa chombo cha dola…tutakulinda mpaka asubuhi”
Aliongea yule askari akimshika mkono Geneviv na kutoka nae nje ya jengo la kituo cha polisi. Geneviv hakuwa na wasiwasi kwani aliamini kazi ya jeshi la polisi ni kuwalinda raia wake. Wakatoka na kuelekea kwenye kibanda kidogo kilichokuwa mita chache pembeni.

****

Hakuna hata mmoja kati ya Mzee Manuel Rwakatare na mkewe Bi Patricia aliyepata hata tone la usingizi. Mpaka inagonga saa nane usiku, Geneviv alikuwa hajarejea nyumbani na hakukuwa na dalili za yeye kurudi. Bi Patricia alikuwa akizidi kulia hali iliyomfanya aanze kuhisi maumivu makali ya kichwa kwani alikuwa bado hajapona. Baada ya kuona mkewe hataki kutulia, ilibidi mzee Rwakatare ajiandae kwenda kutoa taarifa polisi usiku huohuo. Na yeye alionekana kuchanganyikiwa mno, akawa anajilaumu kwa yote aliyoyafanya ambayo ndiyo yaliyopelekea kuibuka kwa tatizo hilo.

Alipiga moyo konde na kujifariji kuwa hakuna binadamu asiyekosea. Baada ya kumaliza kujiandaa alimuaga mkewe ambaye hakumjibu kitu zaidi ya kuendelea kumwaga machozi.Alitoka na safari ya kuelekea kituo kikuu cha polisi cha Blaziniar ikaanza. Ilimbidi abebe mwamvuli kwani mvua nayo ilikuwa imechachamaa kunyesha.Baada ya safari ya takribani dakika arobaini, tayari alishawasili kwenye eneo la kituo cha polisi.

Tangu asimamishwe kazi serikalini,Mzee Rwakatare alikuwa hapendi kabisa kuonekana na polisi kwa kuhofia kukamatwa kwa makosa yake ya uhujumu ambayo bado upelelezi ulikuwa unaendelea, lakini kwa sababu ya mwanae alijikuta hofu ikimuishia. Akawa anapiga hatua za taratibu kusogelea eneo la kituo.

Akiwa hatua chache kabla ya kuufikia mlango mkubwa wa kuingilia kituoni,alisikia sauti ambayo ilimfanya mapigo ya moyo yaanze kumwenda kasi mithili ya injini ya jeti.

Ilikuwa ni sauti ambayo aliitambua vizuri kuwa ni ya mwanae Geneviv ikitokea kwenye kibanda kidogo pembeni ya kituo cha polisi.
Geneviv alikuwa akilalama kwa maumivu makali aliyokuwa anayapata wakati yule askari aliyejifanya kumpeleka kulala akimuingilia kimwili kwa nguvu. Kwa mara nyingine tena, Geneviv alikuwa akibakwa,tena safari hii na Askari polisi.

Mzee Rwakatare hakutaka kuyaamini masikio yake kuwa ile sauti kweli ilikuwa ni ya Geneviv.Ikabidi asogee mpaka karibu ya kile kibanda na kuchungulia ndani kupitia tundu dogo chini ya dirisha.
Hakuyaamini macho yake kwa alichikiona…

“Sh*t, what the hell are you doin with my daughter…im gonna kill you!”
Mzee Rwakatare aliongea kwa hasira kali, na kwa nguvu zake zote aliukanyaga mlango wa kile chumba na kuingia ndani mzima-mzima.

Yule askari alishtuka kuona mlango ukivunjwa na kumharibia starehe yake.Akawa anahangaika kuvaa suruali yake vizuri.
Mzee Rwakatare alimuwahi kwa kipigo kikali cha kushtukiza mpaka yule askari akadondoka chini.Alipotazama pembeni alikiona kipande cha bomba la chuma kilichokuwachini. Alikiokota na kuanza kumuadhibu vikali yule askari kichwani mpaka akazimia.

Kwa haraka alimuinua mwanae Geneviv ambaye bado alikuwa akilia kwa uchungu kutokana na maumivu makali aliyokuwa anayapata huku damu ikimchuruzika kutoka katikati ya miguu yake.Alimuweka begani na akatoka naye kwa spidi ya ajabu na kuanza kukimbia nae kutokomea gizani.

Hakuna askari aliyeelewa kinachoendelea.Mvua nayo ilikuwa ikizidi kupamba moto na sasa zilianza kusikika radi kali zikipiga na kuufanya usiku uzidi kutisha.Mzee Rwakatare hakujali kitu,akawa anazidi kutimua mbio huku Geneviv akiwa begani.
Akiwa umbali wa mita kadhaa,alishtukia kuona anamulikwa na taa za gari lililokuwa likiingia kituo cha polisi. Kwa haraka akamrusha Geneviv chini na yeye akarukia pembeni ya barabara kwenye mtaro.

Kutokana na mvua kubwa iliyokuwa inaendelea kunyesha ikiambatana na ukungu,hakuna mtu yeyote kutoka kwenye lile gari aliyewaona.
Gari ambalo aliligundua kuwa ni la polisi likapita na kuingia pale kituoni.Kwa haraka aliinuka na kumnyanyua mwanae na kumuweka tena begani.Akawa anatimua mbio kurudi nyumbani kwake, safari hii akipitia njia za vichochoroni kukwepa kuonekana tena na polisi.Baada ya kama nusu saa akawa ameshafika nyumbani kwake. Geneviv alikuwa akiendelea kulalama kwa maumivu na hakuelewa kilichofuatia mpaka alipojikuta anaingizwa ndani mwao.

Bi Patricia alishtuka kusikia mlango ukigongwa.
“Nini tena jamani?” Bi Patricia aliuliza kwa sauti iliyokauka kutokana na kulia, na akawa anajikongoja kwa uchovu kwenda kufungua mlango. Alishakata tamaa ya kumuona mwanae Geneviv usiku huo.

“Fungua mke wangu!”
Aliongea mzee Rwakatare kwa sauti iliyomaanisha kuna jambo. Bi Patricia aliharakisha kufungua mlango.
“Ooooh My God!.....”
Bi Patricia alishtuka kupita kiasi.
“What happened to my daughter,oooh…”
Kwa haraka akampokea Geneviv huku mwili wote ukimtetemeka. Akampeleka chumbani kwake na kumlaza kitandani huku mumewe akianza kuhangaika kutafuta huduma ya kwanza. Kila mtu akawa kama amechanganyikiwa, na zaidi Bi Patricia ambaye bado alikuwa hajajua nini kimemtokea mwanae. Kengele ya hatari ikalia kichwani mwa Bi Patricia wakati akiendelea kumchunguza Geneviv ambaye alikuwa hajitambui.

Kitu cha kwanza alichoshtushwa nacho ni kuona jinsi nguo za mwanae zimechanwa-chanwa. Akiwa bado anamchunguza akashtushwa na damu zilizoiloanisha sketi ya mwanae, mapigo ya moyo yakaanza kumwenda mbio…hakutaka kuamini haraka kuwa anachokihisi ndicho kilichomtokea mwanae.

Alitamani iwe ndoto lakini naye hakuweza kuubadili ukweli,akajikuta akipiga yowe kubwa na kuanza upya kuomboleza baada ya kubaini kuwa ni kweli mwanae alifanyiwa ushetani na wanaume.

“Cant believe this…I cant! Unaona ulichomsababishia mwanangu, haya furahi sasa malengo yako yametimia, ooh my Lord!”
Bi Patricia akawa anampiga-piga mumewe mgongoni huku akilia kwa uchungu. Akawa anamlalamikia kuwa yeye ndio chanzo cha yote.

“Mke wangu acha kunilaumu, mbona nimekiri makosa! Cha msingi kwa sasa tusaidiane kuokoa maisha ya geneviv, huu sio muda wa lawama.”
Bi Patricia alikuwa mgumu wa kuelewa na akazidi kulia kwa sauti kubwa kiasi cha kuwaamsha majirani ambao baada ya muda mfupi walikusanyika nje.Baada ya majadiliano ya muda mfupi,muafaka ukafikiwa kuwa Geneviv apelekwe hospitali haraka usiku huo huo.Kila mtu alimuonea huruma.

Jirani mmoja akajitolea kutoa gari lake na kwa haraka Geneviv akabadilishwa nguo na safari ya kwenda hospitali ikaanza mara moja. Japokuwa mvua kubwa ilikuwa inaendelea kunyesha hakuna aliyeonekana kujali, kila mtu akawa anahangaika kuokoa maisha ya Geneviv.

Baada ya kitambo kifupi, gari walilompakia mgonjwa likakwama kwenye matope kutokana na mvua kubwa iliyokuwa inaendelea kunyesha, hali iliyowalazimu mzee Rwakatare na dereva waanze kusaidiana kulitoa gari pale lilipokwama.Baada ya kuhangaika kwa muda mrefu bila mafanikio, huku hali ya Geneviv ikizidi kuwa mbaya, Mzee Rwakatare akaamua kumbeba Geneviv na kuendelea na safari ya kuelekea Hospitali.

“Lakini mvua hii ni hatari kwa mgonjwa, ukizingatia bado radi zinapiga sana, kwanini tusiendelee kulihangaikia gari?”
Dereva alitoa ushauri ambao Mzee Rwakatare alishindwa kuuafiki. Akamuinua mwanae na kumuweka begani na safari ikaendelea. Bi Geneviv naye akashuka na kuanza kuwafuata kwa kukimbia huku akizidi kulia. Dereva akabaki ameduwaa akiwaonea huruma kwa yaliyowakuta.

Baada ya safari ndefu na ngumu, hatimaye walifika kwenye hospitali ya planet Health Aid ambako walipokelewa na manesi waliokuwa zamu na upesi upesi Geneviv akawekwa juu ya kitanda cha wagonjwa na kuanza kukimbizwa kuelekea wodini. Kwa haraka akaanza kupewa huduma ya kwanza. Baada ya muda mfupi alitundikiwa dripu za maji ambazo zilikuwa zikitiririka kwa kasi kuingia mishipani mwake. Saa ya ukutani ya pale hospitali ilionyesha kuwa tayari ni saa kumi ya alfajiri.

Mzee Rwakatare na mkewe wakabaki nje ya wodi wakiwa wamekaa kwenye viti sehemu ya mapokezi huku kila mmoja akiwa amejiinamia kimya. Baada ya muda mfupi nesi akatoka wodini akiwa na faili mkononi mwake na kumuita mzee Rwakatare pembeni.

“Pole mzee!” yule nesi alimpa pole mzee Rwakatare na kabla hata hajajibu kitu akaendelea kuongea…
“Mgonjwa anaendelea kupata huduma ya kwanza na muda si mrefu atazinduka. Uchunguzi wetu umebaini kuwa amebakwa, na kwa taratibu za hospitali zote nchini ni kwamba mgonjwa wa namna hii lazime apitie kituo kikuu cha polisi kuchukua PF3 kwanza ndipo atibiwe, ila kwa kuwa mgonjwa wenu alikuwa na hali mbaya tukaona ni bora tuendelee kumpa huduma ya kwanza, ila matibabu ataanza kupewa baada ya w ewe kuleta hiyo PF3”

Alimaliza kuongea yule nesi na kurudi wodini akimuacha Mzee Rwakatare ameduwaa asijue la kufanya.
Bi Patricia aliinuka haraka na kumfuata yule nesi kabla hajaingia ndani na akawa anamhoji hali ya mgonjwa.

“Maelekezo yote nimempa mzee, nenda atakueleza vizuri”
Aliongea yule nesi kwa kifupi huku akifunga mlango.

Bi Patricia alirudi kwa mumewe aliyeonekana kuchanganyikiwa, akamshika mkono na kumkalisha chini huku akiwa na shauku ya kutaka kujua yule nesi alimwambia nini.

Ukweli ni kwamba tangu usiku alipomuokoa mwanae, mzee Rwakatare alikuwa hajamwambia chochote mkewe juu ya jinsi alivyomuokoa na mazingira aliyomkuta kutokana na hali aliyokuwa nayo mkewe. Ilibidi aanze kumueleza tangu mwanzo jinsi alivyomuokoa Geneviv kabla ya kumwambia maelekezo aliyopewa na yule nesi.
Baada ya kumaliza maelezo marefu, wote walishusha pumzi ndefu wakabaki wakitazamana wasijue nini cha kufanya.

“Sasa tutafanya nini mume wangu, tukizidi kuzubaa tutampoteza mtoto wetu…please do something to save her.”
“Sasa wewe unafikiri mi ntafanya nini, Polisi siwezi kwenda kwa sababu hao ndio walioniharibia mwanangu, isitoshe nimesababisha madhara pale kituoni.Huoni kuwa nikienda nitakuwa nimejipeleka mwenyewe? I cant report anything to them. They are all rotten.”

Mzee Rwakatare na mkewe waliendelea kubishana kuhusu kwenda kuchukua PF3 kama walivyoelekezwa na yule nesi. Mwishowe walifikia uamuzi wa kutokwenda. Wakaamua kumueleza yule nesi ukweli kuwa mtoto wao alibakwa na Polisi haohao hivyo haikuwa na maana kwenda tena kwao kuomba kibali.

“Lakini vipimo vyetu vinaonyesha kuwa amebakwa na watu si chini ya watano, nyie mlikuwa wapi mpaka mtoto anafanyiwa ukatili mkubwa namna hii” Yule nesi alizidi kuongea kwa msisitizo huku akionekana kuwatupia lawama wazazi kwa kushindwa kumlinda binti yao.

“Nesi sio kweli, mwanangu hajabakwa na watu watano, no! mbona bado mdogo,au mmekosea vipimo…Ooh my God! I cant believe th..i…s….”
Bi Patricia alikuwa akimbishia nesi wakati akielezwa ukweli wa yaliyomkuta mwanae huku akilia. Mzee Rwakatare alibaki ameduwaa na yeye akiwa haamini alichokisikia kutoka kwa nesi.

“Anyway, cha msingi we tusaidie mtoto atibiwe,mengine tutazidi kuelekezana taratibu.”

Mzee Rwakatare aliongea kwa kukata tamaa na kwa bahati nzuri yule nesi aliwaelewa. Akarudi wodini na kuanza kumpa matibabu Geneviv ambaye fahamu zilikuwa bado hazijamrudia.

Si mzee Rwakatare wala mkewe waliokuwa tayari kuamini kuwa ni kweli mtoto wao amebakwa na watu zaidi ya watano. Mzee Rwakatare alishindwa kuyazuia machozi yasimtoke, ikawa ni zamu ya mkewe kumbembeleza. Alikuwa akijihisi mwenye hatia kubwa sana mbele ya mwanae na mkewe na zaidi mbele ya Mungu.

Alianza kuamini sasa kuwa ni kweli pombe badala ya kupunguza matatizo ilikuwa ikiongeza.Alijilaumu sana kwa ujinga alioufanya na kumsababisha madhara makubwa namna ile.
“One mistake, five goals…F*ck me because im the source…”
Alikuwa akijisemesha peke yake kama mwendawazimu huku akijipigapiga kichwani.

*****
Mpaka inafika saa mbili asubuhi Geneviv alikuwa bado hajazinduka hali iliyoanza kuwatia hofu hata wale manesi.

“It seems she has been severely damaged in her genitals, Hydro-saline therapy is over and yet the condition is still worse. Lets call the Doctor for emergency”
(Inaonekana ameumizwa sana, dawa tulizompa zinaisha lakini bado hali ni mbaya, inabidi tumuite daktari kwa huduma ya dharula)

Wale manesi waliokuwa wanamhudumia Geneviv tangu usiku walikuwa wakijadiliana nini cha kufanya baada ya kuona hali ya mgonjwa inazidi kuwa mbaya kadri muda ulivyokuwa unaenda. Ikabidi Geneviv ahamishiwe chumba cha wagonjwa mahututi I.C.U (Intensive care unit) ambako alianza kupewa huduma ya dharula ili kuokoa maisha yake.

“Inject her the Ant-spermatids serum, then add Oestrogen 20mls into Hydro-saline therapy… If this will fail to awake her, it will be out of our control”

(Mchomeni sindano ya dawa ya Ant-spermatid, kisha ongezeni mililita 20 kwenye dripu yake yenye dawa… kama bado atashindwa kuzinduka basi itakuwa nje ya uwezo wetu)

Aliongea daktari Bingwa wa magonjwa ya kina mama na watoto, Dokta Barikieli Zayumba akiwaelekeza manesi namna ya kufanya. Kwa muda wote huo, Bi Patricia na mumewe walikuwa wameshikana mikono nje wakiomba sala mfululizo, wakimuomba Mungu wao amnusuru Geneviv

****
Masaa mawili tangu Geneviv abadilishiwe dawa na kupewa dawa za mwisho za kuokoa uhai wake, mapigo yake ya moyo ambayo yalikuwa chini sana yalianza kuongezeka taratibu na kurudi kwenye hali yake ya kawaida. Mara akafumbua macho na kuanza kupepesa huku na kule kama anayejiuliza hapa niko wapi…

“Doctor, she is back to her counciousness, she is awake”
(dokta, mgonjwa amerudiwa na fahamu, ameshaamka…)

Aliongea kwa sauti nesi aliyekuwa akimhudumia akimfuata daktari ambaye naye alisogea pembeni ya kitanda cha Geneviv na kuanza kumpima mapigo ya moyo.
“Unajisikiaje binti? Daktari alimuuliza Geneviv kwa upole huku akimgusa usoni kupima joto la mwili wake!”
Geneviv hakujibu kitu, akawa kama anajitahidi kukumbuka jambo fulani.Baada ya kama dakika tatu tangu fahamu zimrudie, Geneviv alianza kuongea.
Kauli ya kwanza aliyoitoa ilikuwa ni kuuliza aliko mama yake.

“Where is my mum? I need to see her…I need to see my mum”
Aliongea Geneviv na kuanza kushinikiza mama yake aletwe.Ilibidi Bi Patricia aende kuitwa pale nje alipokuwa amekaa. Mzee Rwakatare naye hakutaka kubaki peke yake, akawa anang’ang’ania na yeye aingie wodini.
“Lakini amesema anataka kumuona mama, sio baba” yule nesi alitahadharisha kabla ya kuwaruhusu kuingia. “Hamna tatizo nesi, huyu ndio baba yake, mwache tu tuingie nae”
Aliongea Bi Patricia akimtetea mumewe.Wakaruhusiwa kuingia. Baada ya kumuona mama yake, Geneviv alianza kulia kwa nguvu, Bi Patricia akainama pale kitandani na kuanza kumbembeleza.
“Calm down my dear, everything is going to be right. We love you and we pray for you, get well soon!” (Tuliza nafsi yako mwanangu, kila kitu kitakuwa sawa.Tunakupenda na tunakuombea upone haraka)
Mzee Rwakatare alikuwa amesimama nyuma kabisa na akawa anasogea taratibu. Baada ya kubembelezwa na mama yake, Geneviv alianza kutulia. Alipomuona baba yake tu, ikawa shughuli pevu…Geneviv alianza upya kupiga kelele huku akitoa maneno makali kwa baba yake.

“Get out of here dady, I hate you, I hate men…”
( Ondoka humu ndani baba, nakuchukia, nawachukia wanaume…)
Hakuna aliyeamini kumsikia mgonjwa akitoa maneno makali namna ile kwa baba yake mzazi.Pamoja na kujitahidi kwa kadri ya uwezo wake wote kuokoa maisha ya mwanae, bado Geneviv alikuwa akimchukia mno baba yake, hasa kutokana na vitendo vya kinyama alivyoshuhudia akimfanyia mama yake siku chache zilizopita, na matatizo aliyomsababishia mpaka akawa hapo hospitali.Hakujua kuwa ni baba yake huyohuyo ndiye aliyemuoka kutoka kwenye mdomo wa samba.

Mzee Rwakatare akawa anaomba radhi kwa mwanae akionyesha kuwa amebadilika na hata rudia tena kuwafanyia mabaya yeye na mama yake. Hakuna lililomuingia akilini, akawa anazidi kupiga kelele mpaka madaktari wakaingilia kati na kumtoa nje mzee Rwakatare. Alikubali kutoka huku moyo wake ukiwa umefedheheka mno. Akawa amejiinamia huku akijitahidi kuyaficha machozi.
Bi Patricia akawa na kazi ya ziada ya kumuelewesha mwanae kuwa baba yake amekiri makosa na ni yeye ndiye aliyemuokoa usiku wa manane na kumrudisha nyumbani kisha kumleta pale Hospitalini. Kidogo akaanza kuelewa, ingawa kwa shingo upande.

“Kwani umemfanya nini mwanao mpaka akuchukie kiasi hiki? Unaona baada ya wewe kutoka tu, ametulia!”
Alihoji daktari Barikieli Zayumba akiwa amesimama pale alipojiinamia mzee Rwakatare. Hakuwa na jibu la kutoa zaidi ya kumuangalia daktari kwa huruma. Wakati wanaendelea kutazamana usoni, Daktari alionyesha mshangao wa wazi-wazi baada ya kugundua kuwa kumbe aliyekuwa akiongea nae ni yule Manuel Rwakatare aliyekuwa afisa katika wizara ya madini na nishati kabla ya kusimamishwa kazi na mheshimiwa Raisi.Vyombo vyote vya habari asubuhi ile vilikuwa vikimzungumzia yeye ingawa mwenyewe alikuwa bado hajajua kinachoendelea kutokana na kumhangaikia mwanae Geneviv.

“Ebwana wewe si ndio yule mzee Rwakatare wa wizarani?” Aliuliza daktari kwa mshangao mkubwa. Mzee Rwakatare hakuelewa ni kwa nini ameulizwa swali lile. “Mimi ndiye, kwani…”
Alijibu kwa mkato akitaka kumkatisha asiendelee kumhoji maswali mengi.

“Umesikia kilichotokea usiku pale kituo kikuu cha polisi cha Blaziniar?”
Daktari Barikieli alizidi kumdadisi mzee Rwakatare. Kusikia swali lile alijikuta moyo ukimlipuka pyaaaa! “Aah aah,sijasikia kwani kumetokea nini” alidanganya mzee Rwakatare huku akibabaika. Ilibidi daktari amchukue mpaka ofisini kwake ambako baada ya kukaa, alimtolea gazeti lililotoka asubuhi ileile na kumpa asome mwenyewe.
“Mungu wangu!” Mzee Rwakatare alijikuta akitamka kwa sauti kubwa na kulidondosha lile gazeti chini. Ilikuwa ni habari ambayo hakuelewa yeye amehusishwa vipi. Ilisomeka hivi…

“UJAMBAZI KITUO KIKUU CHA POLISI- ASKARI AULIWA, SILAHA ZAIBWA! RWAKATARE AHUSIKA, ANASAKWA NA POLISI…”

Chini ya kichwa cha habari ile kulikuwa na maelezo ambayo yalieleza kuwa majambazi yenye silaha yamevamia kituo kikuu cha polisi usiku wa manane na kumuua polisi mmoja aliyekuwa zamu, kisha kuvunja stoo ya silaha na kuiba idadi kubwa ya silaha. Habari ilizidi kueleza kuwa, kitambulisho cha mmoja wa majambazi kimeokotwa eneo la tukio na mtu huyo ametambulika kwa jina la Manuel Rwakatare ambaye aliwahi kuwa muajiriwa serikalini kabla ya kusimamishwa kazi. Kulikuwa pia na picha ambayo ilimuonyesha mzee Rwakatare ikiwa na maandishi makubwa juu yake “MOST WANTED”, na taarifa ikazidi kueleza kuwa anatafutwa kwa udi na uvumba, na zawadi nono itatolewa kwa yeyote atakayesaidia polisi kumkamata jambazi huyo hatari.

Mzee Rwakatare alihisi kama akili inaacha kufanya kazi na kutengana na mwili, akawa kama anayeota ndoto za mchana. Alipojikagua mifuko yote akagundua kuwa ni kweli alipoteza kitambulisho, lakini ni wakati anamuokoa mwanae aliyekuwa akibakwa na polisi na si vinginevyo kama habari ile ilivyoeleza.

“Noo! Noo! Mimi sio jambazi, wamegeuza maneno, Noo! Sio mimi…”
Aliongea mzee Rwakatare kwa sauti kubwa huku akivua shati lake na kulitupa chini, kisha akaanza kukimbia kutoka nje ya ofisi kama mwendawazimu. Daktari Barikieli alibaki ameduwaa akimsikitikia mzee mwenzake.
Mara wakaanza kusikia ving’ora vya magari ya polisi yakija na kuizunguka hospitali yote. Mzee Rwakatare akawa kama aliyepagawa, akawa anakimbia huku na kule akitafuta sehemu ya kutokea bila mafanikio. Akajua huo ndio mwisho wake…

Akaona kitu pekee ni kurudi wodini kumuomba msamaha mwanae kwa mara ya mwisho kwani alijua hawezi kusalimika kutoka kwenye mkono wa sheria zilizopindishwa kuwalinda wachache. Kabla hata hajaufikia mlango wa wodi aliyolazwa mwanae Geneviv, alisikia amri kali kutoka kwenye kipaza sauti cha gari la polisi iliyomtaka asimame palepale alipo na kuinua mikono juu. Hakuwa na cha kufanya zaidi ya kusalimu amri huku akipiga kelele,

“mimi sio jambazi, mnanionea bure! Nilikuwa namuokoa mwanangu… I was saving my Geneviv…” Alipiga kelele kwa nguvu kiasi cha kuwafanya waliokuwa wodini kushtuka.Wale Polisi hawakuonekana kujali anachokizungumza, wakamkamata na kumfunga pingu mikononi na miguuni, kisha akabebwa juu juu kama mzigo na kupelekwa lilikopaki karandinga la polisi. Akarushwa ndani kama mzigo kisha milango ikafungwa na gari likaanza kuondoka likisindikizwa na msafara mrefu wa magari ya polisi.

Alipochungulia nje kupitia nyavu za lile karandinga, alimuona mkewe akitoka nje ya wodi huku akikimbia kuyafuata yale magari.
Kwa mbali alisikia mkewe akilia kwa kupiga kelele huku akisisitiza kuwa mumewe hakuwa jambazi, lakini askari waliokuwa chini walimsukuma kwa nguvu, na akashuhudia akidondokea pembeni ya barabara. Alijikuta akimwaga machozi kama mtoto.

Msafara ule uliongoza mpaka gereza kuu la Blaziniar, ambapo Rwakatare alishushwa na kuingizwa gerezani chini ya ulinzi mkali, eneo lote likiwa limezingirwa na polisi wenye silaha na mbwa wa kijeshi. Bado alikuwa haamini kama kweli yanayotokea ni kweli, aliyafananisha na filamu za Mel Gibson.
Aliingizwa mpaka vyumba vya ndani kabisa vya gereza lile, na akafungiwa kwenye chumba kidogo chenye giza.

“Im finished… im gone! Ooh My Lord rescue me from this hell…”
Aliongea Mzee Rwakatare huku akimwaga machozi kama mtoto mdogo, akakaa chini na kuegamia ukuta mchafu wa kile chumba kilichokuwa kikitoa harufu kama choo cha stendi… alitia huruma.
Baada ya kuingizwa ndani ya gereza kuu chini ya ulinzi mkali na kufungiwa kwenye chumba kidogo chenye giza, ndani kabisa ya gereza, matumaini ya kutoka uraiani yanamuishia kabisa Mzee Rwakatare. Kwa jinsi ambavyo anazijua sheria za nchi yake, ilikuwa vigumu sana kwa yeye kuachiwa huru hata kama ukweli haukuwa kama ulivyoelezwa. Ukweli halisi usingeweza kufahamika haraka kutokana na Sheria za nchi kuwa zinachezewa na kupindishwa kwa maslahi ya wachache na kuwaacha maelfu ya raia wakiteseka bila hatia.

Matukio ambayo mwenyewe aliyatafsiri kama mikosi yalikuwa yamemwandama kiasi cha kuielemea nafsi yake. Ni ndani ya muda mfupi sana maisha yamebadilika kabisa, kila kitu kimebadilika kwa kiasi cha kusikitisha. Kwake ni kama mchezo wa kuigiza… tangu aliposimamishwa kazi kwa tuhuma ambazo bado zilikuwa zikifanyiwa upelelezi za uhujumu wa nchi akiwa kwenye ofisi ya madini na nishati, kila kitu kilipoteza mwelekeo na kuharibika mpaka alipojikuta ndani ya kuta za gereza kuu. Hakuwa na la kufanya zaidi ya kuukubali ukweli.

“Jifunze kupokea matatizo kwa moyo mkunjufu bila ya kinyongo, kama unavyopokea furaha”
Maneno hayo yalikuwa yakijirudia rudia kichwani mwake, lakini hakuweza kuhimili kuipokea misukosuko ile kwa moyo mkunjufu kwanialiona inamzidi uwezo.

“God, where are you? Why do you allow this to happen to me and my family? Why me?...”
(Mungu uko wapi?, kwa nini unaruhusu haya yanipate mimi? Kwa nini mimi?)

Alijikuta machozi yakimbubujika kama chemchemi ya maji.
Hakukuwa na matumaini tena ya kusalimika, kilichobaki ikawa ni uvumilivu kwenye mateso. Aliamini huo ndio ulikuwa mwisho wa kila kitu katika maisha yake…

Baada ya kushuhudia mumewe akiwa ndani ya karandinga la polisi akipelekwa gerezani, Bi Patricia almanusra apoteze fahamu pale hospitalini. Tangu alipoanza kuishi na mumewe miaka takribani kumi na tano iliyopita hakuwahi kuhisi kuwa itafika muda kila kitu katika maisha yao kitavurugika na kupoteza mwelekeo kama ilivyokuwa inatokea kwa sasa.

Mumewe hakuwa jambazi wala muuaji kama alivyokuwa akiandamwa na vyombo vya habari na polisi. Aliamini kwa asilimia zote kuwa Mungu alikuwa akiwapima imani na kuona ustahimilivu wao katika mapito magumu kama yale. Hakuyaamini yale aliyoyaona yameandikwa kwenye gazeti kumhusu mumewe. Alirudia tena na tena kuisoma habari ile lakini haikumuingia akilini. Alishindwa kuficha kilichokuwa kinaendelea moyoni mwake, huzuni ya kuonewa.

Dokta Barikieli Zayumba ilibidi aingilie kati na kuanza kumdadisi kwa undani Bi Patricia. Ni kweli kuwa tayari mzee Rwakatare alikuwa mikononi mwa dola na matumaini ya kutoka hayakuwepo kutokana na uzito wa kesi aliyobebeshwa. Lakini je
yaliyosemwa na kuandikwa na vyombo vya habari ndiyo yaliyokuwa yametokea?

Kwa haraka haraka hata raia asiyejua sheria angeweza kubaini kilichokuwa kinaendelea, sheria ilikuwa inapindishwa. Geneviv alikuwa hospitalini kwa matatizo aliyosababishiwa na wanaume (wakiwemo polisi), na hakukuwa na mtu mwingine zaidi ya manesi na madaktari waliofahamu ukweli wa kilichomsibu. Leo harakati za kuokolewa kwake zinageuzwa na kuripotiwa kuwa ni ujambazi…Ilikuwa ni utata mtupu.

Bi Patricia ilibidi amueleze daktari Zayumba kilichotokea kuanzia mwanzo mpaka mwisho. Baada ya kumueleza kwa undani hali halisi ilivyokuwa, alipata picha kamili.

“Lakini hawa polisi wataendelea kunyanyasa raia wasio na hatia mpaka lini? Kazi yao ni kutulinda au kutukandamiza?”
Alikuwa akihoji kwa masikitiko Dokta Barikieli Zayumba . Alijikuta akiingiwa na huruma ya kibinadamu.

“Tunaweza kuwashinda hawa, cha msingi twende tukaongee na binti yenu Geneviv kama atakuwa tayari kutoa ushahidi wa kumkomboa baba yake, basi tutashinda, Mungu yu pamoja nasi…”

Alitoa ushauri Daktari, lakini Bi Patricia alishindwa kuafiki kwa jinsi alivyomfahamu Geneviv.
“Dokta ahsante kwa kuonyesha kuwa upo pamoja nasi. Nimjuavyo mwanangu hawezi kumsaidia baba yake kwani bado anamchukia mno… tuache tu mungu ndiye atakayejua namna ya kutunusuru”

Kauli ile haikumvunja nguvu daktari ambaye sasa alionesha nia ya kutaka kuwasaidia. Waliendelea kuzungumza kwa muda mrefu na hatimaye daktari Zayumba ikabidi achukue jukumu la kumpa tiba ya kisaikolojia Geneviv, kwani ilionekana anamchukia baba yake kwa sababu ya kuumia mno kisaikolojia.

Daktari alizidi kumweleza Bi Patricia kuwa hali kama ya mwanae huwatokea watoto wengi wanaoshuhudia mateso ya kikatili wanayofanyiwa mama zao na kama wasipopata msaada wa kisaikolojia huja kuwa hatari katika maisha yao ya baadae. Baada ya mazungumzo ya muda mrefu, hatimaye Daktari na Bi Patricia walitoka ofisini na kwenda wodini alikolazwa Geneviv ambaye sasa alikuwa amepata nafuu kubwa na aliweza hata kukaa kitandani mwenyewe. Daktari Zayumba alitumia mbinu zake zote za kidaktari na kisaikolojia kumshawishi Geneviv kutomchukia tena baba yake, na baada ya kuzungumza naye kwa muda mrefu hatimaye chuki yote aliyokuwa nayo kwa baba yake iliisha. Kwa muda wote huo walikuwa bado hawajamwambia kuwa baba yake tayari yuko gerezani.

“Do you hate your daddy anymore?”
Aliuliza Bi Patricia huku akimkumbatia mwanae ambaye sasa alianza kuonyesha kuchangamka.
“I love my daddy, I don’t hate him anymore! I’ve learn to forgive and forget…I love him!”

Aliongea Geneviv kwa furaha huku naye akimkumbatia mama yake. Daktari Zayumba alikuwa amesimama pembeni akifurahia mafanikio mazuri ya kazi yake aliyoifanya. Hiyo ilikuwa ni hatua muhimu sana katika safari ya kumkomboa mzee Rwakatare kutoka mikononi mwa sheria zilizopindishwa. Kwa pamoja walimtanguliza Mungu kuhakikisha kuwa haki inachukua mkondo wake na kumuacha huru mzee Rwakatare. Baada ya kumuweka sawa Geneviv, Daktari na Bi Patricia walitoka tena nje na kuelekea ofisini ambako bila ya kupoteza muda walianza kuandaa ushahidi wa kitaalamu ambao ungemtoa gerezani mzee Rwakatare. Walipanga kufichua uovu wa jeshi la polisi kwa kitendo walichomfanyia Geneviv.

Mpango madhubuti ukaanza kuandaliwa chini ya usimamizi wa daktari Zayumba. Kitu cha kwanza walichokifanya ilikuwa ni kutafuta vielelezo muhimu kama cheti cha daktari na vipimo vya awali alivyochukuliwa Geneviv wakati alipofikishwa hospitalini hapo akiwa hajitambui.
“Lakini vipimo vinaonyesha kwamba alifanyiwa kitendo hicho na watu zaidi ya watano, hebu kajaribu kumuuliza kama anaweza kuwakumbuka wote vizuri ili maelezo yetu yasije kupishana”
Daktari Zayumba alitoa hoja ya msingi ambayo Bi Patricia aliiona kuwa inafaa kufanyiwa kazi mapema. Akatoka na kwenda wodini alikokuwa amelazwa Geneviv. Ilibidi atumie mbinu za kiutu uzima kuweza kuufahamu ukweli wa wahusika halisi wa tukio bila ya kumuumiza tena mwanae. Alianza kwa kumueleza yaliyomsibu baba yake mpaka akapelekwa gerezani. “Alikuwa anakuokoa wewe kwa hiyo wewe ndio mtu pekee unayeweza kusaidia akaachiwa huru, nakuomba sana mwanangu tusahau yote aliyotufanyia daddy, tuungane kumsaidia atoke gerezani”Bi Patricia alikuwa akimsihi mwanae.

Geneviv alimuonea huruma baba yake kiasi cha kutoa machozi na akaahidi kufanya kila linalowezekana kumsaidia baba yake.
“Nimekuelewa mumy, niko tayari kufanya lolote kumtoa daddy Gerezani. Mwalimu wetu alitufundisha kuwa gerezani ni kubaya, kuna chawa, viroboto na kunguni, halafu hakuna hewa ya kutosha…daddy akikaa sana atakuwa na upele na magonjwa ya ngozi…” Aliongea Geneviv kwa huzuni. Ni wazi kuwa naye alifahamu hatari iliyokuwa inamkabili baba yake.
Lakini Bi Patricia alipozidi kumdadisi kama anawakumbuka wote waliohusika, Geneviv alisita kusema ukweli ambao hakuna mtu mwingine aliyekuwa anaufahamu zaidi yake. Kabla ya kufanyiwa unyama ule na polisi, tayari alikuwa amefanyiwa na wanafunzi wenzake anaosoma nao Shule moja. Kueleza kila kitu kulimaanisha kuwa hata wale wanafunzi nao lazima wangesakwa na kutiwa mikononi mwa sheria kitu ambacho hakutaka kitokee.
Aliamini wale walifanya vile kwa sababu ya uvutaji bangi ambao kwao ilikuwa adhabu tosha. Kama angewataja ingemaanisha kuwa wangefukuzwa shule na kufungwa miaka mingi Gerezani hivyo kuwaachia huzuni ya kudumu wazazi wao na wanafunzi wenzao. Alijikuta akiwaonea huruma kiasi cha kudondosha machozi. Hakutaka jambo lolote baya liwatokee hasa baada ya kujifunza kuwa usilipe ubaya kwa ubaya kwani madhara yake huwa makubwa kuliko unavyotarajia. Akaapa kuwalinda kwa kutowataja.
Lakini bado alishaahidi kuwa atasaidia baba yake atolewe gerezani, hilo lilikuwa jambo lingine zito lililousumbua moyo wake. Alichokifanya ni kumbembeleza mama yake kuwa Daktari asiandike kama alibakwa na watu watano kwani hiyo ingefanya watu wazidi kumuonea huruma na wengine wazidi kumdharau hasa wanafunzi wenzake. Bi Patricia alimkubalia mwanae bila kujua kuwa ameficha siri nyingine.
Akamuomba amsimulie tukio zima jinsi lilivyokuwa ili na yeye amsaidie mawazo ya namna ya kujieleza.
Geneviv alianza kueleza…
“Siku ile nilivyoondoka nyumbani nilikimbilia porini na nikawa sitaki kurudi nyumbani kwa sababu nilimchukia baba halafu nilidhani nimemuumiza sana nilipompiga na stuli kichwani. Nikawa nakimbia kuelekea nisikokujua mpaka nikafika mbali na nyumbani. Nilipoona nimechoka nikaamua kupumzika chini ya mti…”
Alipofikia hapo kuelezea ilibidi aongee uongo kidogo ili kuuficha ukweli wa wale wanafunzi wenzake.Akaendelea…
“Nilipokuja kushtuka nikakuta giza limeshaingia na mvua inanyesha. Nikaamka na kukimbilia barabarani ambako nilianza kutembea kufuata barabara. Baadae nikaona gari linakuja nikaamua kulisimamisha, kumbe lilikuwa ni la polisi. Nikawaambia kuwa wanisaidie nirudi nyumbani… wakanipakiza kwenye gari mpaka pale kituo kikuu cha polisi”
Geneviv alikuwa akieleza kwa ufasaha kabisa, Bi Patricia akawa anamsikiliza kwa makini huku akiwa na shauku kubwa ya kutaka kujua kilichoendelea.Akaendelea tena…
“Tulipofika kituoni walinishusha na kunikabidhi kwa polisi wengine wawili tuliowakuta pale ndani. Wale wengine wakaondoka na kuniacha na wale wawili. Baadae mmoja alikuja akanishika mkono akidai anaenda kunionyesha sehemu ya kulala.Tukaingia kwenye kichumba cha nje pembeni ya kituo. Tulipoingia ndani alifunga mlango na kuniambia nikipiga kelele ataniua na bunduki. Mi sikujua anataka kufanya nini, nikaona anavua suruali yake halafu akaniziba mdomo. Akawa anani… Geneviv alishindwa kumalizia na akawa analia kwa kwikwi. Alikuwa amekumbuka maumivu yaliyoanza kupoa moyoni mwake. Bi Patricia akawa anambembeleza mwanae huku naye akijifuta machozi.Baada ya kutulia akaendelea kusimulia…
“Yule mmoja alipomaliza alitoka nje akanifungia mlango, halafu akaja mwenzake. Na yeye akanifanyia kama yule wa kwanza…nilishindwa kuvumilia nikaanza kulia kwa sauti lakini akaendelea. Mara nikasikia sauti kama ya daddy nje, halafu mlango ukavunjwa. Kweli alikuwa ni daddy na hata sijui alitokea wapi. Akaanza kumpiga yule polisi mpaka akaanguka chini. Daddy akanibeba begani tukatoka nje ambako mvua ilikuwa ikinyesha sana.
Akaanza kukimbia huku amenibeba begani… baada ya hapo sikumbuki kitu mpaka nikajikuta niko Hospitali nimelezwa kwenye kitanda…” Alimalizia kueleza Geneviv huku akijifuta machozi yaliyokuwa yameuloanisha uso wake. Ulikuwa ni ushahidi mzito ambao yeyote ambae angeusikia angemwonea huruma na kulilaani jeshi la polisi lililopewa jukumu la kuwalinda raia na badala yake likageuka na kuwafanyia ukatili mkubwa kama huo wa Geneviv.


Bi Patricia akawa anaendelea kumbembeleza na kumsisitiza kuwa mtu mwingine akija kumuuliza aeleze kama alivyomueleza bila ya kusahau kitu.
Baada ya hapo Bi Patricia alitoka na kwenda ofisini kwa daktari Zayumba ambako alimueleza kwa undani mkasa mzima ulivyokuwa na wakawa wanaendelea kujadili nini cha kufanya.
“Mi nafikiri tumfuate Raisi Ikulu tukamweleze hali halisi labda atatusaidia kwa sababu Raisi huyu mpya ni mpenda haki na huwa hachagui maskini au matajiri,anawasikiliza wote wenye shida.”
Wazo hilo lilipingwa vikali mno na Daktari Zayumba ambaye alieleza wasiwasi wake peupe kuwa swala hilo lisingeshughulikiwa zaidi ya kuanza kuhangaishana mahakamani ambapo mwisho wa siku lazima watuhumiwa wangeachiwa huru kwa kukosekana kwa ushahidi wa moja kwa moja...
“Nakubaliana na wewe kuwa Rais wetu James Kahungo (the JK) ni mpenda haki, lakini tatizo lipo kwa wasaidizi wake ambao kila mmoja anawaza kujinufaisha yeye, kama hiyo haitoshi wana tabia ya kulindana wanapoona mwenzao amefanya maasi…Watateteana na mwisho hakuna lolote litakaloendelea. Mwanao atakuwa ameshaharibiwa na mumeo ataendelea kuozea gerezani.”
Alichokizungumza daktari Zayumba kilikuwa ni kweli kwani nchi ya Blaziniar kwa sasa ilikuwa imetawaliwa na urasimu na hujuma karibu kila idara tofauti na zamani .Viongozi wa juu walikuwa wakifanya maasi na wakikaribia kubainika walikuwa wakiwatumia raia wa kawaida kama ngao kwao.Walikuwa wakipeana kazi wao kwa wao na kulipana mishahara minono huku mwananchi wa kawaida akizidi kuteseka.Kibaya zaidi walikuwa wakijihusisha na vitendo viovu kama ujambazi kwa kuunda makundi yao, huku wengine wakijihusisha na biashara haramu ya madawa ya kulevya. Zaidi ya yote, ufisadi na uhujumu uchumi ulikuwa ukizidi kupamba moto. Kwa kifupi serikali ya Blaziniar ilikuwa imepoteza kabisa mwelekeo.
“Sasa wewe unafikiri tutafanya nini? Kinachotakiwa hapa ni kuwafichua wote waliohusika na hatimaye ukweli halisi ufahamike na mume wangu aachiwe huru” Aliongea Bi Patricia kwa masikitiko huku akionekana kukata tamaa.
Kuna mbinu mbili ambazo naamini zitafaa sana… ya kwanza ni kumtafuta mwanasheria ambaye atatusaidia kuendesha kesi…lakini tutahitajika kuwa na pesa nyingi za kumlipa na kuendesha kesi na kuna uwezekano njia hii ikachukua muda mrefu sana mpaka hukumu ya mwisho itolewe.
Lakini hii njia ya pili nadhani ndio inafaa zaidi…Bi Patricia alitega masikio yote mawili kwa makini kutaka kuisikia njia hiyo ya pili ni ipi.
“Njia ya pili ni kutumia vyombo vya habari kama sauti yetu sisi wanyonge.Tutakachokifanya ni kuandaa taarifa zote muhimu kuhusu namna tukio lilivyotokea tukiambatanisha na taarifa ya ushahidi wa kidaktari na kuupeleka kwenye vyombo vya habari ili wananchi wote wa nchi hii wafahamu ukweli unaofichwa na serikali juu ya unyama waliomfanyia Geneviv.”
Njia hii ndio iliyoonekana inafaa zaidi na wote wakaiafiki. Wakaanza kutafakari ni chombo gani cha habari kinachoweza kuwa msaada kwao.
“ Mi nadhani twende pale kwenye ofisi za kampuni ya Planet Link Media, unajua wale wanachapisha magazeti yanayosomwa karibu nchi nzima, halafu Redio yao inasikika pande zote za nchi na kama hiyo haitoshi mmiliki wake ni mtu wa Mungu na anapenda siku zote kuona haki ikitendeka. Naamini atakuwa msaada mkubwa kwetu.”
Baada ya makubaliano hayo, walianza kujiandaa bila kupoteza muda. Geneviv akaandaliwa na kwa kutumia gari la Dokta Zayumba safari ya kuelekea Mwenge zilipo ofisi za Planet Link Media ikaanza. Walipofika waliomba kukutana na mkurugenzi, Bwana Samson Liganga ambapo walionyeshwa ofisi yake ilipo na katibu muhtasi (secretary wake). Baada ya salamu, walianza kueleza kilichowapeleka. Bwana Liganga aliwasikiliza kwa makini huku akinote’ mambo ya msingi kwenye kitabu chake cha kumbukumbu. Walieleza kila kitu kuanzia mwanzo mpaka mwisho, na Geneviv akahitimisha kwa ushahidi mzito ambao ulimuacha bwana Liganga ameduwaa. Alipokuwa akimtazama Geneviv, aligundua kuwa hakustahili kufanyiwa unyama kama ule kwani ukiachilia mbali urembo, bado alikuwa msichana mbichi kabisa.
“Oooh My Lord, pole malaika. Hukustahili kupatwa na yaliyokupata, ila kwa kuwa yameshatokea basi Mungu ndio anayejua.”
Aliongea bwana Liganga kwa masikitiko na baada ya hapo ukimya ukatawala ofisini. Kila mtu akawa amezama kwenye mawazo kivyake… zaidi bwana Liganga ambaye alionekana kuumizwa zaidi. Ilibidi awaombe wafumbe macho ili wasali kwa Mungu wao awaongoze katika vita ile kali iliyokuwa mbele yao. Baada ya sala iliyodumu kwa takribani dakika ishirini ikiongozwa na bwana Liganga mwenyewe, wote waliitikia Aaamen! Wakiwa na imani kubwa kuwa Mungu wao angewatangulia na kuwaonyesha njia ya kupita.

Baada ya hapo bwana Liganga aliitisha mkutano wa dharula na waandishi na watangazaji wa kampuni yake. Sekunde chache baadae wakawa wamekusanyika kumsikiliza bosi wao. Aliwaeleza kitu cha kufanya na muda mfupi baadae kazi ikaanza mara moja. Geneviv akachukuliwa na kuingizwa chumba cha habari ambapo alianza kuhojiwa mara moja huku akirekodiwa na mitambo ya kisasa iliyokuwa ndani ya chumba cha habari.
Masaa machache baadae taarifa ile ikaanza kurushwa hewani na kuwafanya raia wote waanze kuufahamu ukweli halisi wa tukio. Shughuli ilikuwa pevu kwani kila aliyeisikia habari ile alibaki mdomo wazi kwa namna ambavyo jeshi lilikuwa limefanya unyama na kisha kuwadanganya wananchi.
“Tumechoka na serikali ya kibabiloni, tuliwapigia kura ili watutetee, ona sasa na wao wanaungana na polisi kupindisha sheria, mimi nashauri wananchi wote tuandamane mpaka haki itakapochukua mkondo wake, tumechoka, tumechoka….”
Alisikika mwananchi mmoja akitoa maoni yake redioni baada ya kuusikiliza kwa makini mkasa ule. Watu walizidi kutoa maoni yao ambapo kila mmoja alisisitiza kuwa lazima wananchi wote waandamane kumtetea binti yule na baba yake na kuwashikisha adabu wote waliohusika.
Habari ile ilizigusa hisia za watu wengi mno kiasi cha kusababisha vuguvugu kali miongoni mwa raia wote wa Blaziniar.
****
Mambo yameanza kuchangamka, wananchi wamekuja juu mno baada ya kuubaini ukweli na sasa wanaishinikiza serikali…
“Huu ndio unaoitwa mchezo mchafu, iweje hawa polisi watuchezee akili kama watoto wadogo? Kumbe matangazo yale yote waliyokuwa wanadai kituo kimevamiwa na silaha zimeibwa ilikuwa ni uzushi mtupu wakijaribu kuficha uozo wao, haiwezekani…”
Hayo yalikuwa ni mazungumzo ya mmoja kati ya watu wengi waliokuwa wameanza kujikusanya makundi makundi karibu nchi nzima wakifuatilia kwa makini kilichokuwa kikitangazwa redioni kuhusu yaliyomsibu binti mdogo Geneviv.

“Enough is enough, inatosha sasa…tumechoka kuonewa! No more tears…”
Aliongea mzee maspedi kwa mbwembwe na kushangiliwa na wenzake waliokuwa wakimsiliza.
Vuguvugu lile liliendelea kushika kasi na kusambaa nchi nzima kama moto wa nyikani huku kila mmoja akilipokea kwa hisia tofauti. Wengi walionekana kuchoshwa na uonevu wa serikali yao kupitia vyombo vyake kama polisi, mahakama na bunge.
Ikawa “nkhondo igwa” nchi nzima. Watu wakaanza kujiandaa kufanya mgomo mkubwa nchi nzima kuishinikiza serikali iwachukulie hatua kali wote waliohusika na wafungwa wote wanaoshikiliwa kiuonevu wakiongozwa na mzee Rwakatare waachiwe huru.
Hakuna aliyeonekana kufanya mzaha tena, kila mtu alidhamiria kuukomesha uonevu wa serikali kwa wananchi wake. Wengi walianza kuamini ule msemo usemao wanaokwenda jela sio wote wana hatia…na sasa kila mmoja alianza kuona ukweli.
“Ndiyo mchezo wao hao, mbona wengine tulishashtuka siku nyingi kabla, tuungane tuukomeshe unyanyasaji kama huu, tatizo na sisi wananchi tumezidi woga, tunaona mambo ya ajabu yanafanyika nchini mwetu tunabaki kimya na kuwa watazamaji, sote tuamke....” Ilikuwa ni kelele mtindo mmoja huku watu wakishangilia kila hoja ilipokuwa inatolewa.
*****
Habari zilizidi kuenea kwa kasi ya ajabu mpaka zikamfikia Raisi ikulu. Ilibidi awaite wasaidizi wake mapema kabla mambo hayajaharibika zaidi kwani kulikuwa na ripoti kutoka sehemu mbalimbali za nchi kuhusu wananchi kutaka kuandamana nchi nzima.Kikao cha dharula kikaitishwa ndani ya Ikulu na maafisa wote wa polisi na usalama wakaitwa.
Raisi alionekana kuchanganywa na habari zilizokuwa zimetapakaa nchi nzima na sasa akawa anahangaika kutuliza mambo kwani alijua kuwa kama atazembea na kutanguliza kujuana na uswahiba angezidi kuwaudhi wapiga kura wake ambao nao walishapoteza imani naye na serikali yake. Ilibidi awe mkali sana ili kuhakikisha ukweli unapatikana haraka sana.Tofauti na maraisi waliokuwa wamemtangulia ambao walikuwa wakipenda kuunda tume kufuatilia mambo kama yale na kupoteza pesa nyingi za walipa kodi na muda, yeye aliamua kulivalia njuga swala lile mwenyewe na kuingia kazini.

Alianza na maafisa wa juu wa polisi ambapo aliwataka waeleze ukweli ni upi kati ya taarifa waliyokuwa wameitoa wao kwa vyombo vya habari na ile waliyoitoa waathirika wa unyanyasaji ule wa mtoto Geneviv na baba yake.
“Hii ni aibu kubwa sana kwangu na kwa serikali nzima. Wananchi wanatulaumu na sasa tumepoteza imani kabisa kutoka kwa wapiga kura wetu.Sijui tufanye nini ili warudishe imani yao kwetu… Mimi kama mkuu wa nchi siwezi kuvumilia kuona hadhi yangu na umaarufu mkubwa niliojijengea unachafuliwa kwa ujinga wa wachache kati yenu.
Lazima niufahamu ukweli mara moja… na ikigundulika kuna uzembe wa aina yoyote hapa, wote mliohusika mtawajibishwa vikali mara moja”
Alikuwa akifoka Raisi James kahungo wakati akiendelea na kikao chake cha dharula na maafisa wakuu wa jeshi la polisi. Baada ya kuongea kwa kifupi, raisi aliamua kuongozana na maafisa wa polisi mpaka kituo kikuu cha polisi ambako iliripotiwa kuwa ndio kile walichokitangaza polisi kama ujambazi ulitokea.
Msafara ule mrefu ulifika kituoni ukiongozwa na raisi mwenyewe na alipofika tu aliwataka Maafisa wa polisi na mkuu wa kituo waeleze na kuonyesha ushahidi wa namna ambavyo kituo hicho kilivamiwa, ghala ya silaha ikavunjwa na polisi kuuwawa kama walivyokuwa wametoa taarifa kwenye vyombo vya habari siku chache zilizopita.
Si mkuu wa kituo wala maafisa waliokuwa tayari kutoa maelezo yaliyonyooka mbele ya Raisi ambaye sasa alikuwa amefura kwa hasira. Wote wakawa wanajikanyaga huku wakitetemeka.
Ukweli ambao ulimshangaza hata Raisi mwenyewe ni kwamba hakukuwa na dalili yoyote ya kuvamiwa kwa kituo kile.
Ghala la silaha lililodaiwa kuvunjwa na majambazi halikuwa na alama yoyote ya kuthibitisha kama ni kweli lilivunjwa ingawa walipoingia ndani waligundua kuwa silaha nyingi hazikuwemo.
Hili nalo halikupata jibu la haraka na la kuridhisha na maafisa wale na mkuu wa polisi kila walipokuwa wakiulizwa hawakuwa na majibu zaidi ya kuanza kutetemeka kila mmoja kivyake.
“Nataka maelezo kuhusu hili, sio kuchekecheka hapa. Unamchekea nani wakati wananchi wangu wanalia…na nchi inaangamia?”
Raisi alikuwa akimfokea mkuu wa kituo ambaye alionekana kuleta mizaha kwenye maelezo yake. Hakuwa na majibu yenye kujitosheleza na badala yake akawa anatanguliza samahani nyingi kwa Raisi.
Baada ya kutoka kwenye Ghala la silaha, Raisi aliomba kupelekwa nyumbani kwa askari aliyedaiwa kuwa aliuawa na majambazi ambapo pia hakuna aliyeweza kuonyesha wala kuthibitisha kuwa ni kweli kuna askari aliuliwa.
Alipoona wote wanatupiana mpira akaomba kutajiwa jina lake, lakini pia hakupata jibu. Akagundua kitu ingawa hakupenda kuwa na maelezo mengi.
Alipoenda kukagua vyumba vya nje ambavyo mtoto Geneviv wakati akihojiwa redioni alieleza kuwa ndiko alikofanyiwa ukatili ule, aligundua kuwa ni kweli mlango ulikuwa umevunjwa na alipoingia ndani alishuhudia mwenyewe kwa macho yake, damu nyingi zikiwa zimeganda na kukauka juu ya kitanda kidogo kilichokuwa mle ndani na pale chini sakafuni.
Alipoomba ufafanuzi wa hilo, pia hakukuwa na majibu zaidi ya kila mmoja kuonekana akijikanyaga kwa hofu.
Raisi alipotoka aliingia mpaka ofisini kwa mkuu wa kituo ambako aliomba majina ya askari wote waliokuwa doria na wale waliokuwa zamu siku ya tukio.
Katika hali ya kushangaza mkuu wa kituo alianza kuwatetea kuwa wao walikuwa kazini na kama yalitokea makosa basi kwa niaba yao anaomba wasamehewe kwani wao ni binadamu na hukosea.
Kwa hali aliyokuwa nayo Raisi Kahungo, alishindwa kuzizuia hasira zake na akajikuta amerusha ngumi iliyompata sawia mkuu wa kituo na kumfanya apepesuke huku akitaka kuanguka kabla ya kudakwa na wenzake. Mara moja Raisi akatoa amri ya mkuu yule wa kituo kuwekwa chini ya ulinzi.
Wanajeshi wa jeshi la watu wa blaziniar (Blaziniar Force Unit) wakapewa jukumu hilo. Ndani ya muda mfupi mkuu wa kituo akawa ndani ya karandinga la jeshi chini ya ulinzi mkali.
Raisi aliwazuia wasimpeleke kwanza kwenye gereza la kijeshi mpaka atoe maelezo ya askari waliokuwa zamu siku ya tukio. Akawa anashindwa kueleza huku akilia kama mtoto. Alikuwa amezoea kunyanyasa sana Raia lakini leo ilikuwa zamu yake.
Rais kahungo hakuwa na masihara tena. Alikuwa amechukia na kuvimba mithili ya nyoka koboko mwenye sumu kali.
Akaitwa msaidizi wa mkuu wa kituo na kuamriwa kutoa majina ya watu waliokuwa zamu siku ya tukio. Baada ya kuona hali aliyokuwa nayo rais, alianza kutetemeka na kutafuta faili lililokuwa na kumbukumbu zote za wafanyakazi.
Akatoa karatasi lenye majina ya watu kumi, ambao wawili kati yao ndio waliokuwa pale kituoni usiku wa siku ya tukio na wengine nane walikuwa Doria.
Akaagiza wote kumi watiwe nguvuni na bila kupoteza muda jeshi likaanza kuwasaka na muda mfupi baadae wakapatikana. Baada ya kupatikana wote, mmoja alionekana kuwa na jeraha kubwa kichwani ambalo alilificha kwa kuvaa kofia kubwa.
Raisi akawa anapita mbele ya kila mmoja akiwakagua na kuwahoji maswali makali.
Alipofika kwa yule mwenye jeraha, alimvua kofia kwa nguvu na akaanza kukumbuka maelezo ya mtoto aliyefanyiwa ukatili wakati akihojiwa redioni.
Akagundua kuwa huyo ndio yule aliyekutwa na baba wa mtoto mzee Rwakatare kisha akapigwa kichwani na kitu kizito. Alipomhoji huku akimkazia macho kuwa lile jeraha kichwani lilisababishwa na nini, alishindwa kujibu na akajikuta akiachia haja ndogo.
Wote waliomshuhudia waliangua kicheko baada ya kumuona yule polisi akiwa hana ujanja mbele ya Raisi mpaka kushindwa kujizuia.
Pamoja na watu karibu wote kucheka, Rais alionekana kuvaa sura ya kazi akiwa hana hata chembe ya mzaha.
Aliendelea kukunja sura huku akizidi kumsogelea yule polisi. Katika hali nyingine, Rais alishindwa kuzuia hasira zake na akajikuta akirusha kibao kizito ambacho kilimpata na kumfanya aanguke mzimamzima kama mzigo mpaka chini.
Wenzake wakamuinua na akawa anaendelea kumhoji maswali magumu. Watu wote walipigwa na mshangao wakiwa hawaamini kama ni yule Raisi waliyemzoea ndio alikuwa mkali kiasi kile, wakajua kuwa kweli moto unawaka.Akatoa amri kuwa wale polisi wote kumi waliokuwa zamu siku ya tukio nao waunganishwe na mkuu wao wa kituo na wapelekwe gereza la kijeshi kwa ajili ya kushikishwa adabu.

Muda mfupi baadae karandinga la jeshi likiwa na watu kumi na moja likaanza safari ya kuwapeleka watuhumiwa kweye gereza kuu la kijeshi.Raisi na msafara wake wakaelekea hospitali alikolazwa mtoto Geneviv akiendelea kupata matibabu. Alitaka kwenda kumuona mwenyewe mtoto aliyefanyiwa ukatili ule wa kutisha.
Muda mfupi baadae msafara ulikuwa tayari pale Hospitali na Raisi akafikia ofisini kwa Daktari mkuu, Barikieli Zayumba ambaye alienda kumuonyesha wodi aliyolazwa Geneviv. Hakutaka mtu mwingine yeyote aingie nae wodini zaidi ya Daktari Zayumba.
Raisi akakutana ana kwa ana na Geneviv na mama yake Bi Patricia aliyekuwa aamejiinamia pembeni ya kitanda alicholala mwanae. Kwa ile hali ambayo Rais James kahungo aliishuhudia pale wodini, ilitosha kumdhihirishia namna ambavyo wananchi wake walikuwa wakiteseka.
“Pole binti kwa yote yaliyokukuta! Pole sana”
Rais alikuwa akimpa pole Geneviv huku akimsikitikia sana. Alisalimiana pia na Bi Patricia na akawahakikishia kuwa ameamua kulifuatilia swala lile yeye mwenyewe na haki lazima ingepatikana baada ya muda mfupi. Alikaa juu ya kitanda cha Geneviv na kumuomba amsimulie hali halisi jinsi ilivyokuwa.
Geneviv bila wasiwasi alimsimulia kila kitu kama alivyosimulia redioni.
Hakuacha kitu. Pamoja na ukakamavu aliokuwa nao Rais, alijikuta akishindwa kuyazuia machozi yasimtoke. Alimuonea huruma mno na hata yeye alikiri kwamba hakustahili kutendewa namna ile kutokana na jinsi alivyokuwa. Baada ya kumaliza kumsikiliza Geneviv, aliaga na akaahidi atarudi tena kumjulia hali binti Geneviv.
Alipotoka nje, wafuasi wake wote walikuwa wakimsubiri mlangoni na wote walishuhudia namna alivyobadilika usoni. Macho yalikuwa mekundu sana kuonyesha kuwa alikuwa akilia. Wakajua hukumu iliyokuwa mbele ya wahusika isingekuwa ya mchezo.
Wote walikuwa wakinong’onezana chini chini kwamba kama Rais angekuwa hivyo kufuatilia mambo yote, hakika nchi ingefika mbali sana kimaendeleo na kidemokrasia.

Baada ya kutoka hospitali msafara uliongoza mpaka gerezani alikokuwa amefungwa Mzee Rwakatare.
Mzee Rwakatare alikuwa amefungiwa ndani kabisa ya gereza kiasi cha kutotambua kilichokuwa kikiendelea katika ulimwengu wa kawaida. Aliamini huo ndio ulikuwa mwisho wake na akawa analia kwa kuiacha familia yake bila mwongozo.
Kule ndani alikofungiwa kulikuwa na giza muda wote kiasi cha kushindwa kutofautisha mchana na usiku. Alikuwa hajui chochote kinachoendelea Uraiani kwa kuwa alizuiwa kukutana na mtu yeyote kutoka nje hata mke wake.
Alijua kuwa kipindi chake cha maisha aliyobakiza hapa duniani kingeishia mle gerezani na akawa hana mategemeo kabisa ya kunusurika. Alichokuwa akikifanya muda wate ilikuwa ni kumlilia Mungu wake amsamehe dhambi zake zote na azidi kuilinda familia yake ambayo sasa ilibaki bila baba.
Baada ya kufika eneo lilipo Gereza kuu, Rais James Kahungo aliamuru mzee Rwakatare atolewe kwa ajili ya kufanya naye mahojiano maalum. Mzee Rwakatare alikuja kushtuka kutoka kwenye lindi zito la mawazo baada ya kusikia mlango mkubwa wa chuma wa kuingilia kule alikokuwa amefungwa ukifunguliwa. Akajua siku ya kwenda kupandishwa kizimbani na kusomewa mashtaka imefika.
Akabaki amekaa vilevile kama alivyokuwa, akimwangalia askari magereza aliyekuwa akihangaika kufungua mlango. Tofauti na alivyotarajia, yule askari magereza alimletea nguo zake alizovuliwa wakati akiingizwa mle gerezani na kwa upole akamwambia kuwa ajiandae haraka kwani kuna mtu muhimu sana amekuja kumtembelea.
Mzee Rwakatare akabaki akijiuliza maswali mengi bila majibu. Kwanza kitu cha kwanza alishangaa kwa jinsi yule askari magereza alivyokuwa mpole kwake tofauti kabisa na siku zote.Pili alishangaa ni nani aliyeruhusiwa kuja kumuona wakati mkuu wa gereza alishatoa amri kuwa asiruhusiwe mtu yeyote kuja kumtembelea. Alipomtazama yule askari usoni alisoma kitu, ikabidi aendelee kuvaa kama alivyoambiwa. Ieleweke kwamba gereza hili lilikuwa na utaratibu mgumu na wa ajabu kwani baada ya mtu kuingizwa ndani, huamriwa kuvua nguo zote na kisha kupewa kaptura chafu ya magereza yenye chawa wengi huku ukiachwa kifua wazi. Kwa muda mfupi tu aliokaa mle ndani, mzee Rwakatare alikuwa amedhoofika sana kiasi cha mbavu zake kuanza kuhesabika.

“Tafadhali fanya haraka mzee!”
Yule askari alizidi kumhimiza mzee Rwakatare kwa sauti ya upole.
Baada ya kuwa tayari, walitoka na kuanza kuelekea ofisini kwa mkuu wa gereza. Akiwa anazidi kwenda alishtushwa na umati mkubwa wa watu ambao aliwatambua kwa haraka kuwa ni viongozi wa juu wa serikalini, huku nje kukiwa na msururu mrefu wa magari. Alishindwa kuificha hofu yake na sasa akawa anatetemeka mwili mzima.
Baada ya kuingia ofisini huku akiwa bado anatetemeka, macho yake yalikutana ana kwa ana na Raisi James Kahungo. Akajua swala lake limekuwa kubwa sana, mpaka Rais amekuja gerezani. Aliona huo ndio muda muafaka wa kujitetea kwa kadri ya uwezo wake wote mbele ya mkuu wa nchi.
“Lakini mimi sio jambazi wala muuaji mheshimiwa Raisi, wamenisingizia tu…sio kweli”
Alianza kujitetea hata bila salamu wala kuruhusiwa kuongea. Mheshimiwa Raisi alisimama na kuamuru watu wote waliokuwa mle ofisini watoke nje na kumuacha na mzee Rwakatare. Baada ya sekunde kadhaa, wakabaki wawili tu.
“Pole sana kwa yaliyokukuta, nimeshaujua ukweli wote na hivi unionavyo nimetoka Hospitali alikolazwa mwanao. Amini nakuambia jogoo hatawika asubuhi ya kesho kabla hujaungana na familia yako.”
Mzee Rwakatare hakuamini alichokisikia kutoka kwa Raisi wake. Alikuta moyo ukimlipuka kwa furaha kiasi cha kuruka juu na kumkumbatia Rais james Kahungo kwa nguvu.
“Kwa kuwa umekisikia kilio changu na kuja kunifungua minyororo ya uonevu na kuniahidi uhuru, nami ntakupa siri nzito ambayo hakuna anayeweza kukwambia.”
Kwa Furaha aliyokuwa nayo, Mzee Rwakatare alijikuta akianza kuropoka na kutoa siri.
Rais alitega sikio na kuanza kumsikiliza kwa makini.Akaendelea…
“Natambua kwamba wewe ni mwanamapinduzi halisi na ndio maana leo uko hapa.
Nitakachokuambia kifanyie kazi na utaubaini ukweli. Kati ya watu zaidi ya mia tatu uliotusimamisha kazi serikalini kwa tuhuma za ufisadi na uhujumu uchumi nikiwepo na mimi,umetuonea kabisa. Ukweli ni kwamba sisi tumegeuzwa ngao ya wakubwa ambao bado wako madarakani na unashinda nao ikulu.
Mafisadi ni hawa ulioongozana nao na niko tayari kukusaidia kuufahamu ukweli wa namna wanavyokuzunguka na mwisho wa siku wanatubebesha sisi watu wa chini misalaba…amini nakwambia, una kazi ngumu sana ya kujisafisha kwani tayari wananchi wamepoteza imani. Nipe nafasi nikusaidie na hii itakuwa kama shukrani yangu kwako kwa kunitoa gerezani.”
Mzee Rwakatare alihitimisha maelezo yake na kumuacha rais akiwa ameduwaa. Mzee Rwakatare alionyesha kuwa na siri nzito sana…na hili lilidhihirishwa na lugha ya macho aliyokuwa akimuonyesha raisi.
“Ok nimekuelewa vizuri na baada ya kutoka humu jioni ya leo nitakuhitaji usiku uje ikulu ili unipe taarifa rasmi. Usimwambie mtu mwingine yeyote na uwe kimya mpaka nitakapotuma mtu kuja kukuchukua usiku wa leo.”
Rais aliinuka na kumuita mkuu wa gereza ambaye aliingia akiwa anakimbia.
Alimuachia maagizo kuwa Mzee Rwakatare aachiwe huru mara moja na ahakikishe anapewa ulinzi na kupelekwa mpaka nyumbani kwake.
Safari ya kurejea ikulu ikaanza huku Rais James Kahungo akiwa na mawazo tele kichwani. Alishindwa kuamini kama kweli watu wake aliowaamini kwa kiasi kikubwa wanaweza kumgeuka na kumsababishia ugumu wa kazi namna ile.Aliapa kuendeleza vita mpaka imani yake kwa wananchi irejee.
Wakati mzee Rwakatarea akimtonyaRaisi kuhusu siri nzito aliyokuwa nayo kuhusu uhujumu nchi na ufisadi, Baadhi ya mashushushu wa viongozi wakubwa waliokuwa nje, walikuwa wakisikiliza mazungumzo yaliyokuwa yakiendelea ndani kwa kutumia mitambo maalumu iliyokuwa imetegwa ndani ya chumba cha mkuu wa gereza.
Baada ya kufika ikulu na kumuacha Rais apumzike kwa kuwa alikuwa amechoka, taarifa za chinichini zikaenea miongoni mwa vigogo ambao waliitisha mkutano wa siri haraka sana.Ajenda kubwa ikawa ni kumuwahi mzee Rwakatare kabla hajatoa siri kubwa kwa Raisi.“Yule bwana tusipokuwa makini atatuharibia kila kitu kwa sababu anafahamu siri zetu nyingi na hasa wizara ya nishati na madini alikokuwa anafanyia kazi.Inabidi tumuwahi na kumpoteza kabla ya usiku hajakutana na Raisi.”
Alitoa hoja kigogo mmoja na kuungwa mkono na wenzake.

“Lakini lazima tuwe makini sana, kwa sababu Raisi akigundua mchezo huu tumekwisha… si mmemuona alivyokuwa leo? Halafu hata wananchi nao wameshaanza kushtuka, lazima tuwe makini”
Kigogo mwingine alitahadharisha hatari iliyokuwa mbele yao na kuwafanya wenzake wakune vichwa. Ilikuwa ni lazima mpango kabambe wa kumuua Mzee Rwakatare uandaliwe siku ileile kabla hajaenda kukutana na Raisi ili kuzidi kuuficha ukweli. Kikao cha siri kiliendelea kwa muda wa masaa matatu mfulilizo na hatimaye muafaka ukafikiwa…ikabakia utekelezaji.
Baada ya muda mfupi kupita tangu mkuu wa gereza aachiwe maagizo na ya kumuachia huru mzee Rwakatare, kweli alitekeleza alichoambiwa.Mzee Rwakatare aliachiwa huru na kupewa ulinzi wa kumrudisha mpaka nyumbani kwake salama.Alipofika nyumbani kwake alikuta nyumba ikiwa kimya kabisa, akajua bado mkewe na Geneviv wako Hospitali, bila kupoteza muda akaingia bafuni kutoa uchafu wote wa gerezani na baada ya hapo alizichoma moto nguo alizokuwa amezivaa na akawa anajiandaa kuelekea Hospitali.Alikuwa bado haamini kama ni kweli ameachiwa huru…alijihisi kama yuko ndotoni. Akiwa bado anajiandaa alisikia mlango ukigongwa. Akatoka kwenda kufungua.
“Ooooh my Lord, welcome back home! God is great…”
Walikuwa ni Bi Patricia na mwanae Geneviv baada ya kuruhusiwa kutoka Hospitali. Ilikuwa ni furaha isiyo kifani kukutana tena pamoja baada ya misukosuko mizito. Walikumbatiana pale pale mlangoni huku wakiwa wameshikana mikono. Wote walikuwa wakitokwa na machozi ya furaha wakiwa hawaamini kilichotokea. Waliendelea kukumbatiana kwa muda mrefu huku kila mmoja akiendelea kulia kwa furaha.
“Haya twendeni ndani, yote yametimia…Mungu akiwa nasi nani wa kutuzuia?”
“Hakunaa!” wote waliitikia na kuinuka kuelekea ndani. Walipofika sebuleni walianza upya kumshukuru Mungu wao kwa kuwakutanisha upya. Waliendelea kusali huku wakiwa wameshikana mikono. Walikaa kwa muda mrefu sana mpaka giza likaanza kuingia. Walisitisha maombi na wakaanza kusimuliana yote yaliyotokea kipindi ambacho walikuwa wametengana. Zilikuwa ni taarifa za kusisimua mno.

Baada ya kusimuliana sana, Mzee Rwakatare aliwapa taarifa juu ya mwaliko wa Rais wa kwenda ikulu jioni hiyo.
“Lakini kwani ni lazima uende leo, mi nafikiri usiku mzima wa leo tungeendelea kumuomba Mungu kwa miujiza aliyotufanyia, tutulie ndani mume wangu, huko utaenda hata siku nyingine..”
Bi Patricia alitoa hoja ya msingi sana, lakini mzee Rwakatare akawa mbishi na wakaanza kubishana kila mmoja akitetea wazo lake.
“Lakini lazima ujue kwamba mheshimiwa Rais ndiye aliyenisaidia mpaka muda huu tuko pamoja, lazima tumlipe fadhila.”
“Ni sawa mume wangu,lakini Mungu ndiye aliyewezesha yote haya. Tumlipe fadhila kwanza Mungu halafu siku nyingine ndio uende huko. Kwani cha msingi kinachokupeleka huko ni nini?”
“Naenda kuwafichua wote wanaoihujumu nchi yetu hasa kwenye ofisi niliyokuwa nafanya kazi, Nawafahamu wote na nazijua mbinu wanazozitumia, nimeshamwahidi Rais kuwa nitamsaidia…na amesema atamtuma mtu kuja kunichukua usiku huu” Alizidi kusisitiza mzee Rwakatare huku aking’ang’ania hoja yake.
“Mungu wangu, yaani hili halijaisha vizuri unataka kutuletea matatizo mengine, wewe hao mafisadi unafikiri watakuangalia vizuri unapoenda kuwachoma mbele ya Rais, tafadhali mume wangu…mambo ya siasa za nchi yetu achana nayo,bado tunakuhitaji…please don’t go!”
Wakiwa bado wanabishana, mara wakasikia muungurumo wa gari likija pale nyumbani kwao. Walipofunua pazia na kuchungulia nje,waliliona gari kutoka ikulu likipaki nje ya nyumba yao. Wakatazama…
“Niruhusu niende tu mke wangu, nilishamuahidi mkuu kuwa lazima niende na kama unavyoona ameshatuma mtu kuja kunichukua, haitakuwa busara kukaidi na ataona kama tumemdharau…please niruhusu!”
Mzee Rwakatare alikuwa akizidi kumshawishi mkewe amruhusu. Moyo wa Bi Patricia ulikuwa mgumu sana kumruhusu mumewe kuondoka. Yeye mwenyewe hakuelewa ni kwa nini hali ile ilimtokea, lakini ni kwamba moyo ulikuwa mgumu sana na akajikuta akiingiwa na hofu juu ya usalama wa mumewe. Geneviv alikuwa kimya akisikiliza mazungumzo ya wazazi wake. Hakuweza kuchangia chochote kwani alikuwa bado hajarudiwa na nguvu zake vizuri baada ya kutoka Hospitali.
Baada ya kuona mumewe akizidi kushikilia msimamo wake, ilibidi amruhusu kwa shingo upande.
“Daddy don’t delay…we will be missing you, and I got something special to let you know this night..” (Baba usichelewe kurudi, bado tunahitaji kukaa na wewe halafu kuna kitu maalum nataka nikuambie ukirudi)
Geneviv aliongea kwa sauti ya chini huku akimsindikiza baba yake kwa macho wakati akitoka kuelekea pale lililopaki gari kutoka ikulu. Alipofika nje aligeuka na kumwangalia mkewe aliyekuwa amejiinamia mlangoni, akampungia mkono na kuingia ndani ya gari. Safari ikaanza kuelekea ikulu.
Kichwani mwake alikuwa akishangilia ushindi kwa jinsi ambavyo angeenda kuwafichua wote wanaoihujumu nchi yao na kuwafanya kila siku wananchi wake wazidi kuwa maskini. Nitaeleza kila kitu… hata kama wakija kuniua bora kufa kishujaa kuliko kuishi kama ng’ombe. Bora kujitoa sadaka kwa ajili ya nchi yangu. Nitasema kila kitu bila kujali litakalonikuta. Mimi ni mwanaume kamili na lazima niutetee uanaume wangu kwa kuushinda woga na kuufichua uozo wa viongozi wetu…Do it or die”
Mzee Rwakatare alikuwa akijisemea moyoni peke yake. Kweli alidhamiria kutoka ndani ya moyo wake kuwa chachu ya mabadiliko nchini mwake. Safari iliendelea na sasa wakawa wameingia barabara kuu ya kuelekea ikulu.
“Dereva tafadhali punguza mwendo, unakimbilia wapi saa hizi? Twende taratibu na tut…
Kabla hata hajamalizia kusema sentensi yake, mzee Rwakatare kwa macho yake aliona roli kubwa lililobeba mawe likiingia barabarani mita chache mbele yao na kuzuia njia. Kufumba na kufumbua walishuhudia gari lingine kama lilelile likija kwa kasi ya ajabu likitokea nyuma yao, wakawa katikati… kufumba na kufumbua kikasikika kishindo kikubwa kama bomu na gari walilopanda mzee Rwakatare na dereva kutoka ikulu likawa kama chapati. Lilikuwa limegongwa vibaya na kukandamizwa katikati ya maroli mawili yote yakiwa yamejaza vifusi vya mawe ya kujengea. Hakukuwa na uwezekano wa mtu kutoka salama.

*****
“Bosi kazi yenu tayari imekamilika tunachokitaka ni mzigo wetu”
Kiongozi wa kundi hatari la majambazi ya “Bandidu killers” alikuwa akiongea kwa simu na mmoja wa vigogo waliokuwa wamekaa nao kikao cha siri cha kumpoteza mzee Rwakatare. Waliahidiwa mamilioni ya dola za kimarekani kama wangemuwahi kabla hajafika ikulu.
“mnasema kweli? Kwa hiyo safari ya ikulu imeshakuwa ya kuzimu? Kazi nzuri sana vijana, tunakuja sasa hivi palepale tulipokutana mchana. Mzigo wenu uko tayari na bila shaka mtafurahi wenyewe.” Ulisikika upande wa pili ukijibu kwa furaha na bila kupoteza muda wakaendaa kukutana pale walipokuwa wamekaa kikao cha siri mchana.
“Kwa hiyo mna uhakika hakuna hata mmoja kati yetu atakayehusishwa na kifo chake” Alihoji mmoja wa vigogo wakati akiwakabidhi Bandidu killers mfuko uliojaa dola za kimarekani.
“Ile ni ajali na tumefanya kama mlivyotuagiza. Hakuna hata mmoja kati yenu atakayehusishwa kwa sababu ajali ni ajali na inaweza kumkumba yeyote muda wowote”
Alijibu kwa sauti nzito kiongozi wao na baada ya makabidhiano kila mmoja akatawanyika wakila kiapo cha kila mmoja kutunza siri ile.
Raisi James kahungo alikuwa tayari ameshaingia kwenye ofisi yake ndogo akimsubiri dereva wake amlete mzee Rwakatare ili ampasulie siri nzito. Alikuwa na hamu kubwa ya kutaka kuwajua hao wanaomzunguka na alijiapiza kuwashikisha adabu bila kujali vitambi vyao.
Akawa anaendelea kungoja. Muda nao ukawa unazidi kuyoyoma huku kukiwa hakuna dalili ya mtu yeyote kuingia ndani. Akaanza kupatwa na wasiwasi. Akainua simu ya mezani iliyokuwa pale mezani kwake na kujaribu kumpigia dereva wake, lakini hakupatikana.
“Whats wrong with them?” Utulivu ulimuisha na akawa anazunguka huku na huko mle ofisini kama anayetafuta kitu. Aliirudia tena ile namba ya dereva wake lakini bado ikawa haipatikani. Ikabidi amtafute mmoja kati ya vijana wake aliokuwa anawaamini kutoka kitengo cha usalama wa taifa. Akampa jukumu la kufuatilia kujua ni nini kilichotokea mpaka muda ule dereva aliyetumwa kumchukua mzee Rwakatare hajarudi na simu yake haipatikani. Hakujua kinachoendelea. Muda huo tayari ilishafika saa tano za usiku.
Wakati akiendelea kumsubiri yule kijana aliyemtuma arudishe majibu, alisikia taarifa ya dharula” Breaking news” ikisomwa kutoka kituo cha redio cha Planet Link fm, ikiripoti kuwa magari matatu likiwemo gari la ikulu yalikuwa yamepata ajali mbaya ya sana ya kugongana na kwamba polisi walikuwa wakiendelea kuhangaika kuwaokoa watu waliokuwa ndani ya magari yale ingawa taarifa iliendelea kueleza kuwa shughuli ya uokoaji imekuwa ngumu kutokana na mawe yaliyokuwa kwenye malori mawili kulifunika gari la ikulu na kulifanya liwe “nyang’anyang’a”.
“Mungu wangu! Whats the hell is this, ntawaambia nini wananchi kama mzee Rwakatare amekufa kwenye ajali? Bila shaka wataamini mimi ndie niliyemuua…”
Rais James Kahungo alipata mshtuko mkubwa sana baada ya kusikia taarifa ile, na akajikuta mwili ukimuisha nguvu na akili ikiacha kufanya kazi. Akadondoka chini na kupoteza fahamu.
Taarifa ile pia ilisikiwa na Bi Patricia ambaye baada ya kusikia tu, alitoa kauli moja tu…
“Nilijua lazima kuna njama za kumuua mume wangu,ona sasa…”
Naye akajikuta mapigo ya moyo yakimwenda mbio na mwili ukikosa nguvu, vikifuatiwa na kizunguzungu kikali kilichomfanya apoteze fahamu.
*****
Usiku ule ule habari zilienea kwa kasi huku kila aliyesikia akihisi kuna njama kali ambazo zilikuwa zimepangwa za kumuangamiza, kila mtu alikuwa haamini masikio yake. Vuguvugu ambalo lilikuwa limeanza kutulia likaanza kulipuka upya.
Shughuli za uokoaji ziliendelea mahali ilipotokea ajali mbaya baada ya magari matatu kugongana, likiwemo gari la ikulu ambalo ndani yake kulikuwa na watu wawili, dereva kutoka ikulu na mzee Rwakatare.
Taarifa za awali zilionyesha kuwa hakuna uwezekano wa mtu yeyote kutoka akiwa hai kwenye ajali ile kwa jinsi ambavyo gari la ikulu lilikuwa limebondeka baada ya kubanwa katikati ya maroli mawili yaliyokuwa yamejaza mawe makubwa. Ajali ilitisha na ikageuka kuwa gumzo la nchi nzima. Hiyo ilimaanisha kuwa huo ndio mwisho wa mzee Rwakatare na safari yake ya kuelekea ikulu ikawa imegeuka na kuwa ya kuzimu.

Ilikuwa ni kama simulizi isiyokwisha. Wananchi walikuja juu hasa baada ya ajali yenyewe kuonekana dhahiri ilikuwa imepangwa na wakawa wanamshinikiza Raisi ajiuzulu huku wengine wakimtaka avunje baraza lake lote. Hata baada ya uokoaji kukamilika, miili iliyopatikana ilikuwa haitamaniki kutokana na jinsi ajali ilivyokuwa mbaya na huo ndio ukawa mwisho wa kusikitisha wa mzee Manuel Rwakatare.
Bi Patricia alikuwa hajitambui na kila fahamu zilipomrudia, alikuwa akizimia tena, akiwa haamini kama ni kweli mumewe ndio ametangulia mbele za haki kwa namna ile. Maelfu ya watu walikusanyika nyumbani kwa mzee Rwakatare na mipango ya mazishi ikaanza kuandaliwa. Kila mtu alizungumza lake lakini ukweli ukabaki kuwa palepale. Mzee Rwakatare alikuwa ameshatangulia mbele za haki.
“Rest in peace daddy! May God grant you eternal light… R.I.P”
Pumzika kwa amani baba, Mungu akujaalie mwanga wa milele, pumzika kwa amani”
Alikuwa aliongea Geneviv na kuwafanya waombolezaji waliokuwa wamejaa pale nyumbani kwao kuzidi kulia kwa simanzi kubwa.
Kwa Geneviv hali ilikuwa mbaya zaidi kwani sasa matukio ya ajabu na mikosi yalikuwa yamekolea. Pengo la kuondokewa na baba yake likawa ni pigo jingine lililozidi kumfanya atoe machozi…Soo many tears(Machozi mengi sana).
Mambo yalikuwa mabaya zaidi kwa Rais ambaye mshtuko mkubwa alioupata baada ya kusikia habari ile ulimfanya apoteze fahamu kwa muda mrefu hali iliyosababisha akimbizwe hospitali usiku uleule kuokoa maisha yake. Hata baada ya kuzinduka siku iliyofuatia, shinikizo la juu la damu lilikuwa limemuelemea kiasi cha kumfanya awe taabani. Aliamini kila mtu angehisi kuwa yeye ndiye mhusika wa kifo cha Manuel Rwakatare kutokana na mazingira ya kutatanisha ya namna ambavyo kifo kile kilitokea.
Taratibu za mazishi zilipokamilika mwili wa marehemu ulipelekwa makaburini tayari kuuhifadhi kwenye nyumba ya haki mpaka siku ya hukumu. Si Geneviv wala Bi Patricia ambaye aliamini kama kweli huo ndio ulikuwa mwisho wa baba yao. Walitia huruma sana kwa jinsi walivyokuwa wakiomboleza kwa huzuni. Wanawake kadhaa walipewa jukumu la kuwasimamia na kuwafariji kwa karibu, lakini bado hakuna aliyeweza kuwatuliza. Bi Patricia alikuwa amemkumbatia mwanae Geneviv huku wakilia kwa pamoja… walihuzunisha sana.

“Jikaze mpendwa, Mungu ana makusudi yake kwetu, tujifunze kumshukuru kwa kila jambo hata liwe la kuumiza sana kama hili…tumwachie yeye kila kitu kwani yeye anafahamu atakavyotufariji na kutulinda katika kipindi kigumu kama hiki.” Yalikuwa ni maneno ya faraja kutoka kwa mmoja wa marafiki wa karibu wa Bi Patricia.
Ilibidi jitihada za ziada zitumike kuwatuliza katika kipindi kile, ambacho kwao kilionekana kuwa kigumu zaidi ya vyote. Baada ya mazishi, maelfu ya waombolezaji walirudi nyumbani kwa mzee Rwakatare ambako msiba uliendelea.
Wakati haya yote yanatokea, Geneviv alikuwa yuko jirani kabisa kufanya mtihani wake wa mwisho wa kumalizia elimu ya msingi na huo ndio ulikuwa mwezi wa mwisho wa kujiandaa. Kutokana na matatizo yaliyokuwa yamemwandama mfululizo, alishindwa kuhudhuria shule kwa siku nyingi na kumfanya ashindwe kujiandaa vizuri. Hata baada ya msiba wa baba yake kuisha, bado hakuweza kwenda kuendelea na shule kutokana na muda mwingi kuwa na majonzi, wakishinda kulia na mama yake. Hakuna aliyeweza kumfariji mwenzake, ikawa ni machozi na maombolezo yasiyoisha. Kila kitu kilipoteza maana na akawa anajiona kama mtu aliyeandikwa matatizo tu chini ya jua. Machozi yalikuwa hayamuishi...Soo many tears.
Wiki tatu tangu Mzee Rwakatare azikwe, Bi Patricia alianza kusumbuliwa na shinikizo la chini la damu, ambapo moyo wake ulikuwa ukifanya kazi chini ya kiwango na kusababisha shinikizo la damu kushuka chini ya kiwango cha kawaida. Wataalamu waliielezea hali hii kuwa inasababishwa na mtu kuelemewa na msongo ambao huzaa huzuni kali, na kama mgonjwa asipopata matibabu ya haraka nay a uhakika athari zake zilikuwa mbaya sana. Tatizo hili lilimfanya Bi Patricia ashindwe kurejea tena kazini hata baada ya likizo ya kufiwa aliyopewa kuisha. Akawa muda mwingi akishinda amelala na mwanae Geneviv wakiwa hawaelewi nini hatma yao baada ya kuondokewa na nguzo yao, mzee Rwakatare.
Pamoja na kuendelea kutibiwa palepale nyumbani kwa msaada mkubwa wa daktari Zayumba, bado hali ya Bi patricia ilikuwa ikizidi kuwa mbaya, huku shinikizo la damu likizidi kushuka siku baada ya siku. Maisha yakaanza kuwa na sura tofauti kabisa na waliyoizoea.
****
Baada ya Rais Kahungo kurejea kwenye hali yake ya kawaida, alijikuta akishindwa kuendelea kuiongoza nchi baada ya wananchi kuendelea kulalamika sana juu ya yaliyotokea huku wakimtupia lawama zote yeye kwa kushindwa kuiongoza nchi kiasi cha kuwapa nguvu wahujumu na mafisadi kuipeleka nchi shimoni.
“I think I have to resign for the benefit of my people and my countrty” (Nafikiri natakiwa kujiuzulu kwa manufaa ya watu wangu na nchi yangu)
Rais Kahungo aliamua kuweka wazi msimamo wake mbele ya mwanasheria mkuu, mkuu wa majeshi na spika wa bunge la watu wa Blaziniar.
“Lakini mheshimiwa kwa nini usiendelee kuwa Rais mpaka kipindi hiki cha kwanza kiishe ndio uchukue uamuzi mwingine? Bado watu wanakuhitaji uendelee kuwaongoza”
Alitoa ushauri mwanasheria mkuu akiungwa mkono na spika wa bunge. Msimamo wa wa James Kahungo ukawa palepale.
“Nijuavyo mimi uongozi wowote ule ni imani ya wale unaowaongoza kwako, kama ikitokea imani hiyo imepungua au imeisha kabisa, huwi tena kiongozi bora ila unabaki kuwa bora kiongozi. Kwa hili sina la kufanya zaidi ya kuwapisha wengine nao wajaribu.” Aliendelea kusisitiza Rais james Kahungo na baada ya majadiliano mazito, walimkubalia alichokitaka kwa maslahi ya taifa na wananchi wake.
Siku iliyofuatia Raisi james Kahungo akatangaza rasmi kujiuzulu wadhifa wake kama Rais baada ya wananchi wake kukosa imani naye na kwa serikali yake. Alivunja baraza lote la mawaziri aliowateua na kumkabidhi Madaraka yote mwanasheria mkuu, bwana Sebastian Manyika. Kwa mujibu wa sheria za nchi ya Blaziniar, baada ya Rais kutangaza kujiuzulu, nchi huongozwa na mwana sheria mkuu akisaidiwa na mkuu wa majeshi mpaka uchaguzi mpya utakapofanyika.
Wengi waliipokea taarifa ya kuvunjwa kwa baraza la mawaziri kwa shangwe kubwa na wakazidi kumpongeza Raisi kwa uamuzi wa kishujaa wa kulinda hadhi yake aliouchukua na zaidi kwa kuiokoa nchi yake. Baada ya kuachia Madaraka, raisi na familia yake walirudi kijijini kwao Mtae iliko asili yao ambako walianzisha mashamba na kuendelea na shughuli za kilimo cha kisasa na ufugaji. Nchi ikawa inaongozwa na mwanasheria mkuu akisaidiana kwa karibu na mkuu wa majeshi ya ulinzi na usalama.
******
Hali ya Bi Patricia ilizidi kuwa mbaya siku baada ya siku, huku shinikizo la damu likizidi kushuka chini. Ilibidi apelekwe hospitali ambako angepatiwa huduma kwa ukaribu zaidi. Daktari Zayumba alijitolea kumsaidia mpaka ahakikishe anapona. Geneviv akajikuta ameanza upya shughuli ya kumuuguza mama yake mpendwa. Alishindwa kuelewa kwa nini yeye tu ndio anaandamwa na mikosi mikubwa namna ile. Alikuwa akilia sana akikumbuka yote yaliyompata ndani ya muda mfupi tu.
Akawa anamuomba Mungu usiku na mchana amsaidie mama yake kupona kwani yeye ndio alikuwa msaada pekee uliosalia maishani mwake . Hakutaka kuamini kabisa kuwa maisha yake ndio yalikuwa yakianza kupoteza mwelekeo kwa kasi namna ile. Ni ndani ya miezi michache sana, mambo yote yalikuwa yamebadilika kwa kiasi ambacho kingemshangaza kila mtu. Kutoka kuwa mtoto wa afisa wa juu wa serikali mpaka kuwa yatima asiye na baba akishinda hospitali kutwa nzima kumhudumia mama yake.
Hakufahamu ataishi vipi ndani ya ulimwengu uliojaa kila aina ya mabaya, tena akiwa bado binti mdogo kabisa. Alikuwa akitokwa na machozi kila alipomtazama mama yake ambaye hali yake ilikuwa ikizidi kuwa mbaya licha ya madaktari kuendelea kumhangaikia. “Kwani tatizo la my mum ni hilo tu la shinikizo la chini la damu au kuna jingine?, mbona mnampa dawa kila siku lakini haponi au kuna kingine, niambieni nijue please…”
Alikuwa akilalama Geneviv akionyesha kupoteza matumaini ya mama yake kupona.
“usiwe na wasiwasi Geneviv, Mungu atamsaidia mama na bila shaka atapona. Endelea kumuomba mungu usiku na mchana… Atapona tu umesikia eeeh!” alikuwa akiongea Daktari Zayumba akimtia moyo Geneviv. Alijitahidi kumpa msaada mkubwa wa kisaikolojia kwani ilionyesha dhahiri akili yake imeshindwa kuhimili matatizo makubwa yaliyokuwa yakimuandama akiwa bado na umri mdogo sana. Alijikuta akimuonea huruma sana.
“Nini hatma ya mama yangu? Mbona amepewa dawa nyingi sana lakini bado haamki?”
Aliuliza Geneviv akionyesha kuanza kukata tamaa ya mama yake kupona. Daktari Zayumba akawa anazidi kumpa moyo kuwa mama yake atapona tu, hata kama atachelewa. Pamoja na kuendelea kupewa kila msaada, Bi Patricia alishindwa kuzinduka na akawa ni mtu wa kulala masaa ishirini na nne. Hata kujigeuza pale kitandani alikuwa hawezi, Geneviv akabaki kuwa msaada wake wa mwisho.

Baada ya kuona hakuna nafuu inayopatikana, madaktari walishauri kuwa bora arudishwe nyumbani ili kupunguza gharama za kulala hospitali ambazo sasa zilikuwa kubwa. Geneviv hakuwa na la kufanya zaidi ya kuukubali ushauri ule. Daktari Zayumba akawasaidia usafiri wa kuwarudisha nyumbani na akaahidi kuzidi kutoa misaada kila mara.

Geneviv akawa amerudi na mama yake nyumbani, akitakiwa kufanya kila kitu ili mama yake aendelee kuishi. Ni yeye ndiye aliyetakiwa kuhakikisha mama yake anakula, anabadilishwa nguo na kufanyiwa usafi kila siku. Hakukuwa na mtu mwingine aliyeendelea kuwasaidia zaidi ya daktari Zayumba. Hata wale ndugu ambao kipindi maisha yao yakiwa mazuri walikuwa wakija kuwasalimu mara kwa mara na kujazana pale kwao, hawakuonekana tena. Ikawa ni Geneviv na mama yake, peke yao.

“Me and my mum…”
Alikuwa akiongea Geneviv kwa sauti ya kunong’ona akiwa amekaa pembeni ya kitanda cha mama yake akimtazama kwa huruma. Alionekana kupoteza kabisa matumaini ya mama yake kupona… akawa anangoja chochote kitakachotokea. Bi Patricia alikuwa amelala kimya akiwa hajui chochote kinachoendelea. Alikuwa amefumba macho na kupoteza nuru ya maisha. Kifo cha mumewe kilikuwa kimemmaliza kabisa, akawa ni kama anayengojea siku yake ifike akaungane na mumewe. Hali hii ilikuwa ikimfanya Geneviv alie usiku kucha. Hakuelewa nini hatma ya maisha yake baada ya nguzo zake zote kupotea, tena akiwa bado na umri mdogo kabisa. Alitia huruma.

Kadri siku zilivyokuwa zinasonga, ukali wa maisha ukaanza kujionesha dhahiri. Pesa ya akiba iliyokuwepo pale ndani iliisha na kusababisha aanze kushindwa kumpatia mahitaji muhimu mama yake. Mwisho chakula nacho kikaisha na kumfanya Geneviv aanze kuhaha huku na kule kuomba misaada. Hakutaka kuona mama yake anakosa mahitaji muhimu kama chakula, akawa anasumbuliwa na mawazo ya nini cha kufanya kuhakikisha mama yake anaendelea kupata huduma.

Akawa anaamka asubuhi na kuanza kuzunguka mitaani kwa kwa ndugu na majirani kuhakikisha wanapata japo chakula cha yeye na mama yake. Wote waliokuwa wakimfahamu walikuwa wakimuonea huruma sana. Siku za mwanzo wakawa wanamsaidia mahitaji madogomadogo lakini kadri siku zilivyokuwa zinasonga, misaada nayo ikapungua na maisha kuzidi kuwa makali. Ilifika mahali akawa anashindia uji siku nzima.

Alipoona mambo yanazidi kuwa magumu, ilibidi aende kwa rafiki yake wa siku nyingi waliyekuwa wakicheza pamoja siku za nyuma, Alice. Tofauti na yeye, mwenzake Alice hakusoma hata darasa la kwanza kutokana na wazazi wake kukosa kabisa uwezo wa kumsomesha. Lakini japokuwa hakusoma, Alice alikuwa akiishi maisha ya kujitegemea na alikuwa amepanga chumba ambacho alikuwa akikilipia kodi yeye mwenyewe. Alionekana kuyamudu maisha yake licha ya umri wake kuwa mdogo na haikufahamika mara moja alikuwa akifanya kazi gani.

“Nimekuja shosti, mwenzio maisha yamenishinda. Tangu baba afariki, mama anaumwa na wala haponi. Tumetumia hela zote za akiba kumtibia lakini bado hapati nafuu na saizi hata chakula tunakosa. Naomba unisaidie mawazo ya kazi ya kufanya ili niendelee kumtunza mama, mwenzio roho inaumaa…”
Aliongea Geneviv huku machozi yakimtoka. Alice alikuwa akimsikiliza kwa makini, na akajikuta akimuonea huruma. Alijua fika jinsi ugumu wa maisha unavyoumiza kwani na yeye alipitia maisha magumu sana.

“Jamani pole shosti, lakini nasikitika sana kukuambia siwezi kukusaidia kwani kazi ninayoifanya na inayoniwezesha mimi kuishi maisha mazuri kama haya wewe huiwezi. Ni kazi ya hatari sana. Hutaiweza Geneviv…” Aliongea Alice huku akimkumbatia Geneviv ambaye urafiki wao ulianza tangu wakiwa wadogo kabisa.

Geneviv alishangaa kwa nini Alice anasema vile, na akawa hajaelewa anamaanisha nini. Akaendelea kusisitiza kuwa ataweza tu kwa kuwa anashida.
“Kwani wewe umewezaje mpaka uniambie mimi siwezi? Na mimi nimekuwa mkubwa, nitaweza tu. Niambie tafadhali, nitajitahidi na nitaweza tu. Na mimi nataka niishi vizuri kama wewe. Nataka kumtunza mama yangu kwa uwezo wangu wote.”
Baada ya Geneviv kumbembeleza sana, ilibidi amwambie ukweli ila akamsihi asimwambie mtu yeyote.

Ukweli ni kwamba Alice alikuwa akifanya biashara ya kujiuza na hiyo ndiyo iliyomuwezesha kuishi maisha mazuri kama yale. Aliweza kulipa kodi, kununua vitu vya thamani kama makochi, redio kubwa, Tv na vingine vingi ambavyo vilikifanya chumba chake kionekane kama anaishi mtu mwenye uwezo mkubwa sana. Ni biashara hiyohiyo ya kujiuza ndiyo iliyomfanya amudu kufanya yote hayo.
“ Whaaat! Alice unajiuza? Siwezi…siwezi mimi bora nife maskini” Geneviv aliongea kwa sauti akiwa ameshtushwa mno kusikia rafiki yake akifanya biashara ya hatari kama ile. Kwa haraka aliinuka na kukimbia kutoka nje…huku nyuma akamuacha Alice akimkejeli

“Lakini nilikwambia hutaweza ukang’ang’ania, sasa unashangaa nini? Kama huwezi basi kaendelee kushinda na njaa na mama’ako. Utakufa maskini na uchumi umeukalia… utashaa…”
Baada ya kutoka kwa rafiki yake, Geneviv alikimbia mpaka chumbani alikolala mama yake. Akakaa pembeni ya kitanda na kuanza kumwaga machozi. Alikuwa katika wakati mgumu sana wa kuamua nini cha kufanya. Hakuna kitu alichokilaani maishani mwake kama uchangudoa. Lakini alipomtazama mama yake akiwa hoi pale kitandani, alijikuta akizidi kuchanganyikiwa zaidi. Alihitaji kupata pesa ili amsaidie mama yake, lakini hakuwa na namna ya kuzipata pesa hizo. Akawa anajiuliza mara mbilimbili juu ya alichoambiwa na rafiki yake Alice.

“Yaani mimi nikajiuze? No, No! haiwezekani. I wont dare it!” Aliongea kwa sauti na akaanza kulia tena. Hakuna aliyekisikia kilio chake… hakuna aliyeweza kumfariji. Akamuinamia mama yake pale kitandani huku akizidi kumwaga machozi. Bi Patricia alikuwa amefumba macho akiwa hajui chochote kinachoendelea. Aliendelea kulia kwa muda mrefu huku akizidi kutafakari alichoambiwa na rafiki yake Alice. Mpaka muda wa kulala unafika, alikuwa bado hajapata jibu. Mawazo yalikuwa yakishindana akilini mwake kiasi cha kumfanya aanze kuhisi kichwa kimekuwa kizito.

Akiwa amelala usiku, wazo jingine likamjia. Alifikiria sana jinsi ambavyo thamani yake ilitolewa kikatili baada ya kubakwa. Alijiuliza tena kama aliweza kubakwa na watu wengi kwa wakati mmoja, tena bila kupewa kitu, kwa nini asihalalishe kile alichoanza kufanyiwa ili amnusuru mama yake? Mawazo yalikuwa yakishindana kichwani na mwisho akafikia uamuzi wa mwisho. Aliamua kuuweka utu wake pembeni ili amnusuru mama yake. Akapania kuwa asubuhi na mapema atawahi kwa rafiki yake Alice kumwambia kuwa yuko tayari.


Asubuhi na mapema, Geneviv aliamka na kumtayarishia mama yake uji. Baada ya kumnywesha, alitoka na kueleka kwa rafiki yake Alice. Alipofika, Alice alikuwa bado amelala kutokana na kurudi usiku sana, ikabidi amuamshe na kumueleza kuwa amejifikiria usiku kucha kuhusu walichoongea jana yake, na ameamua kukubaliana naye.

“Kwa hiyo tutakuwa pamoja etii! Shaka ondoa, nitakufundisha kila kitu usijali. Cha msingi ondoa woga na utazoea sasa hivi.”
Alice alimpokea kwa furaha na kumuahidi kumfundisha kila kitu kuhusu kazi yake. Wakaandaa kifungua kinywa kwa pamoja na kuanza kula huku wakipiga stori zao za kawaida.

“Yaani Geneviv ulivyo mzuri mpaka nakuonea wivu. Usiku tukienda kazini utaona watakavyokugombania. Yani utapata hela nyingi sana mpaka mwenyewe utashangaa.”

Aliongea Alice na kumfanya Geneviv atabasamu. Hakufurahishwa na sifa zile, akilini mwake alikuwa akiwaza namna atakavyoianza kazi ya hatari usiku. Baada ya kunywa chai nzito kwa Alice, walitoka na kwenda kumuangalia mama yake Geneviv. Waliendelea kukaa pale nyumbani mpaka jioni ambapo Alice alimuelekeza Geneviv kuwa amuandalie kila kitu mgonjwa kabla hawajaondoka.
“Sasa mama atabaki na nani? Hatutachelewa kweli kurudi?” Geneviv alikuwa bado anasitasita, Alice akawa anamtoa hofu kuwa hawatachelewa.

Baada ya kuweka kila kitu sawa, Geneviv alifunga milango na madirisha akimuacha mama yake akiwa amelala na kuondoka kuelekea kwa Alice. Walipofika bila kupoteza muda walianza kujiandaa kuelekea kazini, kujiuza. Alice alikuwa mzoefu sana na kazi ya uchangudoa kwani aliianza tangu akiwa mdogo. Alikuwa akimuelekeza Geneviv kila kitu, kuanzia namna ya kujipodoa usoni, kichwani na mwilini na pia namna ya kuvaa nusu uchi. Geneviv alikuwa mgeni wa kila kitu. Alikuwa akishangaa kila kitu hali iliyomfanya Alice awe anamtania mara kwa mara kumcheka.

Ilipotimia saa tatu za usiku, walikuwa tayari wameshajiandaa kila kitu na wakawa wanatoka. Geneviv alikuwa akijishangaa kwenye kioo kilichokuwa mle ndani kwa jinsi alivyobadilika. Alikuwa akionekana mrembo kupita kawaida. Nguo alizoazimwa na Alice zilimfanya aonekane tofauti kabisa, zikimuacha sehemu kubwa ya mwili ikiwa wazi. Walipofika barabarani Alice aliita taksi na kumpa maelekezo dereva.

Tupeleke Valentino cassino tafadhali… Aliongea kwa manjonjo Alice na akafungua mlango akimuonyeshea Geneviv kwa ishara kuwa waingie ndani.
Safari ikaanza kuelekea Valentino Cassino, kilipokuwa kituo kikuu cha makahaba na machangudoa.

Ndani ya Valentino Cassino, kulikuwa kukifurika wasichana na wanawake wanaojiuza, wakubwa kwa wadogo, wamama kwa vibinti vidogo wote wakiwa wamevalia mavazi ya ajabuajabu ili kutangaza biashara.
“Full time mpaka asubuhi elfu thelethini, short time tunaelewana, hata ukiwa na buku tano poa tu!”

Dada mmoja wa makamo alikuwa akiongea biashara na kijana mmoja wakiwa wamesimama kwa upande wa nje. Geneviv aliyasikia mazungumzo yale na akabaki ameduwaa. Hakuwahi kufikiri kuwa uzinifu unaweza kuzungumziwa kibiashara namna ile, huku watu wakiwa hawana hofu kabisa. Wateja wa biashara ile walikuwa ni wanaume, vijana, wazee, wanafunzi na wahuni wa mitaani, lakini wengi wakiwa ni wale ambao tayari wana familia zao, na walikuwa wakiwafuata palepale na kuchagua mizigo kisha kuondoka na wanaempenda. Pombe aina zote zilikuwa zikiuzwa, madawa ya kulevya na kila aina ya uovu ulikuwa ukipatikana, sauti ya muziki ilikuwa kubwa sana muda wote. Palionekana kama Jehenum ndogo.

Geneviv alikuwa akitetemeka mwili mzima kwani hakuwahi hata mara moja kuingia kwenye kumbi za starehe, tena usiku kama huo. Vurugu za mle ndani zilimtia hofu akawa kama anayeota, Alice alilitambua hilo na akawa jirani kabisa kumuondoa wasiwasi. Ile wanaingia tu mlangoni, wote waliokuwa ndani waliwakodolea macho na zaidi kwa Geneviv ambaye uzuri sura yake na umbo lake ulimfanya kila mmoja kummezea mate.

Dakika chache baadae walikuwa wamezungukwa na wanaume kibao, kila mmoja akitaka kuondoka na Geneviv. Kwa kuwa Alice alikuwa mzoefu, alisimamia kisawasawa biashara na akataka anayetaka kuondoka na Geneviv atoe kwanza hela alizonazo na mwenye dau kubwa ndio atakaeondoka nae. Muda mfupi baadae mdau mwenye mihela kibao alishinda tenda kwa kutangaza dau kubwa kuliko wote, Geneviv akabebwa juu juu na wakaingia ndani ya gari moja la kifahari sana na kupotelea gizani. Kiumri yule mwanaume alikuwa sawa na baba yake, lakini kwa kuwa ndiye aliyetoa dau kubwa Geneviv akawa hana ujanja. Akaenda kugeuzwa kitoweo.

Mpaka inafika asubuhi, Geneviv alikuwa ameingiza pesa nyingi sana mpaka mwenyewe akawa anashangaa. Japokuwa kazi ile hakuipenda, alijikuta akitabasamu wakati Alice akimhesabia mauzo ya usiku.

“Ama kweli Geneviv una bahati. Yaani usiku mmoja tu umeingiza hela ambayo kwangu ningejiuza wiki nzima ndio nifikishe kama hii. Kweli kizuri hujiuza..”

Aliongea Alice na wote wakacheka na kugongesheana mikono. Bila kupoteza muda waliingia bafuni kuoga na baada ya kujiandaa Geneviv aliondoka huku akikimbia kwenda kumuangalia mama yake. Alipofika alianza kumuandalia kifungua kinywa mgonjwa, na kwa kutumia hela aliyoipata usiku, aliweza kununua na kuandaa chakula kizuri sana.

Huo ndio ukawa mwanzo wa kuzama kwenye tabia ya uchangudoa. Ikawa kila siku usiku, Alice anakuja kumchukua na wanaenda nyumbani kwake kujiandaa na baada ya hapo wanaingia mawindoni mpaka asubuhi.

Pamoja na kufanya yote hayo, Geneviv alikuwa hamsahau mama yake. Alikuwa akijitahidi kumlisha chakula kizuri na kumnunulia mashuka mazuri ya kisasa pamoja na nguo. Pale ndani kwao pakaanza kubadilika na taratibu Geneviv akaanza kuzoea kila kitu na kuona kama hakuna cha ajabu. Japokuwa nafsi yake ilikuwa ikimshtaki, hakuwa na la kufanya zaidi ya kujilazimisha kuzoea.

***
Baada ya mwezi mmoja baadae, Geneviv tayari alikuwa mzoefu na aliweza kukusanya pesa nyingi sana. Akaamua kuzitumia kumpeleka tena mama yake hospitali. Safari hii hakutaka kumrudisha tena palepale Planet health care, akaamua kumpeleka kwenye kliniki ya kisasa iliyokuwa imefunguliwa siku za karibuni, ikitoa huduma kwa wagonjwa wa moyo na matatizo ya kisaikolojia. Japokuwa matibabu katika kliniki ile yalikuwa ghali sana, Geneviv aliweza kumudu kutokana na pesa nyingi alizokuwa anazipata kwenye mchezo wao na Alice. Mama yake akaanza kupewa huduma bora huku akiangaliwa kwa ukaribu zaidi. Pesa ilikuwa ikifanya kazi yake.

Wakati hali ya mama yake ikianza kuwa nzuri, Geneviv alianza kujisikia dalili za ajabu. Alikuwa akisikia kichefuchefu na kutapika kila baada ya kula au kusikia harufu ya chakula. Tumbo lake nalo likaanza kuongezeka ukubwa taratibu.

“What the hell is this, mbona tumbo linazidi kuwa kubwa?” Geneviv alikuwa akijiuliza maswali peke yake akiwa bafuni kuoga baada ya kuona tumbo lake linazidi kuwa kubwa. Ilibidi amwambie rafiki yake Alice.

“Hiyo itakuwa ni mimba tu, lakini hilo ni tatizo dogo sana. Ntakupeleka kwa mtaalamu aiporomoshe, wala hata usiwe na wasiwasi”

Geneviv alishangaa namna ambavyo Alice alikuwa akirahisisha mambo. Alivyoelewa yeye, utoaji mimba ulikuwa ni hatari sana kwani huweza hata kusababisha kifo kwa mhusika. Pia ilikuwa ni dhambi kwa Mungu na hata vitabu vya dini zote vilipinga kabisa suala hilo.

Huo ukawa mtihani mwingine kwenye maisha ya Geneviv. Lakini alipofikiria kwa undani, aliona ni bora tu kufanya alichoshauriwa na Alice kwani hata kama angekataa, asingeweza kuzaa kwani umri wake ulikuwa bado mdogo na hata hivyo hakujua baba wa mtoto huyo ni nani kwani alishakuwa amekutana na wanaume wengi tayari, tena bila tahadhari yoyote. Akaamua kuufuata ushauri wa Alice, kutoa mimba.

***
Huwezi kuamini, baada ya Bi Patricia kufikishwa kwenye kliniki ile na kupewa tiba ya uhakika alianza kupata nafuu kwa haraka sana.Wiki moja tu baadae alishaanza kupata nguvu za kuinuka mwenyewe ingawa bado alikuwa hawezi kuongea chochote.

“Cant believe it, kweli Mungu mkubwa, yani mama leo unaweza hata kucheka…tulishakata tamaa, kweli Mungu mkubwa”
alikuwa akiongea Geneviv huku akimkumbatia mama yake kwa furaha pale kitandani.

Hali ya Bi Patricia ilishakuwa ya kuridhisha na sasa aliweza hata kuongea, ingawa bado alikuwa akiongea kwa shida. Geneviv aliendelea kumhudumia kwa kila kitu mpaka hali yake ikawa nzuri kabisa. Wale waliokuwa wamemkatia tamaa Bi Patricia kuwa lazima afe, walikuwa hawaamini kusikia kuwa amepata nafuu na karibu ataruhusiwa kurudi nyumbani. Wakawa wanaenda Hospitali kuhakikisha kama ni kweli alikuwa amepona.

“Kweli Mungu mkubwa, yaani yule mwanamke amepona, mi nilishamuhesabia kuwa tayari ni marehemu”Alisikika mama mmoja akiwahadithia wenzake baada ya kutoka hospitali. Upande wa pili Geneviv alikuwa akijiandaa kwenda kuitoa ile mimba kabla watu na hasa mama yake hajamshtukia kwani alihisi huenda akamuumiza zaidi mama yake atakapogundua kuwa ni mjamzito. Hakutaka hilo litokee, akawa anafanya maandalizi ya mwisho kabla ya kupelekwa kwa mtaalamu wa Abortion.
“Lakini mwenzio naogopa sana, nisije nikafa nikamuacha mama yangu peke yake, bwana mi siendi!”
Alikuwa akilalamika Geneviv kwa Alice.

“Sasa umeanza mambo ya ajabu, ntaacha kukusaidia mimi! Unafikiri mama yako akikuona na akigundua una mimba si ndio atakufa kabisa kwa presha? Fanya mambo kiutu uzima, acha ushamba” alikuwa akiongea Alice akionekana kughadhabishwa na woga wa Geneviv.

Baada ya Bi Patricia kupona, aliendelea kubaki hospitali kwa matibabu zaidi ili kuhakikisha tatizo lake halijirudii tena. Alimshukuru sana Mungu wake kwa kumuokoa kutoka kwenye shimo la mauti kwani alishafikia hatua ambayo hata yeye mwenyewe hakuwa na matumaini ya kupona. Alimshukuru zaidi mwanae Geneviv kwa yote aliyomfanyia kuokoa maisha yake.

Pamoja na hayo yote, Alishangazwa na mabadiliko ya mwonekano na tabia za Geneviv. Alishangaa kugundua kuwa Geneviv ameanza kutumia vipodozi vikali, ameanza kuseti nywele na anavaa mavazi ya ajabu ambayo hakujua ameyapata wapi kwani hakuwahi kumnunulia hata mara moja. Pia alikuwa akimiliki simu ya kisasa ya mkononi na zaidi urafiki wake na Alice ulionekana kushamiri na kila walikokwenda walikuwa wanaongozana.

Alitambua kuwa mwanae na Alice walikuwa marafiki tangu enzi wakiwa bado wadogo, lakini wakaja kutengana kutokana na Geneviv kuwa bize na shule. Pamoja na hayo alikuwa akizifahamu vizuri tabia za Alice na hasa ile ya uchangudoa. Akaanza kuingiwa na wasiwasi juu ya mwanae. Hakutaka kuendelea kuumiza kichwa kwa kumhoji maswali Geneviv kwani alihisi huenda akajikuta akirudi kwenye ugonjwa wake wa moyo. Akawa anangoja apone kabisa ndio akae na binti yake, lakini moyoni alishaanza kuhisi kitu.

Pamoja na hayo alikuwa akijiuliza ni nani aliyemleta kwenye Hospitali ya gharama namna ile ambayo imeokoa maisha yake. Alikuwa bado hajajua kuwa ni jitihada za mwanae kujitoa sadaka ndio zimemfanya apone. Alikuwa akimshukuru zaidi mungu kwa kumpa nguvu mpya na kumrudishia uhai. Mawazo juu ya kuondokewa na mumewe yalishaanza kupotea na akawa anawaza jinsi atakavyoanza maisha mapya na mwanae Geneviv.

*****
Geneviv na Alice walikuwa wakielekea kwenye Dispensari moja ya uchochoroni iliyokuwa ikisifika kwa kufanya kazi ya utoaji mimba. Machangudoa wote na wanafunzi wa kike waliokuwa wakipata mimba bila kutarajia pale ndio kilikuwa kituo chao cha kufanyia mauaji ya vichanga. Daktari Maguru alikuwa akipata pesa nyingi sana kwa kazi ile haramu. Japokuwa kila mtu alikuwa anafahamu kuhusu kinachofanyika pale, bado hakuna sheria zozote zilizokuwa zinachukuliwa dhidi yake.

Mabinti wengi walikuwa wakipoteza maisha kila uchao wakati wakitolewa ujauzito na wengine walikuwa wakiachwa na vilema vya maisha. Mapigo ya moyo ya Geneviv yalikuwa yakienda mbio kupita kawaida walipokuwa wakiikaribia Dispensari ile. Alice alimshika mkono na wakaingia mpaka ndani ambako walikuta foleni kubwa ya wasichana wengine nao wakiwa wanasubiri huduma. Kidogo wasiwasi ulipungua baada ya kuona kuwa hakuwa peke yake, na zaidi kulikuwa na wasichana wengi ambao kiumri walikuwa wadogo kwake.

Alibaki akijiuliza bila kupata majibu inakuwaje watoto wadogo kama wale aliokuwa anawaona mle ndani tena wengi wakiwa ni wanafunzi, walikuwa hawaogopi kufanya dhambi kama ile ambayo yeye aliiona kama mbaya zaidi na ni sawa na kuua kiumbe kisicho na hatia. Baada ya kungoja kwa muda mrefu kwenye foleni, hatimaye zamu yao ya kukutana na daktari Maguru ilifika.

Chumba cha daktari kilikuwa kikitoa harufu kali ya damu kama machinjioni. Kitanda kilikuwa kimeloa damu na hata nguo alizovaa daktari zilikuwa na damu. Kilichomtisha zaidi Geneviv ni vifaa vilivyokuwa vinatumika. Mikasi mikubwa, visu na vyuma vya ajabu-ajabu vilivyokuwa vimetapakaa damu vilimtisha mno.

“Mungu wangu… im finished! Alice mi naondoka, siwezi, siwezii”
Aliongea Geneviv kwa sauti kubwa na akawa anataka kukimbia na kutoka nje. Daktari Maguru alimuwahi na kumrudisha ndani. Alice akaanza kuwaka baada ya kuona Geneviv anataka kumwaibisha.

“Ni mara yake ya kwanza etii” daktari Maguru alimuuliza Alice huku akiwa anasafisha vifaa vyake tayari kwa kumshughulikia Geneviv. Alice aliitikia kwa ishara na wote wakacheka. Geneviv alikuwa akitetemeka kupita kiasi, hakuamini kama angeweza kutoka hai kwenye kile chumba kilichokuwa kinatisha kama machinjioni. Baada ya kumtuliza, daktari Maguru alianza kumhoji maswali machache huku akiendelea kuandaa vifaa vyake na kuvisogeza karibu na kitanda…

“Wenzio wanatoa hata zaidi ya mara nne na bado wanadunda mitaani ndio itakuwa wewe. Tulia nikufanyie mambo, mimi ndio Maguru mtaalamu mwenyewe, hakiharibiki kitu hapa.” Alikuwa akijisifia yule daktari huku akivaa gloves ndefu tayari kwa kazi. Alimtoa Alice nje na kubaki na Geneviv. Akamuamuru kuvua nguo na kubaki kama alivyozaliwa ili afanye kazi yake vizuri. Kwa kuwa alikuwa na shida, Geneviv alitii huku akijificha uso wake kwa aibu.

“Mtoto mzuri huyu sijapata kuona, lazima nimuonje kwanza kabla ya kazi… nikimuachia watanicheka sana.” Daktari Maguru alikuwa akijisemea kimoyomoyo huku udenda ukimtoka. Ikabidi atumie mbinu uchwara za kidaktari kumuweka sawa Geneviv. Alimdanganya kuwa njia yake ilikuwa ndogo hivyo ilikuwa ni lazime ailainishe kwa kumuingilia ndio aendelee na kazi. Geneviv hakuwa mbishi,

akamuacha afanye anachokitaka mradi mimba itoke. Baada ya kumfaidi bila huruma, Daktari Maguru aliendelea na kazi yake. Masaa mawili baadae alikuwa ameshamaliza kazi. Akafungua mlango na kumuita Alice aje amchukue Geneviv.

“Pole shosti huo ndio ukubwa. Ulikuwa unaogopa nini,mbona hujafa sasa!” alikuwa akiongea Alice kwa masihara hali iliyozidi kumkasirisha Geneviv. Alikuwa akisikia maumivu makali kupita kiasi. Akajikaza na kushuka kitandani, Alice akamshika mabegani na kuuzungusha mkono mwingine kiunoni, wakawa wanatoka huku Geneviv akichechemea. Walipofika nje ilibidi wakodi taksi kwani Geneviv alishindwa kabisa kutembea. Ikawapeleka mpaka kwa Alice ambako baada ya kufika tu, Alice alimchemshia maji ya moto na kuanza kumkanda. Geneviv alikuwa akilia sana kutokana na maumivu aliyokuwa akiyasikia
**********

Bi Patricia alishangaa kuona muda wa chakula cha mchana unapita bila ya Geneviv kumpelekea chakula wakati haikuwa kawaida yake. Akawa anaangaza macho huku na kule akidhani labda atamuona akija. Mpaka jioni inafika alikuwa hajafika. Muda mfupi baadae Alice alienda kumpelekea chakula akiwa peke yake. “Mwenzio yuko wapi, mbona hata mchana hakuja?” Bi Patricia alimdaka juu juu Alice na kuanza kumhoji maswali mfululizo. Ikabidi Alice adanganye…

“Geneviv anajisikia vibaya mama, kichwa na tumbo vinamuuma tangu asubuhi tulivyotoka hapa. Nimemuacha amepumzika lakini anaendelea vizuri”
Bi patricia hakutaka kuhoji zaidi, akaishia palepale ingawa alipomkazia macho Alice alisoma kitu kwenye macho yake. Muda ulipoisha akondoka na vyombo kurudi nyumbani. Bi patricia alishaingiwa na wasiwasi juu ya mwanae Geneviv, akabaki kumuachia Mungu.

Tumbo liliendelea kumuuma Geneviv bila kupata nafuu. Japokuwa alikuwa amepewa dawa za kumaliza maumivu na kusafisha tumbo, aliugulia usiku kucha akijigalagaza kitandani kwa Alice. Alikuwa akisikia maumivu makali sana ambayo yalikuwa yakiongezeka kadri muda ulivyokuwa unaenda. Mpaka kunakucha, alikuwa hajapata hata tone la usingizi. Kutokana na maumivu, alishindwa kumuandalia kifungua kinywa na kumpelekea mama yake hospitalini. Ikabidi Alice aende tena peke yake.

“Vipi mbona umekuja tena peke yako, ina maana bado Geneviv hajapata nafuu, au ni malaria? Lakini bahati nzuri na mimi nimesharuhusiwa, nisubiri tuondoke wote”

Aliongea Bi Patricia wakati akipata kifungua kinywa alicholetewa na Alice. Wasiwasi ulianza kumuingia Alice baada ya kusikia mama yake Geneviv ameruhusiwa kurudi nyumbani. Alijua lazima siri yao ingefichuka… “Sijui itakuwaje huko nyumbani akienda kumuona Geneviv, leo tumepatikana” alikuwa akijisemea Alice wakati akimsaidia mama Geneviv kufungasha vitu vyake tayari kurudi nyumbani baada ya kupona na kuruhusiwa kutoka hospitali.

Bi Patricia alikuwa tayari amekusanya vitu vyake vyote tayari kwa safari ya kurudi nyumbani baada ya kukaa Hospitali kwa muda mrefu. Alice alikuwa akimsaidia na muda mfupi baadae wakawa ndani ya gari tayari kwa kurudi nyumbani.

Alice alishindwa kuificha hofu yake kwani alikuwa akifahamu fika hali aliyomuacha nayo Geneviv. Alijua lazima tatizo lingine kubwa lingetokea baada ya Bi Patricia kufahamu mchezo mchafu walioucheza na Geneviv. Akaamua kufanya kitu ili kunusuru shari iliyokuwa jirani kutokea.

Geneviv alikuwa akiendelea kuugulia maumivu makali ya tumbo. Mara ujumbe mfupi wa simu uliingia kwenye simu yake ya mkononi aliyoinunua siku za karibuni. Ulikuwa umetoka kwa Alice na ulisomeka hivi…

… “Shosti leo tumepatikana, sijui utamweleza nini mama yako…lazima atagundua tu kuwa umefanya abortion. Hivi saizi ndio tunatoka nae hospitali, amesharuhusiwa. Anza kujiandaa kwa msala!”

Baada ya kumaliza kuusoma ujumbe ule kwenye simu yake, Geneviv alijikuta ameshtuka
Kupita kawaida. Hakutegemea kuwa mama yake angetoka Hospitali siku ile, na zaidi kilichomchanganya ilikuwa ni hali aliyokuwa nayo.

Alijua lazima mama yake angemgundua na alijua ataumia sana akiufahamu ukweli. Akajikuta amepona ghafla… alijitahidi kuinuka kitandani na kwa haraka akavaa vizuri.

Lengo lake ilikuwa ni kumkimbia mama yake ili kuepusha matatizo mengine ambayo yangetokea baada ya mama yake kuujua ukweli.

Alipokuwa tayari alitoka mpaka ndani mwao na kwa haraka akachukua kalamu na karatasi na kuandika ujumbe akimdanganya mama yake kuwa kichwa na tumbo vimemzidia hivyo ameenda hospitali. Akili yake ilikuwa ikifanya kazi kwa spidi ya ajabu. Alipomaliza kuandika uongo alitoka na akawa anajivuta kuelekea mtaa wa nyuma. Alipohakikisha amefika mbali na kwao, alimpigia simu dreva teksi aliyekuwa anakuja kuwachukua usiku na Alice, na akamwambia aende haraka kumchukua.

Muda mfupi baadae akawa ameshafika na kumfungulia Geneviv mlango. Akaingia ndani ya gari nakumuamuru dereva aondoe gari upesi.

“Mbona leo mapema aunt, si nikupeleke kiwanja kilekile cha sikuzote?” Aliuliza dereva Taksi wakati akiwasha gari na kuondoka. Alikuwa amezoea kuwachukua Alice na Geneviv na kuwapeleka kwenye biashara yao ya Uchangudoa, akajua na muda huo ndiko Geneviv alikokuwa anaenda.

Geneviv hakujibu kitu zaidi ya kuendelea kuugulia tumbo. Alipanga kwenda gesti yoyote na kupanga chumba mpaka apate nafuu ndio arudi kwa mama yake. Alijua yale maumivu ni ya muda mfupi na yangeisha kama daktari Maguru alivyokuwa ameahidi na kumpa moyo.

“Nishushe hapo kwenye hiyo gesti…aliongea Geneviv kwa sauti ya chini akionyesha namna alivyokuwa akisikia maumivu. Alimlipa dereva pesa yake na akajikongoja mpaka ndani alikochukua chumba self contained na kujifungia. Tumbo liliendelea na sasa alishindwa kuvumilia, akawa analia kimyakimya.

“Eeeh Mungu nisamehe dhambi zangu! Niponye tumbo langu nirudi nyumbani kwa mama, why me my Lord!” alikuwa akiongea Geneviv huku akilia.

*****
Bi Patricia aliongozana na Alice mpaka nyumbani, na akamsaidia kushusha mizigo na kuingia ndani. Alipoingia tu alianza kuita…

“Geneviv….Genny… where are you my dear, im back…uko wapi?” Alikuwa akiita Bi Patricia huku akizunguka huku na huko kumtafuta Geneviv, nyumba ilikuwa kimya.

Alienda mpaka chumbani kwake lakini hakumkuta. Akiwa huko alishangaa jinsi chumba cha mwanae kilivyobadilika. Alikuwa amenunua vipodozi vingi na kuvijaza mezani, pia alikuwa amenunua nguo nyingi alizozijaza kwenye begi kubwa. Mashuka na mablanketi nayo yalikuwa mapya…Bi Patricia akabaki mdomo wazi.

Alishindwa kuelewa ni nani aliyemnunulia Geneviv vitu hivyo ambavyo kwa harakaharaka aliviona kuwa na thamani kubwa. Akiwa bado anashangaa mabadiliko makubwa aliyokuwa nayo Geneviv, aliona ujumbe kitandani na kwenda kuusoma. Ulikuwa umeandikwa na Geneviv akieleza kuwa ameenda Hospitali.

Bi Patricia hakutaka kuamini kwa haraka kama ni kweli Geneviv ameenda Hospitali kama alivyoandika. Akiwa bado anaendelea kukisanifu kile chumba, aliona kiboksi kidogo chenye dawa kikiwa pembeni ya kitanda. Akakisogelea na kukichukua. Alipokitazama vizuri alijikuta akisisimkwa na mwili kupita kawaida.

Zilikuwa ni dawa ambazo alizigundua haraka kuwa ni za kusafisha kizazi na nyingine zikiwa ni vidonge vya kuzuia mimba, Alijikuta akiishiwa nguvu. Mpaka hapo alishapata picha kamili ya kilichokuwa kikiendelea.

Akatoka na kurudi sebuleni ambako alimkuta Alice akiendelea kusafisha na kupanga vyombo. Alimtazama kwa hasira akiamini yeye ndie chanzo cha Geneviv kuharibika.
“Hebu niambie ukweli, mwenzio yuko wapi?” Bi Patricia alimbana Alice na kutaka amueleze ukweli aliko Geneviv. Alice akawa anatetemeka kwa hofu. Akazidi kubanwa kwa maswali mfululizo na mwisho akajikuta akitoa siri.

“mama ukweli ni kwamba Geneviv anaumwa sana tumbo…Tusamehe ni shetani alitupitia, mimi ndio niliempeleka kutoa mamba tukiogopa kukuumiza zaidi kwa kuwa ulikuwa bado hujapona vizuri, tusamehe”

Whaaat! Geneviv ametoa ujauzito, Mungu wangu wee, ni nani aliyempa? Bora angejifungua tu ningelea mjukuu, si ameshaharibika moja kwa moja sasa, Oooh My Lord, kwanini matatizo hayaniishii mimi? Nimekosa nini kwa Mungu maskini mimi!”
Bi Patricia aliongea kwa uchungu na kuanza kulia.

“Mama usilie, utaanza kuumwa tena, Geneviv atapona tu, mbona hata mimi iliwahi kunitokea na nikapona” alikuwa akiongea Alice akimbembeleza Bi Patricia. Kauli ile ilimfanya Bi Patricia amtazame usoni Alice kwa hasira. Pamoja na kuwa yeye ndio alikuwa chanzo, alijikuta akimuonea tena huruma. Hakuna kitu ambacho kilikuwa kikimuogopesha kama kutoa ujauzito.

Akajikuta akijifikiria jinsi watoto wa siku hizi walivyoharibika. Enzi wakati yeye akikua, ilikuwa ni vigumu sana kwa watoto wadogo kama Alice kujihusisha na umalaya na kujikuta wakitoa mimba zisizohesabika. Ilikuwa ni kama laana.

Akapiga moyo konde na kuamua kuangalia njia ya kumsaidia Geneviv ingawa tayari alikuwa amechelewa. Wakaanza kumtafuta na kazi haikuwa ngumu kwani Alice alimpigia simu na kumuuliza alipo huku mama yake akisikiliza.

Geneviv alijibu huku akilia kuonyesha kuwa hali yake ndio inazidi kuwa mbaya. Kwa haraka Bi patricia akiongozwa na Alice wakatoka na kuanza kukimbia kuelekea kule walikoelekezwa na Geneviv.

Kila aliyemuona Bi Patricia akikimbia mitaani alishangaa na wengine wakawa wanahisi kuwa labda amerukwa na akili kwani ni siku hiyohiyo ndio alikuwa ametoka Hospitali. Baadae wakafika pale walipoelekezwa. Wakaingia mpaka mapokezi ambapo baada ya kuulizia waliambiwa kuwa binti huyo aliingia muda mchache uliopita ingawa alikuwa akionekana amezidiwa sana.

“Yuko chumba gani jamani, ni mwanangu…” Aliongea Bi Patricia huku akihema kwa nguvu. Nguo alizozivaa aliziona kama mzigo, akawa anahaha huku na kule kama aliyepagawa. Yule mhudumu wa mapokezi alitoka na kuwapeleka chumba alichoingia Geneviv. Walipofika karibu na mlango walisikia Geneviv akilia kwa uchungu na ghafla akanyamaza, kukawa kimya…

“Geneviv! Geneviv! Fungua mlango, ni mimi mama yako… fungua please, sikufanyi chochote mwanangu…”
Bi Patricia alikuwa akigonga mlango kwa nguvu huku akimsihi mwanae Geneviv afungue kwani alikuwa amejifungia kwa ndani. Pamoja na kugonga kwa nguvu kwa muda mrefu, bado kulikuwa kimya kabisa.

“Tuvunje mlango…inawezekana amepoteza fahamu ndani. Tumuwahi asije akapoteza maisha.”
“Ngoja nikachukue funguo ya akiba,msivunje kwanza mlango.”

Mhudumu alitoka mbio kwenda kuchukua ufunguo wa akiba. Bi Patricia alikuwa hajiwezi kwa wasiwasi. Hakujua mwanae ana hali gani mle ndani. Sekunde chache baadae mhudumu alirejea na funguo mkononi. Wakafungua mlango na wote wakaingia ndani.
“Mungu wangu weee! Mwanangu jamani…uuuuwii!” Bi Patricia alianza kupiga mayowe kwa sauti. Geneviv alikuwa amejilaza sakafuni akiwa amelalia tumbo,mwili wake ukiwa umetulia tuli. Ilionekana kama maumivu yalikuwa yamemzidia kiasi cha kumfanya apoteze fahamu.

Alipomsogelea na kusikiliza mapigo yake ya moyo, yalikuwa bado yanapiga kuonyesha alikuwa bado yuko hai. Mama usilie, cha msingi hapa tumuokoe Geneviv…

Harakati nyingine zikaanza haraka mno. Akabebwa juu juu mpaka nje ambako taksi iliitwa haraka na akapakiwa. Safari ya kumkimbiza Hospitali ikaanza mara moja. Ongeza mwendo dereva, mwili wake umeanza kuwa wabaridi… dereva akanyoosha mguu kwenye excretor na kukanyaga mafuta mpaka mwisho.

Muda mfupi baadae wakawa tayari wameshafika Hospitali. Akabebwa juu ya kitanda cha wagonjwa na kukimbizwa ndani na manesi.
“Huyu mgonjwa si ndio yule binti Geneviv aliyekuwa anamuuguza mama yake hapa, imekuwaje tena… na werwe mama si umeruhusiwa kutoka hapa Hospitali asubuhi ya leoleo, imekuwaje tena.

“jamani wasaidieni kwanza kumuokoa mtoto, maswali mengine baadae” Ilibidi wote wawili, Geneviv na mama yake waingizwe upya wodini kwani Bi Patricia naye alianza kuhisi tatizo lake linamrudia baada ya kuona hali aliyokuwa nayo Geneviv. Mama wewe usipanic kwa sababu utakosa yote sasa, daktari alikushauri ukifika nyumbani upumzishe mwili…jikaze kama mwanamke, mwanao atapona.

Ilibidi kazi ya ziada itumike kumtuliza Bi Patricia na kuokoa tatizo lake la shinikizo la chini kulipuka upya, ilibidi wamchome kwanza sindano ya usingizi huku wengine wakijitahidi kuokoa maisha ya Geneviv. “Jamani huyu binti ameharibiwa vibaya sana! It seems amefanya abortion, hebu ona…” manesi waliokuwa wakimhudumia Geneviv walikuwa wakishangaa hali waliyoiona kwa Geneviv.

“Hata akipona sijui kama ataweza kupata mtoto maishani mwake, she got the loose cervix (Mlango wake wa uzazi umefunguka na kubaki wazi) ”

“Maskini, mbona hafanani na kufanya umalaya, usoni anaonekana mpole kumbe muuaji”
“Tusimhukumu bure, hatuwezi kujua kilichofanya atoe , kwanza hayatuhusu sisi tufanye kazi yetu hayo mengine atajua mwenyewe na wazazi wake.”

Wale manesi walikuwa wakizidi kuulizana maswali wenyewe kwa wenyewe huku wakiendelea kumhudumia Geneviv. Baada ya muda mrefu, Geneviv alizinduka na kurudiwa na fahamu zake. Mama yake naye alishazinduka muda mwingi na akawa amekaa juu yaq kitanda chake akimtazama mwanae kwa huruma. Baada ya kurudiwa na fahamu, Geneviv alianza kuangaza macho huku na kule kama anayeshangaa amefikaje mahali pale. Mara akageukia upande alikokuwa mama yake. Bi Patricia alikuwa kimya akimtazama.

“Mum im sorry, ni shetani alinipitia… samahani mama! Sikukusudia kufanya hivi, basi tu imetokea…” Geneviv alianza kuloloma akimuomba msamaha mama yake. Hakujionea huruma yeye kuliko mama yake.

Bi Patricia alijibu kwa upole…”Mwombe msamaha Mungu wako kwa dhambi kubwa uliyoifanya, na wala si mimi”
“Mama ni Alice ndio alinidanganya, mi nisingeweza kabisa, kwanza nilikataa”

“Yaani hapo ulipo una utoto gani wa kudanganywa na wewe unakubali.Kila mtu atabeba mzigo wake…Alice wa kwake na wewe wa kwako, ila nina wasiwasi na afya yako baada ya kufanya dhambi kama uliyoifanya…inawezekana hata ukipona ukakosa uwezo wa kuzaa, soo sorry for you”

Geneviv alizidi kupatwa na uchungu baada ya kuambiwa kuwa kuna uwezekano wa kuja kushindwa kuzaa akiwa mkubwa, alibaki kujilaumu mno… “Ninge…” alishindwa kumalizia na akawa analia. “Hata ukilia sana mwanangu huwezi kuubadili ukweli. Tunamsikitikia mtu anayepatwa na jambo kama hilo bila kutegemea, lakini wewe ulikusudia…unastahili matokeo yake na wala hakuna wa kumlaumu” Bi Patricia alizidi kumchoma Geneviv kwa kumpa ukweli.

“But mum I did it for the sake of you (Lakini mama nilifanya haya yote kwa ajili yako)” aliongea Geneviv kwa sauti ya juu ikiambatana na kilio. Bi Patricia alishtuka kusikia kauli ile, hakuelewa Geneviv ana maana gani. Ilibidi ashuke kitandani alipokuwa amelazwa na kusogeleaa pale alipolala Geneviv. Ikumbukwe kwamba walikuwa wamelazwa vitanda viwili vilivyofuatana na Bi Patricia hakupata mshtuko mkubwa kama awali kwa hiyo hali yake ilirejea kuwa nzuri mara tu baada ya kurejewa na fahamu.

Ilibidi amsogelee jirani kabisa ili aweze kuelewa vizuri alikuwa na maana gani kwa kauli ile aliyoitoa( But mum I did it for the sake of you). “Hebu nieleze vizuri nini kilichokusibu na unamaanisha nini kusema hivi…” Ilibidi Bi Patricia awe mpole ili apate ukweli. Geneviv alifuta machozi na kukaa vizuri tayari kuanza kumueleza mama yake kila kitu. “mama kipindi kile wakati unaumwa na umezidiwa kabisa, hakuna mtu aliyekuwa ananisaidia kukuuguza. Ilifika kipindi hata chakula kikaisha nyumbani, nikawa nashindwa hata kukuandalia uji na mimi nikawa nalala bila kula au siku nyingine nakunywa uji siku nzima.

Nilipoona hali inazidi kuwa mbaya na wewe unazidi kuteseka, niliamua kuanza kuomba misaada kwa majirani na wapiti njia, lakini bado walinisaidia kidogo tu na hali iakzidi kuwa mbaya. Niliukuwa naumia sana kwa hali ulivyokuwa nayo na hasa nilipokumbuka kuwa baba tayari ametutoka. Ikabidi niende kwa rafiki yangu Alice kuomba ushauri…” Alpofika hapo, Geneviv alikatisha kusimulia na akawa analia kwa kwikwi.

Hapo kidogo Bi Patricia alianza kupata picha ya matukio yaliyoendelea wakati akiwa kwenye usingizi wa nusu kifo. Alijikuta akianza kumuonea huruma mwanae. “Nyamaza usilie, endelea kueleza…”

Geneviv akaendelea kusimulia “Nilipoenda kwa Alice alinifundisha kutafuta hela kwa kujiuza usiku, nikawa nafanya uchangudoa” … “Whaaat, yaani na wewe ukakubali kumsikiliza, si bora ungetafuta msaada sehemu nyingine, ungetafuta hata kazi ya uhausigeli mwanangu…kwa hiyo ukawa changudoa? My God…”

Geneviv aliendelea kusimulia kila kitu jinsi alivyofanya kazi hiyo na mpaka akapata pesa za kutosha kumpeleka mama yake hospitali ya kisasa mpaka akapona.Bi Patricia alijikuta akisisismka mwili mzima. Hakutegemea kuwa mwanae anaweza kujitoa sadaka namna ile kuokoa uhai wake. Alibaki ameduwaa akimkodolea macho Geneviv akiwea kama haamini kile alichokisikia. Geneviv hakuishia hapo, akaendelea kueleza mpaka alivyopata ujauzito akiwa anaendelea na kazi ya kujiuza na jinsi ambavyo Alice alimpeleka kuitoa. Hakuficha kitu, alieleza yote. Bi Patricia akawa anajihisi kama yuko ndotoni, aliona kuwa kumbe alikuwa akimlaumu Geneviv kimakosa, akaanza kujisikia vibaya kwa kuwa hakuwa amemtendea haki kumshutumu kuwa alijitakia wakati bila msaada wake asingekuwa hai mpaka muda huo.

Basi mwanangu, yaliyopita tuyasahau tumwombe Mungu atusamehe dhambi zetu zote na tumshukuru kwa kutufanya tuwe hai mpaka muda huu kwani tuliyopitia yeye ndio anajua”
Wakashikana mikono na kuanza kusali kwa pamoja. Muda mfupi baadae nesi aliingia na kumuita Bi Patricia wazungumze pembeni.

“Nasikitika sana mama kukwambia juu ya hali ya mwanao kiafya. Najua utaumia zaidi lakini sina jinsi zaidi ya kukwambia ukweli” Aliongea yule nesi wakiwa wameytoka nje ya wodi alikolazwa Geneviv. Kuna nini tena nesi, niambie tu nitajikaza. Afya yake imefanya nini, niambie tu yule ni mwanangu… niko tayari kusikia chochote, usinifiche kitu tafadhali. Bi Patricia alianza kutetemeka wakati nesi akijiandaa kumwambia alichomuitia.

Nesi alimtazama Bi Patricia alivyokuwa amechanganyikiwa wakati akitaka kuelezwa hali ya afya ya mwanae. Akagundua kuwa amehisi kitu tofauti na alichotaka kuambiwa, akajikuta akitabasamu.
“Kwani we unafikiria mwanao ana nini? Mbona umeshtuka sana wakati ni suala la kawaida? Okey, mwanao amegundulika kuwa ana…”

Nesi alishindwa kumalizia kauli yake kwa hali aliyokuwa nayo Bi Patricia. Alivyoonekana alihisi kuwa nesi anataka kumwambia kuwa Geneviv ameambukizwa ugonjwa hatari wa Ukimwi, lakini haikuwa hivyo. Alihisi vibaya na kujikuta akipata majibu tofauti akilini mwake hata kabla ya kuambiwa. Geneviv hakuwa na Ukimwi kama mama yake alivyodhani…

“Punguza hofu mama tuangalie namna ya kumsaidia mtoto. Vipimo vinaonyesha ameambukizwa ugonjwa wa Kaswende lakini ondoa hofu kwani ugonjwa huu unatibika na atapona kabisa!”

“Sio Ukimwi nesi, au unanificha?” Bi Paticia alikuwa haamini kama ni kweli mwanae amesalimika kupata gonjwa hatari la Ukimwi. Alijikuta akiinua mikono mbele ya nesi na kumshukuru Mungu kwa sauti… “Oooh! Ahsante Mungu, umetenda miujiza yako kwa kumnusuru mwanangu kutoka kwenye mdomo wa Jehanum, Amen”

Kwake tatizo la mwanae kuja kushindwa kupata mtoto tena halikumpa taabu akaamini Mungu atafanya maajabu yake tena, cha msingi mwanae yuko salama na anaendelea kuishi. Akarudi wodini huku akikimbia, akaenda kumkumbatia mwanae pale kitandani na wakaendelea kusali na kumshukuru Mungu. Geneviv alianzishiwa dozi ya Kaswende aliyoendelea nayo kwa muda wa wiki mbili. Hatimaye alipona kabisa na wakaruhusiwa kurudi nyumbani.

“Mwanangu inaonekana shetani anatunyemelea sana kutaka kutuangamiza kwa sababu matatizo ndani ya familia yetu hayaishi, likiisha hili linaanza jingine, yaani kila siku sisi ni watu wa matatizo tu! Inabidi tufanye kazi ya ziada ya kumuomba Mungu.” Bi Patricia alikuwa akiongea na mwanae Geneviv usiku kabla ya kulala. Wakaona njia bora ni kufunga kwa wiki nzima wakikesha kusali usiku na mchana.

“mama mi siwezi kufunga, sijawahi hata siku moja halafu bado mwili hauna nguvu!” Geneviv alianza kutoa visingizio kukwepa kazi ngumu ya kufunga. Bi Patricia alikuwa mkali katika hilo na ikawa ni lazima kufunga na kusali. Siku nzima walikuwa wakijifungia ndani mwao wakisali na kutubu dhambi zao mbele za Mungu wao. Waliendelea hivyo kwa muda wa siku saba mfululizo.

Baada ya siku saba kuisha, mabadiliko makubwa yalianza kutokea. Kwanza Bi Patricia alipokea barua kutoka kazini kwake ikimtaka kurudi kazini na kuendelea na kazi. “The storm is over my dear! Umeamini kuwa Mungu yupo na anasikia maombi yetu eeeh?”
Bi Patricia alikuwa akiongea na mwanae mara baada ya kuisoma ile barua ya kumtaka arudi kazini. Kesho yake akaanza kujiandaa kurudi kazini.

Matumaini mapya yalianza kurejea na lile giza lililotanda kwa muda mrefu maishani mwao likaanza kupotea na maisha kujawa na nuru mpya. Hawakuacha kumshukuru Mungu wao kwa kila kitu. Siku iliyofuata, Bi Patricia alijiandaa tayari kwa kwenda kazini baada ya siku nyingi kupita. Geneviv ilibidi abakie pale nyumbani. “Usiondoke mwanangu umesikia, ukae hapahapa maana huko mitaani kumejaa matatizo, we mwenyewe unafahamu…kosa sio kosa ila kurudia kosa,Mungu akulinde”

Bi Patricia alikuwa akimuaga mwanae wakati akitoka kuelekea kazini. Baada ya kuondoka, Geneviv alijifungia ndani na akachukua Biblia na kuanza kuisoma. Hakuwa na mazoea ya kusoma Biblia lakini kwa miujiza aliyotendewa na Mungu hadi akawa hai mpaka muda huo, alijikuta akimpenda Mungu. “Thank you my Lord…” aliongea Geneviv kwa sauti ya chini akiwa amejifungia chumbani kwake.

Muda mfupi baadae akasikia mlango wa nje ukigongwa, akanyanyuka huku ameshikilia Biblia yake mkononi na kwenda kufungua mlango… Alikuwa ni Alice.
“ Vipi shosti, naona saizi umeshapona na kuwa fit kabisa…basi leo kuna bonge la stori nataka kukupa.”

Aliongea Alice kwa manjonjo na uchangamfu kama kawaida yake, lakini Geneviv hakumuonyesha uchangamfu kama walivyozoeana. Akamkaribisha ndani wakakaa sebuleni. Alice alishtushwa na hali aliyokuwa nayo Geneviv na alipomtazama vizuri mkononi alikuwa ameshika Biblia.
“He Geneviv umeanza lini kusoma Biblia? Mbona makubwa! Unajizeesha bure shosti, achana na mambo ya kizamani,weka huo mbiblia wako pembeni nikupe stori yenyewe”

Alice aliongea na kumpokonya Geneviv Biblia na kuitupia juu ya meza. Akaanza kumhadithia Geneviv kilichomleta.
“basi leo usiku kutakuwa na bonge la tamasha pale Valentino cassino, kiwanja chetu. Unaambiwa muziki utakesha mpaka asubuhi, halafu leo ni watu wenye hela zao ndio watakaoruhusiwa kuingia…wazungu, wahindi na mapedeshee, jiandae ntakuja kukuchukua tukale bata… mwenzio nishapata mtu wa kutoka nae ameniambia atanipa dola mia moja mpaka asubuhi, wee usipime mtoto wa kike…”

Alice alikuwa akiongea maneno mengi mno mfululizo. Alikuwa anampa taarifa Geneviv kuwa usiku wa siku hiyo waende kwenye eneo lao walilokuwa wakifanyia uchangudoa kwa kuwa kuna sherehe kubwa imeandaliwa. Geneviv alimtazama kwa dharau Alice bila kujibu chochote. Akainuka na kwenda kuichukua tena Biblia yake, akafungua na kuendelea kusoma akimuacha Alice akizidi kuongea.

“Yaani mi nakupa dili la maana unajifanya uko bize sio, dharau au kitu gani. Umeshawahi kusikia wanajeshi wakiwa vitani halafu mmoja akaasi huwa wanamfanya nini? Kama umeamua kuokoka wewe ni muasi kwetu, ntakushikisha adabu.”

Alice alinyanyuka na kutoka huku akibamiza mlango kwa nguvu. Geneviv alitikisa kichwa kwa kumsikitikia, akaenda kuufunga mlango na kurudi chumbani kwake. Hakutaka kumpa tena shetani nafasi ya kumtawala, aliamua kubadilika kwa moyo wake wote.

Geneviv aliendelea kumwomba Mungu ambadili rafiki yake Alice ili siku moja na yeye aachane na tabia ya uchangudoa. Hakutishika na vitisho alivyoachiwa na Alice, zaidi akawa anamuombea mema kwa Mungu. Muda mfupi baadae alisikia mlango ukigongwa na alipotoka kufungua, alikutana na rafiki yake wa kiume waliyekuwa wakisoma darasa moja, Joackim au Kim kama waliovyozoea kumuita shuleni. Geneviv alishtuka kumuona Kim amekuja nyumbani kwao kwani hakuwahi kufika hapo kabla.

“Karibu ndani kaka Kim, vipi habari za siku nyingi” Geneviv alimkaribisha Joackim ndani kwa uchangamfu na wakaanza stori zao za shule. Joackim alikuwa amekuja kutaka kufahamu kwa nini Geneviv aliacha shule ghafla na hata mtihani wake wa mwisho hakufanya. Alikuwa hafahamu chochote kilichomtokea zaidi ya kusikia juu juu kuwa alikuwa anaumwa na alifiwa na baba yake mzazi, mzee Rwakatare.

Geneviv alijisikia aibu kidogo kwani alihisi Kim anafahamu yote yaliyomtokea na hasa lile la kubakwa na mwisho uchangudoa na alikuwa amekuja kumsanifu. Alikuwa mgumu wa kueleza kilichomfanya mpaka akaacha shule zaidi ya kueleza kwa kifupi kuwa alikuwa na matatizo makubwa likiwemo la kuondokewa na baba yake. Kim hakutaka kuzidi kumdadisi maswali mengi kwani alihisi anamkumbusha machungu aliyoanza kuyasahau. Kim akamsimulia yote yaliyotokea baada ya yeye kuacha shule mpaka walipofanya mtihani wao wa mwisho wa kuhitimu elimu ya msingi.

Alimueleza kuwa wao tayari wameshaanza kidato cha kwanza na katika darasa lao hakuna aliyefeli, wote walikuwa wamechaguliwa kuendelea na sekondari. Taarifa zile zilimuumiza sana Geneviv akajikuta akishindwa kuyazuia machozi. Kim alipoona Geneviv analia, alimsogelea jirani na akawa anambembeleza.

“bado una nafasi ya kuendelea mbele dada Geneviv, unaweza kuwaomba walimu ukarudia tena darasa la saba halafu mwakani na wewe ukaanza sekondari. Pole usilie…yote yana mwisho”
Kwa mara ya kwanza Geneviv alihisi akifarijika mno. Uwepo wa Kim pale na jinsi alivyokuwa akimbembeleza kwa upole ulimfanya ajihisi kama anaingia kwenye dunia mpya.

Wakatazamana usoni na macho yao yakagongana, Geneviv akahisi kama moyo unamwenda mbio, akaangalia pembeni kwa aibu za kike. Alijikuta akisahau matatizo yote aliyopitia na taratibu tabasamu lililopotea kwa miaka mingi usoni mwake likaanza kuchanua upya.
“Ahsante kaka Kim, Mungu akubariki kwa kunifariji…sio siri siku ya leo imekuwa tofauti sana kwangu, sina cha kukulipa kwa wema wako kwangu.”

Waliendelea na mazungumzo ya kawaida kwa muda mrefu na baadae Kim akaaga na kuondoka. Geneviv alibaki akijiuliza maswali mengi kichwani bila kupata majibu. Kim alikuwa amemfanyia ‘Surprise’ kubwa kwani tangu aanze kuandamwa na mikosi, hakuna rafiki yake hata mmoja kutoka shule aliyewahi kuja kumtembelea. Kim ndio alikuwa wa kwanza.

Kingine kilichomfanya ajiulize maswali mengi ni jinsi alivyokuwa akijihisi wakati akibembelezwa na Kim. Alikuwa akijihisi kama amehama kutoka kwenye dunia aliyoizoea na kuingia ulimwengu mpya. Alijikuta akitaabasamu peke yake. Akachukua Biblia yake na kuendelea kujisomea.

Jioni mama yake alirudi na kumkuta akiwa amejifungia chumbani. Tofauti na siku zote, leo alionekana kuwa na furaha huku sura yake ikiwa imejawa na tabasamu. Alimpokea mama yake kwa furaha, na akamhadithia juu ya ujio wa wageni wawili, Alice na Joackim.

“Huyo Alice amefuata nini tena hapa, sitaki kabisa kumuona hapa nyumbani. Akija tena umwambie sitaki kumuona akikanyaga hapa”
Alikuwa akiongea Bi Patricia kwa jazba.

“Mum lakini mi naona tutafute jinsi ya kumsaidia kwani na yeye hapendi kufanya anayoyafanya ila ni hali ya maisha ndio inamlazimisha kujiuza. Tumsaidie atabadilika”
Aliongea Geneviv kwa busara sana kiasi cha kumfanya mama yake amuunge mkono. Lakini alitoa onyo kuwa Alice asiruhusiwe kuingia ndani kama yeye hayupo na hata mazungumzo yao wawe wanayafanya na yeye akiwepo. Geneviv alimkubalia mama yake.

“Na huyo mwingine aliyekuja ni nani?” Bi Patricia alizidi kumdadisi Geneviv. Alitoa tabasamu pana kabla ya kujibu. Alimueleza kuwa ni rafiki yake wa siku nyingi waliyekuwa wakisoma pamoja na alikuwa amekuja kumtembelea kumjulia hali. Alieleza kila kitu walichozungumza naye.
“Kumbe ndio maana leo una furaha hivyo, natamani kumfahamu huyo Kim aliyekufanya ufurahi namna hiyo, ikibidi nimpe zawadi! Yaani naona amekusahaulisha machungu yako yote… huyo ndio rafiki mwema anayekukumbuka hata ukiwa na shida.”

Wote walifurahi na wakawa wanacheka wakionekana kusahau yote yaliyowapata siku za nyuma. Wakaanza kuandaa chakula cha jioni na baada ya kula, waliingia chumbani wakaanza kusali na kumshukuru Mungu kwa yote aliyowafanyia. Baada ya kusali kwa muda mrefu hatimaye walilala.

Aubuhi na mapema, walisikia mlango ukigongwa… “nani tena asubuhi yote hii?” aliongea Bi Patricia kwa sauti ya chini akimuamsha mwanae Geneviv. Wote waliamka na kwenda kufungua.
“Hee, kumbe ni wewe shemeji, karibu sana…habari za nyumbani? Baba na mama hawajambo?”

Alikuwa ni mdogo wa marehemu mzee Manuel Rwakatare, alikuwa akiitwa Magafu, waliyezaliwa tumbo moja na baba yake Geneviv. Alikuwa amefunga safari ndefu kutoka Musoma nchini Tanzania waliko wakwe wa Bi Patricia kuja kuleta ujumbe aliotumwa kutoka kijijini kwao. Baada ya kukaribishwa na kuingia ndani, Bwana Magafu Rwakatare alitoa barua aliyopewa kutoka kijijini kwao na kumkabidhi Bi Patricia.

Hakuifungua kwanza, wakawa wanaendelea na mazungumzo mengine. Katika mazungumzo yale, Bi Patricia aligundua kitu ambacho kilimfanya aishiwe nguvu. Ilivyoonekana ujumbe uliokuwa ndani ya ile barua haukuwa mzuri. Tangu kifo cha mumewe, hakuna ndugu hata mmoja aliyewahi kuja kuwajulia hali ingawa walikuwa wakifahamu fika kuwa baada ya kuondokewa na mumewe Bi Patricia na mwanae Geneviv hawakuwa na msaada mwingine.

Akainuka na kuingia chumbani kwenda kuifungua ile barua na kusoma kilichomo ndani yake. Geneviv alibaki sebuleni na baba mdogo wake wakiendelea na mazungumzo ya kawaida. Baada ya kuufungua ule ujumbe, Bi Patricia alikutana na kitu ambacho kilimmaliza nguvu kabisa.
“Mungu wangu, yaani bado hatujatulia yameanza mengine! Sijui nitafanya nini mimi…huu mtihani siuwezi, bora kufa!”

Alijikuta machozi yakianza kumtoka. Baada ya Geneviv kuona mama yake anachelewa, aliamua kumfuata kule chumbani alikomkuta amejiinamia huku akitiririkwa na machozi.
“Mum what’s wrong? Umepatwa na nini?...”


Baada kuona mama yake anachelewa, ilibidi Geneviv amfuate kulekule chumbani. Alimkuta akiwa amechanganyikiwa baada ya kuisoma ile barua na ilivyoonekana ujumbe uliokuwa ndani yake ulikuwa ni shari tupu. Geneviv alitamani kujua Kilichokuwa ndani yake.

Akauchukua na kuanza kusoma. Wazazi na ndugu wa marehemu mzee Rwakatare, baba yake Geneviv walikuwa wamekaa kikao cha ukoo na kufikia maamuzi yafuatayo:

Bi Patricia alitakiwa kurithiwa na mdogo wa marehemu mume wake, bwana magafu Rwakatare ambaye tayari alikuwa na mke na watoto wengi kijijini kwao. Pia nyumba waliyokuwa wanaishi ilitakiwa iuzwe halafu wao, Bi Patricia , mwanae Geneviv na “mumewe mpya” walitakiwa kwenda kuishi kijijini kwa mzee Rwakatare.

Ama kwa hakika lilikuwa ni jambo la ajabu. Bi Patricia alishindwa kuamini kama ni kweli bado kuna jamii katika ulimwengu wa leo zilizokuwa zimepitwa na wakati kiasi kile.

Kurithi wajane? Kujimilikisha mali za marehemu ilhali familia yake bado inateseka?
“Yaani mimi nirithiwe, tukaishi kijijini…haiwezekani! Siko tayari bora kufa kuliko mchezo kama huu.” Bi Patricia na mwanae Geneviv waliendelea kukaa chumbani wakimuacha mgeni peke yake pale sebuleni.

Kwa jinsi hali ilivyoonyesha, kama Bi Patricia angeendelea kunyamaza kimya, ni kweli ndugu zake wangetekeleza kile walichokipanga.

Kwa jinsi mila zao zilivyokuwa, baada ya baba wa familia kufa, mke alitakiwa kurithiwa na kaka au wadogo wa marehemu na mali zote alizoacha huuzwa na wanandugu kugawana. Mke na watoto hawakuwa na haki yeyote ya kurithi zaidi ya kuwa watazamaji.

“What can we do mum? We need to act very soon, I promise I will support you!”
(Tutafanya nini mama, inabidi tuchukue hatua za haraka sana, naahidi nitakuunga mkono kwa kila kitu). Baada ya kuongea hayo, Geneviv alitoka mpaka sebuleni alikomuacha baba mdogo wake. Akakaa jirani naye na kuanza kumhoji maswali.

“ mwalimu alitufundisha kuwa mila za kurithi wajane ni mbaya kwa kuwa zinaweza kuwa chanzo kikuu cha magonjwa kama Ukimwi, mbona wewe unataka kumrithi mama?”
Bwana Magafu alicharuka na kuanza kuwa mkali baada ya kuulizwa swali lile na Geneviv.

“Ndio mama yako alivyokutuma uje kusema siyo? Haya mambo hayakuhusu kwanza we bado mtoto usiingilie mambo ya kikubwa, nyamaza”.

Muda mfupi baadae Bi Patricia alitoka chumbani na kukuta shemeji yake akifoka. Hakutaka kulaza damu, akaamua kuweka wazi msimamo wake.

“Shemeji nakuheshimu sana na pia nawaheshimu ndugu zangu wote, lakini kuhusu haya mnayoyataka niseme wazi kuwa siko tayari, sihitaji msaada wa mtu kuiongoza familia, naamini ninaweza kila kitu kwa hiyo mniache na mwanangu…” kauli ile iliamsha hasira za bwana Magafu kwani aliamini angepokelewa kwa mikono miwili kama baba mpya, na wangefaidi baada ya kuuza nyumba na kuhamia kijijini.

Alishangaa ni kwa nini Bi Patricia alikuwa na ujasiri wa kumjibu vile kwani kwa mila za kwao zilivyokuwa mwanamke hakuruhusiwa kujibu kitu au kupinga maamuzi ya wana ukoo. Aliendelea kufoka na kutoa kauli za vitisho kuwa ni lazima watii maamuzi ya wana ukoo na kama wakiendelea kubisha watakiona cha mtema kuni.

Bwana Magafu aliinuka na kubeba mizigo yake kwa hasira na akawa anatoka huku akiendelea kutoa vitisho kuwa atarudi tena baada ya siku chache kufanya utekelezaji wa yale yaliyoamriwa.

Alitoka na kubamiza mlango kwa nguvu akiwaacha Geneviv na mama yake wameduwaa. Huo ulikuwa ni mtihani mwingine ambao ama kwa hakika ulikuwa mgumu kwa Bi Patricia. Walishikana mikono wakapiga magoti na kuanza kumuomba Mungu wao awaonyeshe njia sahihi.

Baada ya sala iliyodumu kwa mrefu, hatimaye Bi Patricia na mwanae Geneviv walianza kujadiliana nini cha kufanya.

Hakuna aliyekuwa na jibu la haraka la juu ya nini kifanyike kabla mambo hayajaharibika. Kila mbinu ilionekana kuwa na matatizo.

“Mi nafikiri tufunge safari na kumfuata Raisi aliyejiuzulu, bwana Kahungo…si unakumbuka kipindi kile alitusaidia sana!” Lakini yeye sio Raisi tena, we unafikiri atatusaidia nini?”

“Hata kama sio Raisi tena, yule ni mwanamapinduzi wa kweli na lazima atatusaidia hata kwa mawazo na ushauri juu ya nini cha kufanya.”
Wazo la kumfuata raisi mstaafu likaonekana ndio bora.

Hakuna aliyekuwa tayari kuona wanarudishwa kwenye matatizo kwa sababu ya tamaa ya ndugu zao. Walijizatiti vilivyo kupambana mpaka dakika ya mwisho.

Ngoja kesho nikaombe ruhusa kazini na wewe jiandae, nikirudi tu tunaanza safari.
********

Baada ya Bwana Magafu kufikisha ujumbe aliotumwa kutoka kijijini na kukataliwa na Bi Patricia na mwanae Geneviv, aliondoka akiwa na hasira kupita kawaida. Katika maisha yake hakuwahi kugomewa kitu na mwanamke hasa huko kijijini kwao.

Aliona kama amedhalilishwa kwa sababu aliamini kuwa anazo haki zote za kumrithi mke wa marehemu kaka yake kwani mila za kwao zilikuwa zimehalalisha jambo hilo.

Na zaidi alitegemea kuwa baada ya yeye kufanikisha nyumba ile kuuzwa, angepata pesa nyingi za bure na heshima yake kijijini kwao ingeongezeka. Hakutaka kurudisha jibu kijijini kuwa ameshindwa kufanya kazi aliyotumwa na wanaukoo kwani hiyo ingekuwa aibu kwake.

Alijiapiza kuwa ni lazima afanikishe alichotumwa, kuuza nyumba na kurudi na mkewe mpya Bi Patricia kijijini.

Baada ya kuondoka pale nyumbani kwa vurugu, Bwana Magafu Rwakatare alienda kupanga chumba gesti na kuanza kuandaa mipango ya namna ya kurudi upya na mashambulizi makubwa zaidi.

Hakutaka kupoteza muda…siku ileile akaanza kutafuta mteja wa kununua nyumba kupitia kwa madalali.

Mpaka jioni giza linaingia alikuwa ameshapata wateja watatu ambao wote walikuwa na nia ya kununua nyumba, na wakaelewana kuwa asubuhi na mapema wawahi ili aende kuwaonyesha mahali nyumba ilipo na wakubaliane bei.

Alijikuta akijipongeza hata kabla hajamaliza kazi kwani aliamini hiyo ndio dawa ya mwanamke mbishi anayejifanya amesoma. Hakufikiria kuwa anaweza kupata upinzani kama aliokutana nao asubuhi ile.

Bi Patricia na mwanae hawakupata hata tone la usingizi usiku ule. Walikuwa wakizidi kumuomba Mungu wao awalinde kwani wa hakika vita iliyokuwa mbele yao ilikuwa si ndogo.

Kulipokucha tu, Bi Patricia aliwahi kuondoka lengo lake likiwa ni kwenda kuomba ruhusa kazini ili aweze kushughulikia kisawasawa hatua za kuwazuia ndugu wa mumewe wasisababishe madhara kwake na kwa mwanae Geneviv. Hakuwa tayari kuona anarithiwa wala nyumba yake inauzwa.

“Mum usikawie kurudi, mi naanza kujiandaa…” Geneviv alikuwa akimsihi mama yake wakati akitoka. Muda mfupi baadae baada ya Bi Patricia kuondoka, Bwana Magafu alirudi pale nyumbani akiwa ameongozana na watu watatu na hata bila kuingia ndani, akaanza kuwaonyesha ile nyumba na wakawa wanazunguka kuithaminisha.

Alikuwa amekuja na wateja wa kununua nyumba ile, na hakutaka kumshirikisha kitu chochote Bi Patricia.
Geneviv alishtuka kusikia watu wakizunguka nyumba yao huku wakianza kuelewana bei.

“Mungu wangu, yaani baba mdogo kweli ameenda kuleta wateja, mi nilifikiri anatania! Tutakuwa wageni wa nani sisi kama kweli atauza nyumba yetu? People are no good, I hate them…”

Geneviv alijikuta akiongea peke yake wakati akiwachungulia wale wateja wakipatana bei na baba yake mdogo. Alitamani kufanya kitu kuwazuia lakini hakujua afanye nini kwa wakati ule.

Alitamani mama yake arudi nyumbani haraka ili aje ajionee mwenyewe maajabu ya walimwengu. Akajikuta akipatwa na ujasiri wa ajabu na akatoka mpaka nje na kuwafuata pale walipokuwa wamesimama wakiendelea kupatana bei.

Alipowasogelea hata bila ya kuwasalimu, alianza kuongea kwa sauti ya juu akiwaeleza kuwa hiyo nyumba sio ya yule waliyekuwa wakielewana nae bei, bali ni ya mama yake na yeye… na kwamba baba yake ndiye aliyeijenga akisaidiana na mama yake.

Hakuna aliyemjali, walimpuuza na wakaendelea na maelewano yao. Walimchukulia kama mtoto asiyeelewa anachokizumgumza.

Alipoendelea kupiga kelele, Bwana Magafu alimvuta pembeni na kumshikisha adabu kwa kumtandika vibao mfululizo vya usoni mpaka Geneviv akawa anahisi kizunguzungu. Alikimbilia ndani ambako alijifungia chumbani kwake na kuanza kulia akimtaja marehemu baba yake.

Baada ya makubaliano yao kumalizika, baba mdogo Magafu aliondoka na wale watu wakaelekea kusikojulikana.

Muda nfupi baadae Bi Patricia alirudi baada ya kuruhusiwa kazini kwake na alipofika alimkuta Geneviv amejifungia chumbani akilia huku usoni akiwa na alama za kupigwa.

“Hee! imekuwaje tena, mbona hivyo…what’s wrong with you?”
Ilibidi aeleze kila kitu kilichoendelea baada ya yeye kuondoka.

Alibaki mdomo wazi baada ya kusikia kuwa shemeji yake amerudi akiwa na wateja na tayari wameshakubalia na kupatana kuhusu nyumba ile bila ridhaa yao. Alijikuta nguvu zikimuishia.

Bila kupoteza muda wakajiandaa na kutoka kuelekea nyumbani kwa Raisi mstaafu kwenda kuomba msaada wa kisheria. Ilikuwa ni safari ndefu kwani baada ya kujiuzulu, Bwana James Kahungo aliamua kuhamia kijijini kabisa alikokuwa anaendelea na shughuli za kilimo na ufugaji pamoja na familia yake yote.

Muda mfupi baada ya kuondoka, yule mteja aliyeshinda kununua ile nyumba alienda kumkabidhi bwana Magafu kiwango kikubwa cha pesa kama walivyokubaliana.

Akaandaa barua ya notisi na kwenda kuibandika mlangoni mwa ile nyumba akiwataka wote wanaoishi ndani ya nyumba ile wawe wameondoka baada ya masaa 72 (siku tatu) ili kupisha ukarabati aliokuwa akitaka kuufanya kabla ya kuhamia.
******
Safari ilikuwa ndefu sana na iliwachukua zaidi ya masaa 6 kufika kijijini alikokuwa anaishi Raisi mstaafu. Walipofika walipokelewa na wafanyakazi wa ndani na wakakaribishwa mpaka ndani.

“Sijui kama tunaweza kuongea na mheshimiwa?” aliuliza Bi Patricia kwa sauti ya chini akimuuliza mmoja wa wafanyakazi wa ndani wa Bwana James Kahungo. Jibu walilopewa lilizidi kuwamaliza nguvu kabisa, waliambiwa kuwa Bwana Kahungo alikuwa ameenda nje ya nchi kwa mapumziko marefu na angechelewa kurudi.

“Whaaat?... Ameondoka lini na atarudi lini? We are Finished… tutafanya nini sasa mwanangu? Yote tumwachie Mungu”

Bi Patricia aliongea kwa kuhamaki kiasi cha kuwafanya wale wafanyakazi waanze kuulizana kulikoni. Wakaondoka hata bila kuaga wakiwa wamechanganyikiwa kupita kiasi. Ilivyoonekana ni kuwa juhudi zao za kupambana na ndugu wa marehemu zilikuwa zikielekea kugonga mwamba.

Walianza safari ya kurudi nyumbani kwao wakiwa hawaelewi nini hatma yao. Safari nzima hakuna aliyekuwa akimsemesha mwenzake, kila mmoja alikuwa kimya akiwaza ya kwake.

Hatimaye walirudi mpaka nyumbani kwao, na walipofika tu, walikutana na tangazo mlangoni likiwataka kuhama ndani ya masaa 72 ili kupisha ukarabati.

Bi Patricia alihisi kichwa kikimchemka kama amemwagiwa maji ya moto. Alishindwa kuelewa nini cha kufanya na akajikuta taratibu shinikizo la damu likianza kushuka na mwili kukosa nguvu. Ilibidi apitilize moja kwa moja chumbani kwenda kulala.

Geneviv akabaki amekaa mlangoni akiwa amejiinamia. Ilikuwa tayari ni jioni na jua lilikuwa likianza kuzama. Akiwa bado amejiinamia pale mlangoni, alikuja kushtuliwa na rafiki yake Joackim “kim” aliyekuwa amekuja kumtembelea.

“Vipi dada Geneviv mbona unaonekana una mawazo namna hiyo, are you okay?” Aliongea Kim na kukaa jirani na Geneviv kwenye ngazi za pale mlangoni. Geneviv alijilazimisha kufurahi lakini alishindwa kuificha huzuni iliyokuwa moyoni mwake. Kim aliligundua hilo na akawa anamdadisi kwa upole kilichomsibu.

Geneviv hakujibu kitu zaidi ya kumuonyesha lile tangazo pale mlangoni.
Kim aliinua macho na kuanza kulisoma. Hapo ndipo alipogundua kwa nini Geneviv alikuwa na hali kama ile. Alirudia kulisoma zaidi ya mara tatu kisha akawa anamtazama Geneviv kwa huruma.

“Kwani ni nani aliyeandika hivi na kwa nini amefanya hivi?” Aliuliza Kim akiwa na shauku ya kutaka kujua. Ilibidi Geneviv amueleze kila kitu kuanzia mwanzo mpaka mwisho. Geneviv alijikuta akidondosha upya machozi baada ya kumaliza kumsimulia Kim.

“Shed no more tears Geneviv…everything gonna be alright! (Usilie tena Geneviv, kila kitu kitakuwa sawa)…

Kim alikuwa akimbembeleza Geneviv kwa sauti ya chini huku akimfuta machozi. Alimhakikishia kuwa yuko tayari kuwasaidia kwa kuwa baba yake ni mwanasheria na ameshawahi kushughulikia kesi kama hizo mara nyingi sana na mara zote lazima alikuwa akishinda. Geneviv alimtazama usoni Kim akiwa kama haamini alichokuwa anakisikia kutoka kwake.

Ni hapo ndipo alipokumbuka kuwa ni kweli baba yake Kim alikuwa ni mwanasheria mzoefu na alishawahi hata kuja shuleni kwao siku za nyuma kuwapa semina juu ya ukatili dhidi ya wanawake na haki zao. Alijikuta akianza kuingiwa na matumaini mapya.

“Naomba nikamuite mama uje umwambie na yeye asikie, She is depressed na ameshakata tamaa tusipomsaidia mapema kuna uwezekano mkubwa akaanza upya kuumwa. Geneviv aliinuka haraka na kwenda kumuamsha mama yake aliyekuwa amelala baada ya kupoteza matumaini na kutojua nini cha kufanya.

“Mama…mama! amka kuna habari njema, njoo usikilize” Geneviv alikuwa akimwambia huku akimtimgisha mama yake aliyekuwa tayari amepitiwa na usingizi. Bi Patricia aliamka na kwenda kusikiliza alichoitiwa. Aliinuka kwa uchovu na kutoka nje ambako alimkuta Kim akiwa amesimama mlangoni. Alimkaribisha ndani na Geneviv akamtambulisha kuwa yule ndio Kim.

“Kumbe wewe ndio Kim, karibu sana mwanangu na nakushukuru kwa kuwa msaada nuhimu kwa dada yako Geneviv”. Baada ya mazungumzo mafupi ya kujuana, Kim alianza kumweleza mama Geneviv kuwa baba yake ni mwanasheria mashuhuri na ameshawahi kushughulikia mikasa kama hiyo mara nyingi na anao uzoefu mkubwa sana.

“Lakini sina hela za kumlipa kwa sasa, atakubali kweli kutusaidia?” Bi Patricia alikuwa akiongea kwa sauti ya chini. Kim aliwahakikishia kuwa baba yake ni mtu wa watu na angekuwa tayari kuwasaidia bila shida. Bi Patricia alikuwa bado haamini kama kweli wanaweza kupata msaada wa kutetewa haki yao bila kuwa na pesa.

Baada ya mazungumzo marefu, Kim aliaga na kuondoka akiwaacha Geneviv na mama yake wakiwa na matumaini mapya. Aliwaahidi kuwa usiku huohuo angeenda kumweleza baba yake na wangekuja naye kesho yake asubuhi na mapema. Baada ya Kim kuondoka, Bi Patricia na mwanae waliendelea kujadiliana kwa muda mrefu hadi usingizi ulipoanza kuwachukua. Hawakuacha kumuomba Mungu wao kabla ya kulala kama ilivyokuwa kawaida yao.

Asubuhi na mapema kabla hata hawajaamka, walisikia mlango ukigongwa na walipotoka kufungua, walikuwa ni Kim na baba yake. Bi Patricia na Geneviv waliwakaribisha kwa uchangamfu… “Karibuni ndani wageni…” Baada ya kuingia ndani Kim alimtambulisha baba yake na akamtaka mama ake Geneviv amweleze hali halisi ya mkasa mzima. Geneviv na Kim wakaambiwa watoke nje ili kuwapisha wazungumze mambo yao kwa uhuru.

Baada ya Geneviv na Kim kutoka nje, Bi Patricia alianza kumueleza Bwana Magwaza (baba yake Kim) mkasa mzima tangu mwanzo hadi mwisho. Walizungumza kwa muda mrefu na kwa pamoja wakakubaliana nini cha kufanya. Mwanasheria Magwaza, baba yake Kim, alikuwa akisifika kwa kuwatetea wajane na watoto yatima waliokuwa wakitaka kudhulumiwa mali zao na ndugu au watu baki. Alikuwa na historia nzuri ya kusimamia haki na katika kesi zote alizokuwa akizisimamia, haki ilikuwa ikipatikana bila ubishi…na alimhakikishia Bi Patricia kuwa hakuna kitakachoharibika.

“Ondoa wasiwasi kabisa, cha msingi nipe hiyo hati ya nyumba na mimi naanza kuwashughulikia asubuhi hii hii. Mpaka jioni nitakuwa nimeshakamilisha kila kitu, nikirudi nitakuja kukueleza nini cha kufanya. Ondoa wasiwasi na uwe huru kabisa. Hapa ni kwako na hakuna atakayekutoa wala kukudhulumu haki yako.”

Geneviv na Kim walikuwa wamekaa nje wakilitazama jua la alfajiri lilivyokuwa linachomoza kutoka upande wa mashariki. Walikuwa wametulia kila mmoja akiwaza la kwake kichwani.
“But Kim, why do you act good to me like this? What special thing did I have to deserve this?” ( Lakini Kim, kwanin unanifanyia mambo mazuri namna hii? Nina nini cha ziada mpaka nistahili haya?)

Geneviv alimuuliza Kim swali ambalo hakulitegemea. Kim alimgeukia Geneviv wakawa wanatazamana usoni. Aliachia tabasamu pana kisha akaanza kumjibu kwa sauti ya chini…

“Sidhani kama kuna lolote kubwa nimekufanyia, yote ni ya kawaida, na lengo langu kubwa ni kutaka kukuona ukifurahi, I want you to shed no more tears…Geneviv! I want to see you rejoicing (sitaki kukuona ukitoa tena machozi Geneviv, napenda kukuona ukifurahi).”

Kim alijibu kwa sauti ya chini lakini iliyokuwa imebeba ujumbe mzito ndani yake…Wakatazamana tena na kila mmoja akatabasamu! Mara walisikia mlango ukifunguliwa na wazazi wao wakawa wanatoka. Bi Patricia alikuwa akimsindikiza Bwana Magwaza baada ya kufikia muafaka wa nini cha kufanya ili kuhakikisha nyumba ile haiuzwi wala Bi Patricia harithiwi na shemeji yake.

Geneviv na Kim walisimama na kuwafuata wazazi wao.
“Mbona mlikuwa mmetulia sana, mi nilijua hampo kumbe mna…”
Aliongea kwa masihara Bi Patricia na wote wakacheka kwa furaha. Ilikuwa ni asubuhi waliyoianza vizuri na hiyo iliashiria siku njema pia.

Bwana Magwaza na mwanae Kim waliaga na kuondoka huku Geneviv akizidi kuwasindikiza kwa macho akitoa tabasamu kwa Kim. Alikuwa akijiuliza bila kupata majibu ya kuridhisha kwa nini alikuwa akijisikia tofauti na kuwa na furaha sana akikaa karibu na Kim, na kwa nini Kim alijitolea kuwasaidia namna ile wakati hawakuwa na undugu wowote.

“Wewe nawe, ukishamuona Kim utachekecheka siku nzima, anakupa nini?” Bi Patricia alizidi kumtania mwanae huku akimpigapiga mabegani na wote wakawa wanacheka kwa furaha… wakaingia ndani. Matumaini ya kuishi salama yalikuwa yakizidi kuongezeka kadri muda ulivyokuwa unaongezeka. Baada ya kumaliza kujiandaa, Bi Patricia aliondoka na kuelekea kazini akimuacha Geneviv peke yake pale nyumbani.

“Ubaki salama dear, najua leo mmeonana na Kim asubuhi asubuhi utakuwa na furaha siku nzima… take care, see you!” Aliaga Bi Patricia na kumuacha Geneviv akicheka peke yake. Walau ile furaha waliyokuwa wameizoea kabla hawaajaanza kuandamwa na jinamizi la mikosi ilianza kurudi. Geneviv aliendelea kufanya shughuli ndogo ndogo za nyumbani na baada ya kumaliza, aliinga chumbani kwake na kama kawaida alichukua Biblia yake na kukaa nayo kitandani.

Majira ya kama saa saba mchana, alisikia mlango ukigongwa kwa nguvu.
“Nani tena anayegonga mlango kwa fujo hivyo?” Geneviv alikuwa akijiuliza wakati akiinuka na kwenda kufungua. Alikuwa ni baba yake mdogo. Japokuwa ilikuwa bado ni mapema, alionekana tayari amelewa chakari… bila hata kukaribishwa akaingia hadi ndani. Geneviv alikuwa mpole ghafla akitaka kuona baba yake mdogo angefanya nini. Kitu cha kwanza alichokitaka ni chakula.

“Fanya haraka nipikie chakula, njaa inaniuma!” Aliongea kwa kufoka Bwana Magafu, na bila hiyana Geneviv aliingia jikoni na kuanza kuandaa chakula. Wakati Geneviv akiendelea kuandaa chakula, Bwana Magafu alikuwa akifikiria yake. Sio kweli kwamba alikuwa na njaa kama alivyodai bali kuna kitu alichokuwa anajiandaa kukifanya.

Aliinuka huku akipepesuka kutokana na kuzidiwa na pombe na akaenda kufunga mlango wa kutokea nje kwa ndani. Alipohakikisha ameufunga kabisa, alimfuata Geneviv aliyekuwa akiendelea kumuandalia ‘baba mdogo’ wake chakula.

Alimfuata mpaka kule jikoni na akasimama mlangoni akimtazama Geneviv aliyekuwa akihangaika kusonga ugali. Hakujua kama kuna mtu anamtazama nyuma yake, akawa anaendelea kupika. Bwana Magafu aliendelea kumtazama mwanae kwa jicho la uchu na katika hali ya kustaajabisha, alianza kumshikashika Geneviv kiunoni, hali iliyomfanya ashtuke kupita kiasi na kuacha kazi aliyokuwa anaifanya.

Akiwa hana hata chembe ya aibu, alimsogelea Geneviv mwilini na kumkumbatia kwa nguvu. Geneviv alishindwa kuelewa baba yake alikuwa akitaka nini. Alifanikiwa kumtoka mikononi na akakimbilia sebuleni ambako alimuwahi na kumshika tena. “Unataka nini baba?” Geneviv alimuuliza baba mdogo wake huku akitetemeka baada ya kushindwa kuelewa alichokuwa anakitaka kutoka kwake.

“Si nimekwambia njaa inaniuma mamaa!” aliongea kilevi Bwana Magafu huku mate ya uchu yakimtoka.
“Lakini si ndio niko kukupikia… alijitetea Geneviv huku akijitoa mikononi mwa baba yake.
“Usiwe kama mtoto mdogo, we umeshakuwa mkubwa sasa, simaanishi chakula kama ulivyoelewa, ila ninamaanisha nanii…”
Bwana Magafu alishindwa kumalizia alichotaka kusema, akamsukumia Geneviv juu ya kochi na kumlalia. Wakaanza kuvutana, Geneviv akijitahidi kuchoropoka kutoka pale juu ya kochi kwa nguvu zake zote.

Bwana Magafu alizidi kumbana kisawasawa lakini Geneviv akawa anazidi kujaribu kuchomoka, mwishowe baba mdogo wake alimzidi nguvu. Akiwa bado anafurukuta, alishangaa kumuona akifungua mkanda wa suruali yake na kuishusha chini.
“Mungu wangu, yaani hata wewe baba unataka ku…”
Kabla hata hajamalizia kusema, alimziba mdomo kwa nguvu na kuanza kumvua sketi aliyokuwa ameivaa.
*******

Geneviv aliendelea kusumbuana na baba mdogo wake pale juu ya kochi kwa muda mrefu. Hakukubali kuona anabakwa tena kwa mara nyingine kirahisi namna ile. Alikuwa na historia mbaya ambayo bado ilikuwa haijafutika akilini mwake, na sasa baba yake alikuwa akitaka kumfanyia yaleyale tena. Alijitahidi kwa kadri ya uwezo wake wote kuzuia kitendo kile kisimtokee tena… na mbaya zaidi safari hii alikuwa ni baba yake mdogo. Zile purukushani zilizokuwa zinaendelea, zilitoa nafasi kwa Geneviv kupiga kelele za kuomba msaada.

Kim alikuwa anaenda kumtembelea Geneviv kama kawaida yake. Alipofika jirani na nyumba yao, alishtuka kusikia sauti kama ya Geneviv akilia kwa nguvu kuomba msaada, akahisi kuna tatizo liliompata. Kwa haraka alikimbia mpaka mlangoni, lakini alipojaribu kusukuma mlango, ulikuwa umefungwa kwa ndani huku Geneviv akizidi kupiga kelele za kuomba msaada.

Alichanganyikiwa kusikia Geneviv akilia namna ile, akahisi kwa vyovyote kuna jambo baya linamtokea. Akili ikamjia haraka, akaona ni bora avunje mlango ili kuwahi kumuokoa Geneviv. Alirudi nyuma kwa nguvu na kujianza kutaka kuurukia mlango na kuingia nao.

Alipokaribia alisita kufanya alichotaka kufanya baada ya kusikia sauti nyingine ambayo ilimshtua. Ilikuwa ni sauti kubwa ya mwanaume aliyekuwa akiguna kutokana na maumivu. Alishindwa kuelewa ni nini hasa kilichokuwa kikiendelea mle ndani. Kelele za yule mwanaume zilizidi kuongezeka na Geneviv akawa hasikiki tena kama anaomba msaada. Akagundua lazima kuna mchezo mchafu unaoendelea ndani. Akajikuta akipandwa na mori kuliko awali. Hakuwa tayari kuona Geneviv anapatwa na jambo lolote baya.


Baada ya kuzidi kubanwa, Geneviv alikumbuka mbinu moja ambayo alishawahi kufundishwa na rafiki yake Alice. Alibana miguu yake kwa nguvu zake zote, kisha akapeleka mdomo wake shavuni kwa baba yake. Mzee akajua amemzidi nguvu na amelainika, akazidi kumsogezea shavu. Geneviv alitumia fursa hiyo ipasavyo. Alimng’ata na kuingiza meno kisawasawa shavuni kwa Magafu, akawa anazidi kuongeza nguvu ya kung’ata hali iliyomfanya Bwana Magafu ahisi maumivu makali kupita kiasi. Uvumilivu ulimshinda na akajikuta akiguna kwa sauti ya juu kutokana na maumivu. Geneviv alizidi kumshikilia shavu kwa meno yake makali na kumfanya azidi kupiga kelele.

Kim alikuwa akihangaika kuvunja mlango. Aliurukia kwa nguvu lakini haukufunguka, akarudia kuukanyaga kwa miguu yote miwili huku akitumia nguvu zake zote, lakini bado haukufunguka. Akakusanya nguvu upya na kuurukia mlango kwa nguvu zake zote. Kitasa kilivunjika na kuufanya mlango ufunguke kwa nguvu. Kim aliingia kwa kasi ndani na kuanza kufuata sauti ilikokuwa inatokea. Alikimbia mpaka sebuleni huku akitweta… alichokiona hakuamini macho yake. Alibaki kuduwaa asijue cha kufanya. Alijihisi kama yuko ndotoni, akajifikicha macho kuhakikisha kama ni kweli au anaota.

“Kim save me! Save me my dear im dying”… Geneviv aliongea kwa sauti na kuanza kulia baada ya kumuona Kim ameduwaa. Akili ilicheza kwa haraka na akaona huo ndio muda muafaka wa kumuonyesha Geneviv kuwa anamjali. Kwa haraka aliokota stuli na kuanza kumpiga nayo mgongoni Magafu kwa nguvu zake zote. Aliendelea kumpiga nayo mpaka alipohakikisha amemuachia Geneviv. Baada ya kuona amemuachia, alimkanyaga usoni kwa nguvu…akaangukia upande wa pili wa kochi akiwa taabani.

Kwa haraka Kim alimuinua Geneviv na kumkumbatia kwa nguvu. “Are you okey Genny, didn’t he harm you? Oh My God…(Uko salama Geneviv? Vipi hajakudhuru? Oooh Mungu wangu…)

Geneviv alishindwa kujibu chochote zaidi ya kuendelea kulia kwa uchungu huku akimkumbatia Kim na kukilaza kichwa chake kifuani mwake huku akizidi kumwaga machozi. Kim alimtoa nje Geneviv na kwenda kumkalisha nje kwenye hewa safi. Alishtuka kuona Geneviv akiwa na damu mdomoni…akahisi alikuwa ameumia. Geneviv alimweleza kuwa hajaumia mahali popote ila zile damu alizipata baada ya kumng’ata mbaya wake. Japokuwa alikuwa ametoka kwenye purukushani nzito, alijisikia amani sana kuokolewa na Kim.

“Kweli wewe ni mwanaume, sijaamini kwa jinsi ulivyoweza kuniokoa…kumbe unanipenda eeh! Ahsante sana Kim, sina cha kukulipa ila Mungu ndiye atakayenilipia!” Aliongea Geneviv huku akianza upya kutokwa na machozi. Kim akawa anamfuta machozi huku akizidi kumbembeleza. Alianza kumueleza kila kitu kilivyokuwa. Kim alijikuta akimuonea huruma sana, na akajiona shujaa kwa kumsaidia kutoka kwenye wakati mgumu aliokuwa nao.

Magafu alifanikiwa kusimama kutoka pale chini alipokuwa ameanguka, na kuanza kujkongoja kutoka nje. Aliona ingekuwa aibu sana endapo watu wengi zaidi wangesikia kilichomtokea. Akawa anajivuta kutoka nje, usoni akiwa na alama za meno shavuni huku damu zikiwa zinaamchuruzika. Mgongo nao ulikuwa kama unawaka moto kwa kipigo kikali alichopokea. Alikuwa akijuta kuabishwa na watoto…

Akatoka mpaka nje na kuanza kuwatolea macho Geneviv na Kim waliokuwa wamekaa pale chini wakibembelezana. Aliwatazama kwa hasira na akaapa kuwa lazima angerudi tena kuja kulipa kisasi. ”Mnajifanya wajanja siyo, ngoja niende…nikirudi mtanitambua mimi ni nani.”

Muda mfupi baada ya Magafu kuondoka, Bi Patricia alirudi kutoka kazini. Aliwakuta Geneviv na Kim wamekaa nje, akajua wako kwenye mazungumzo yao ya ujana kama kawaida yao, wakasalimiana juu juu na kupitiliza hadi ndani. Alipofika sebuleni alishangaa kuona vitu vikiwa vimevurugika ovyo ovyo. Macho yake yalitua juu ya kochi na alipolikaribia aligundua kuwa limevunjika upande.

Alipozidi kuchunguza akaona michirizi ya damu. Akajikuta mwili wote ukimsisimka.
“Whats the hell is this!” Ilibidi atoke kwenda kumuuliza Geneviv ni nini tena kilichotokea. Wakakutana mlangoni Geneviv naye akiwa anamfuata ndani huku akiwa na hamu ya kutaka kumsimulia mama yake kilichotokea. Kim alibaki nje kuwapisha wafanye mazungumzo yao kwa uhuru.

Geneviv alieleza kila kitu kilichotokea kwa mama yake. Bi Patricia alibaki ameduwaa kwa mshangao. “Hivi ni kweli au naota? Yaani hawa watu wanataka nini kutoka kwetu? Mi nafikiri wanataka roho zetu,this is too much! sasa wameuwasha moto, ama zetu, ama zao!” Aliongea kwa jazba na kuingia ndani kwenda kubadilisha nguo. Japokuwa alikuwa akimwamini Mungu, alijikuta akipandwa na hasira kuliko kawaida.

“Wanafikiri kwa sababu mimi ni mwanamke ndio kila mtu anaweza kunitendea anavyotaka, haiwezekani! Noo! Na nitahakikisha napigana mpaka dakika ya mwisho, kama matatizo nimeshayazoea, siogopi kitu tena ”
Bi Patricia alikuwa akijisemesha peke yake kwa jazba. Aliapa kupambana na kila mtu anayetaka kumharibia maisha yake na mwanae wa pekee Geneviv.

Muda mfupi baadae, Bwana Magwaza (baba yake Kim) alikuja kumpa taarifa ya hatua alizozifikia katika suala lao la kutaka kudhulumiwa haki yao. Ilikuwa ni taarifa njema ambayo kwa kiasi Fulani ilimtuliza Bi Patricia ambaye alionekana kuanza kuchanganyikiwa baada ya binti yake kuponea chupuchupu kufanyiwa kitu mbaya na shemeji yake.

Bwana Magwaza alikuja na taarifa kuwa suala lile limefikishwa mbele ya mahakama ya jamii na imeamriwa kwamba, aliyenunua nyumba na aliyemuuzia wote wanatakiwa kuwekwa chini ya ulinzi na kufikishwa mbele ya mahakama kujibu mashtaka ya unyanyasaji na udhalilishaji wa kijinsia kwani walikuwa wamekiuka sheria mpya iliyokuwa imetungwa maalum kwa ajili ya kuwatetea wajane na mayatima.

Aliwahakikishia kwamba, baada ya hayo masaa 72 ambayo waliamriwa kuwa yakiisha wawe wamehama, wasiondoke kwani polisi watakuwepo kuwapa msaada wa kuwakamata wahusika.

Taarifa ile ilileta utulivu ndani ya mawazo ya Bi Patricia na akaanza kuona njia ya kutokea kwenye tatizo lile lililokuwa likimkabili. Aliwaona Kim na baba yake kama malaika walioshushwa na Mungu kutoka mbinguni kuja kuwafuta machozi yeye na mwanae Geneviv. Alishindwa namna ya kushukuru kwa msaada ule aliokuwa amepewa na Bwana Magwaza na mwanae Kim, zaidi ya kumshukuru sana Mungu kwa kuwakutanisha.
Siku tatu (masaa 72) waliyopewa Bi Patricia na mwanae kuhama yakawa yanaelekea kuisha.

Hawakuwa na hofu tena kwani wanausalama walishawahi kufika pale nyumbani asubuhi na mapema wakiwa na Bwana Magwaza, na wakaandaa mtego kabambe wa kuwatia nguvuni Magafu na mteja wake aliyemuuzia nyumba. Ilibidi bi Patricia asiende kazini ili kutoa ushirikiano kwa wanausalama kuhakikisha haki yake haichukuliwi na watu wengine. Baada ya masaa machache baadae, Bwana Magafu na mteja wake wakawa wanakuja, wakiwa wameongozana na mabaunsa watatu kwa lengo la kuwatoa kwa nguvu Bi Patricia na mwanae.

Hao wanakuja, tena wamengezeka na mabaunsa… Wanausalama walikuwa wakijiandaa kupambana nao. Walitaka kusubiri kidogo waanze kufanya vurugu ndipo wawakamate wakiwa na ushahidi na vidhibiti vya kutosha kuwatia gerezani. Wale wanausalama wakajificha mle ndani na wakamuamuru Bi Patricia awapokee halafu awasikilize wanachotaka kukifanya. Bi Patricia akatii kama alivyoambiwa. Kwa muda huo Geneviv alikuwa amerjifungia chumbani akiwa hataki kabisa kumuona baba mdogo wake.

Wakasogea mpaka mlangoni na kuanza kubisha hodi kwa vurugu. Bi Patricia akafungua mlango na kuwasikiliza walichokuwa wanakitaka. Bila hata kuongea nae kitu, waliwaamuru wale mabaunsa kuanza kutoa vitu vyote nje, na bila kupoteza Muda wakaanza kazi yao. Wakawa wanarusha vitu nje na kuvitupia mbali. Muda mfupi baadae wale wanausalama wakaibuka kutoka mafichoni na kuwazunguka wote watano, Magafu, Mteja aliyenunua nyumba na mabaunsa watatu.

“Mko chini ya ulinzi, wote inua mikono juu…” takayekadi tunamwaga damu yake ardhini” Mkuu wa wale wanausalama alitoa amri kali huku wakiwanyooshea bunduki.

Baada ya Bwana magafu na wenzake kubanwa na polisi eneo la tukio, waliishiwa ujanja na kuamua kusalimu amri. Polisi waliwakamata na kuwatia pingu na muda mfupi baadae gari la polisi likafika na kuondoka nao kuwapeleka gereza maalumu la kijamii. Bi Patricia, Geneviv, Kim na baba yake waliendelea kupongezana kwa kazi nzuri ambayo hatimaye ilifanikiwa. Ilikuwa ni kama mpango wa Mungu kwani bila msaada wa Kim na baba yake, hakika nyumba ile ingeshauzwa. Walimshukuru sana Mungu wao kwa yote aliyowafanyia.

Furaha ikawa imerudi upya. Siku nzima ilikuwa ya furaha mno kwa kila mmoja. Bi Patricia alikaa kwa muda mrefu na Bwana Magwaza wakizidi kupongezana, huku Geneviv na Kim nao wakiendelea kufurahi kwa pamoja. Masaa yalikatika kwa haraka na hatimaye usiku uliingia. Waliaga na kuondoka wakiwaacha Geneviv na mama yake wakiendelea kufurahi.

Baada ya kula chakula cha usiku, walimshukuru Mungu kama kawaida yao na kwenda kulala. Walijadiliana pia kama kuna umuhimu wa kumuongezea mashtaka Bwana Magafu baada ya kitendo chake cha kutaka kumfanyia kitu mbaya Geneviv.
“Mum we should forgive him, let the world teach him” (mama mi nafikiri tumsamehe tu, dunia ndio itayomfunza), aliongea Geneviv kwa upole na mama yake akamuunga mkono. Wakakubaliana kumsamehe na kutomuongezea kosa lingine la kutaka kumbaka Geneviv.

Usiku wa manane wakiwa wamelala, walianza kusikia mambo ya ajabu juu ya paa la nyumba yao. Paka wengi walikuwa wakicheza juu ya bati huku wakilia milio ya ajabu, wengine kama watoto wachanga huku wengine wakicheka kama watu.
“Mama!... mamaa!… hebu sikiliza huko nje…”
Geneviv alikuwa akimnong’oneza mama yake baada ya kusikia kelele za mapaka zikizidi kuongezeka juu ya paa la nyumba yao.

3 comments:

THE DARKEST HOURS (SAA ZA GIZA TOTORO)- 1

Mtunzi: Hashim Aziz (Hashpower) 0719401968 “Ngo! Ngo! Ngo! Fungua!” “Nanii?” “Fungua!” “Jitambulishe kwanza, wewe nani?” “Nimese...