Sunday, August 29, 2010

TIBA KWA KUTUMIA RANGI!

SWALI: Bibi Asia Mohamed wa Makutupora Dodoma anauliza, sheikh niliwahi kusikia kwamba kuna tiba inayofanyika kwa kutumia rangi. Je ni kweli, na hizo rangi zinatumika vipi?

JIBU: Ni kweli unaweza kutibu kwa kutumia rangi, tiba hii ya rangi au kwa kiingereza inaitwa Chromotherapy ni utaalamu wa zamani sana wa kutibu ambao misingi yake ni namna rangi zinavyokuwa na athari katika sehemu tofauti za mwili wa binaadam.



Kwa mfano, sehemu ya mwisho ya Spektra (mpangilio maalum wa Taswira zinazotokana na miali ya mnunurisho) ambayo ina rangi zilizochangamka kama vile Nyekundu, rangi ya Machungwa na rangi ya Njano. Hizi zina kazi ya kukurekebisha na kukujaza nguvu, ujasiri na matumaini kwa wale wanaokata tamaa upesi na waoga.


Rangi zilizotulia au kupoa za Bluu, Bluu iliyoiva na Urujuani (Violet). Hizi zina kazi ya kuupoza na kuutuliza mwili wa binaadam ambao unaweza kuwa umeathirika kutokana na wasiwasi.

Rangi ya kati katika Spektra ambayo ni Kijani hii inafanya kazi ya Mizania ili mwili usitetereke kutokana na athari yeyote ile.

Kazi hii inafanyika kwa kupanga kila moja ya rangi hizo saba katika sehemu saba za mwili zinazotoa Nishati ambayo inausaidia au kuudhibiti mwili katika jambo fulani, likiwa la hasira, wasiwasi, hofu na kadhalika.

Sehemu hizo ni katikati ya kipaji cha uso ambayo ni sehemu ya rangi Nyekundu, Bega la kushoto ambayo ni sehemu ya rangi ya Njano, Bega la kulia ambayo ni sehemu ya rangi ya Machungwa, Moyo ambayo ni sehemu ya rangi ya Kijani, kitovuni ambayo ni sehemu ya rangi ya Urujuani (violet), sehemu ya juu ya mguu wa kushoto ambayo ni rangi ya Bluu iliyoiva (Indigo) na sehemu ya juu ya mguu wa kulia ambayo ni rangi ya bluu.

Sehemu hizi zilizotajwa kuna Neva ambazo zina mawasiliano ya moja kwa moja na ubongo.

Tiba inafanyika kwa kuweka rangi inayohusika katika sehemu inayohusika na iliyoathirika na maradhi ya huyo mgonjwa.

Kazi hii hufanywa katika jua au kwenye taa ya umeme ambayo mwanga wa jua au taa unapitia katika kifaa maalum kinachotoa rangi. Tiba hii inafanyika kwa muda wa saa moja mpaka masaa mawili.

Katika tiba, rangi zina muda wake ambao zinaweza kukusaidia aidha kwa kuvaa nguo ya rangi hiyo au kwa kuitazama rangi hiyo kwa muda wa dakika kumi mpaka ishirini au kwa kutumia taa ya rangi inayohusika.

Mfano rangi ya Njano, muda wake ni asubuhi, katika kipindi hicho rangi hii inasaidia kuamsha akili na uwezo wetu wa kufikiria na kutupa mawazo yenye mantiki.

Wakati wa mchana rangi ya Machungwa ndio yenye nguvu. Huu ni wakati mzuri wa kuonyesha hisia za kweli, kuvumbua na kushirikiana katika starehe. Miali ya Njano katika wakati huu inatusaidia kuondoa ile hali ya kusita kufanya jambo fulani, au kukumbuka mambo yaliyopita na vile vile inatusaidia kuondoa huzuni, majonzi na wasiwasi au woga.

Muda wa jioni tunatakiwa tufanye kazi na rangi Nyekundu ambayo athari zake zinaonekana Mbinguni wakati Jua linapozama.

Rangi Nyekundu inatupa ujasiri, nguvu na kutufanya tuonekane wenye mandhari bayana.

Rangi ya Urujuani au Violet muda wake ni kipindi cha mwanzo cha usiku. Athari za miali ya rangi hii ni kujitolea mhanga au kafara na utakaso. Rangi hii inasaidia unapofanya taamali, au kutafakari (Meditation).

Usiku wa manane rangi iliyo na nguvu na inayofaa ni rangi ya bluu iliyoiva (Indigo). Rangi hii ina uhusiano na hali ya kutafuta ukweli wa kiroho na mizimu na msukumo wa kuandika (wakati huu watu wengi wanaandika vitabu au kusoma). Elimu na busara zinafikiwa kwa urahisi katika kipindi hiki cha usiku.

Muda wa Alfajiri rangi inayofaa ni Bluu. Rangi hii ina athari za uaminifu, matumaini na imani. Rangi hii ya Bluu inautuliza mwili na kutupa uwezo au kipaji cha kuelewa au kuhisi kitu haraka.

Kabla jua halijachomoza rangi ya kijani ndio inayofaa. Rangi hii ina uwezo mkubwa katika masuala ya kukua kwa biashara au kupanda kwa hali yako ya kimaisha au kuwa na afya nzuri.

No comments:

Post a Comment

THE DARKEST HOURS (SAA ZA GIZA TOTORO)- 1

Mtunzi: Hashim Aziz (Hashpower) 0719401968 “Ngo! Ngo! Ngo! Fungua!” “Nanii?” “Fungua!” “Jitambulishe kwanza, wewe nani?” “Nimese...