WAZAZI CHANZO KIKUU CHA MIMBA MASHULENI MANYARA

Baadhi ya wazazi wasio na mwamko wa elimu mkoani Manyara, wamedaiwa kuwa chanzo cha wanafunzi wa kike hasa wanaosoma katika shule za sekondari za kata kukatisha masomo kwa sababu ya tatizo la mimba mashuleni. Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wanafunzi, walimu, viongozi wa serikali na baadhi ya wazazi wamekiri kuwa kuna idadi kubwa ya wanafunzi wanaopata ujauzito mkoani humo na kukatisha masomo kutokana na baadhi ya wazazi kutoona umuhimu wa elimu na kuwatafutia wachumba mabinti zao ili wakaolewe na kupata mahari kabla hawajamaliza masomo.

Hayo yamebainika baada ya uchunguzi wa kina uliofanyika katika mikoa 17 Tanzania bara na visiwani, ambapo lengo la utafiti huo ilikuwa ni kuangalia ukubwa wa tatizo la wanafunzi wa kike kukatisha masomo na sababu zinazochochea tatizo hili. Mkoa wa Manyara ambao wakazi wake wengi ni wafugaji wa jamii ya kimasai na jamii nyingine, ni iongoni mwa miko iliyofanyiwa utafiti na imebainika kuwa kuna idadi kubwa ya wanafunzi wanaokatisha masomo kutokana na ujauzito, na kwa kipindi cha kuanzia mwaka 2009 hadi Mei 2010, jumla ya kesi 40 ziliripotiwa katika wilaya ya Hanang pekee.

Kwa mujibu wa Afisa Elimu wa Wilaya ya Hanang, Deo Sukumsi, tatizo kubwa la jamii ya wafugaji wa kimasai ni mwamko mdogo wa elimu walionao wazazi wa jamii hiyo.
“Kesi nyingi za watoto kupewa ujauzito zinamalizwa na wazazi na watuhumiwa kinyemela, wanalipana mahari ya ng’ombe au pesa taslimu kisha wanahalalisha ndoa kwa binti aliyepewa ujauzito na mtuhumiwa. Hali hii ni hatari sana kwa taifa letu, na tunafanya kila tunaloweza kupambana nao” alisema Bwana Sukumsi.

Akizitaja kata zinazoongoza kwa matukio ya mimba wilayani Hanang, Bwana Sukums alisema kata za basodesh na Lighanga zinaongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya kesi za mimba zinazomalizwa kienyeji bila kufikishwa kwenye vyombo vya sheria. Katika kata tajwa, imebainika kuwa pia baadhi ya vingozi wasio wa waaminifu wa mabaraza ya kata, hushiriki kula rushwa kuoka kwa wazazi na watuhumiwa ili wasiyafikishe mashtaka yao mbele ya sheria.

Kwa upande wa wilaya ya Kiteto, kuna matukio mengi sana ya wanafunzi kukatisha masomo kutokana na tatizo la ujauzito, lakini ni kesi tano pekee ndizo zilizofikishwa mbele ya vyombo vya sheria kwa kipindi cha mwezi Januari hadi Mei mwaka huu. Akilizungumzia hili, Mkuu wa Wilaya ya Kiteto, Bwana Frank Uhaula, alisema wazazi wa jamii ya kifugaji ni tatizo kubwa katika vita dhidi ya mimba mashuleni.

“Tunajitahidi kwa kadri ya uwezo wetu kuwaelimisha wazazi juu ya umuhimu wa watoto wa kike kusoma, tuna mikakati mingi ya kuhakikisha elimu inafika kwa jamii ya wafugaji. Lakini tunajitahidi pia kuhakikisha kesi zote za mimba zinashughulikiwa ipasavyo na watuhumiwa wanachukuliwa hatua za kisheria, lakini tunavunjwa nguvu na wazazi ambao hawafikishi kesi hizi mbele ya vyombo vya habari na wanamalizana kienyeji.nawaomba waache mara moja mchezo huu kwani wakibainika tutaanza kuwachukulia hatua wao kwanza.”

“Ni dhahiri kuwa wazazi kama hawa wakielimishwa na kuelewa umuhimu wa elimu kwa watoto wao, hususan wa kike, hawatakuwa tayari kuwaachisha mabinti zao shule na kuwaoza kwa tama ya kupata mahari, na badala yake watawalinda kwa hali na mali ili kuhakikisha walau wanahitimu elimu ya sekondari kwa faida ya maisha yao ya baadae, alisisitiza Bwana Uhaula.