Monday, October 19, 2009

MY HEART IS BLEEDING ( MOYO WANGU UNAVUJA DAMU)-3

Wakati kesi nzito inayomkabili kijana mdogo anayeshtakiwa kwa kufanya mauaji makubwa na ya kutisha ikiendelea kugusa hisia za maelfu ya watu, kitu cha ajabu kinatokea mahakamani.

Jaji mkuu Profesa Kadir Mudhihir Simba anaanguka mahakamani na kupoteza fahamu akiwa katika hatua za mwisho za kutoa hukumu. Anakimbizwa Hospitali hali yake ikiwa mbaya sana na kadri muda unavyozidi kwendahali yake inakuwa mbaya zaidi.

Huku nyuma anaacha watu wakiwa wamepigwa na bumbuwazi wakiwa hawaelewi nini kilichomsibu na tukio lile linamaanisha nini. Vurugu nyingine inazuka mahakamani lakini polisi wa kutuliza ghasia wanaidhibiti na kufankiwa kumrudisha mshtakiwa gerezani.

Watu wanaanza kufuatilia chanzo cha tukio lile miaka mingi iliyopita. Historia inaonyesha kila kitu kilivyokuwa mpaka kumsababisha kijana yule kufanya mauaji makubwa kiasi kile yaliyotikisa nchi.

Twende pamoja ufahamu chanzo...
Kwa jinsi wazazi wa Miriam, Mzee Shamsi na mkewe walivyokuwa wakimpenda mkwe wao, ilibidi wamshawishi Khalfani pamoja na mkewe Miriam wahamie nyumbani kwa Mzee Shamsi. Mzee Shamsi na mkewe hawakuwa na mtoto mwingine zaidi ya binti yao Miriam, hivyo kuondoka kwake na kumfuata mumewe, kuliwafanya wabaki wapweke sana kwenye himaya yao.

Khalfan na mkewe hawakuwa na kipingamizi chochote, wakakubali kuhamia nyumbani kwa mzee Shamsi, (Ukweni). Maisha yao yakazidi kuwa mazuri siku baada ya siku, na sasa Khalfan akawa ameachana na biashara yake ya mboga mboga na matunda.

Badala yake akawa akimsaidia mzee Shamsi kwenye shughuli zake za Biashara ya madini ya Ruby. Muda mwingi akawa akitembezwa kwenye gari ndogo aina ya “Mercedes Lexus 5 New Model” ya kisasa, akimwonyesha vitega uchumi vyake na kumwelelekeza jinsi ya kuhudumia mali zote walizokuwa nazo.

Kwa kifupi mzee Shamsi alimuamini sana Khalfan, kiasi cha kumchukulia kama mwanae wa kumzaa. Hakumficha kitu chochote, alikuwa akimpa mpaka siri zake za ndani. Aliamini kuwa kwa kuwa hakubahatika kupata mtoto wa kiume, basi khalfan ndio atakuwa mrithi wa mali zake zote akishirikiana na mkewe Miriam.

Alichokuwa akimsisitiza siku zote ni kumpenda kwa dhati mkewe, mtoto wao wa pekee Miriam. Alikuwa akimuonya pia kuwa makini sana na marafiki wa kibiashara ambao atakuwa akishirikiana nao hususani kwenye bashara ya madini kwani akili za mwanadamu hubadilika sana akiona vitu vya thamani. Nasaha alizokuwa anapewa kila siku zilimjenga upya kifikra na kumpa ujasiri kuliko ilivyokuwa mwanzo. Alijiona anaweza kufanya mambo makubwa hata kama hakuwa na elimu kubwa kichwani

Ilikuwa ni majira ya saa nne asubuhi, Miriam akiwa anamuandalia mumewe Khalfan kifungua kinywa, huku wakitaniana utani wa mume na mke! Kila mmoja alikuwa na furaha kuwa na mwenzake. Wakawa wakitaniana na kucheza kama watoto huku Miriam akiendelea kuandaa kifumgua kinywa.

Wakati hayo yakiendelea taarifa ya habari iliyokuwa inasomwa kutoka kituo maarufu cha redio, “The Bulletin FM” iliwashtua wote kiasi cha kufanya kila mtu aache alichokuwa anakifanya na kukimbilia jirani na redio ili asikie vizuri taarifa ile.

Ilikuwa ni habari mbaya ya ajali ya kutisha ya ndege iliyotokea muda mfupi uliopita. Ajali hiyo ilihusisha ndege ya kampuni ya “TRY EMIRATES” aina ya Jet B710 Sossoliso, iliyokuwa inatoka uwanja wa kimataifa wa Blazinair International Airport (BLIA) kuelekea Muscat Oman. Habari ilizidi kuelezea kuwa ajali hiyo ilisababishwa na hitilafu katika moja ya injini zake, hali iliyosababisha ndege hiyo kulipuka muda mfupi baada ya kuruka, kisha ikaangukia baharini.

Kilichosikitisha ni kwamba abiria wote 67 waliokuwemo kwenye ndege walikuwa wakihofiwa kupoteza maisha katika ajali ile. Habari ilihitimishwa kwa mahojiano na watu walioshuhudia ajali ile ambapo kila aliyehojiwa alikiri kuwa hakuwahi kusikia wala kushuhudia ajali mbaya kama ile.

Khalfan na mkewe walibaki wakikodoleana macho, wasijue nini cha kufanya. Kilichowashtua ni kwamba ni asubuhi ya siku hiyo masaa machache tu yaliyopita walitoka kuwasindikiza mzee Shamsi na mkewe uwanja wa ndege, wakielekea oman kupeleka biashara yao ya madini ya Ruby.

Haikuwa kawaida kwa mzee Shamsi kusafiri na mkewe, kwani mara zote yeye aliposafiri mkewe alibaki kuwa msimamizi wa mali zao, lakini baada ya binti yao kuolewa na Khalfan Mwalukasa, shughuli zote za usimamizi wa mali zilibaki kuwa chini ya uangalizi wa Khalfan kwani walimchukulia kama mtoto wao, na kwa pamoja walikubaliana kuwa yeye ndiye atakayekuwa mrithi wa mali zao, pindi mauti yatakapowafika.

Ni masaa mawili tu yaliyopita majira ya kama saa mbili za asubuhi Khalfan na mkewe waliwasindikiza wazazi wao uwanja wa ndege na wakasubiri mpaka walipopanda ndege ya kampuni ya usafiri wa anga ya TRY EMIRATES tayari kwa safari ya Oman. Ni baada ya kuhakikisha kuwa wamepanda ndege, ndipo Khalfan na mkewe waliporudi nyumbani kuendelea na shughuli zao.

Wakiwa wanajiandaa kupata kifungua kinywa ndipo taarifa ya kusikitisha na kutia majonzi iliposikika. Hiyo ilimaanisha kuwa mzee Shamsi na mkewe walikuwa wamepoteza maisha katika ajali ile. Msiba mkubwa kiasi gani. Habari ya ajali ile iliwashtua watu wengi, ambao kwa namna moja au nyingine waliwapoteza ndugu, jamaa na marafiki zao waliokuwemo kwenye ndege ile.

Kwa Khalfan Mwalukasa, licha ya ukweli kwamba aliguswa na vifo vya wakwe zake, hii ilikuwa ni kama bahati ya mtende kuota jangwani, waswahili wanasema kufa kufaana. Ni Khalfan huyu huyu aliyekimbia kwao kutokana na ugumu wa maisha, akawa akifanya biashara ya mbogamboga na matunda, ndiye sasa alitakiwa kuwa mmiliki wa hazina ya utajiri ulioachwa na mzee Shamsi. Hakuwahi kuota wala kutegemea kuwa ipo siku atakuja kumiliki hazina kubwa ya utajiri kama ile. Kweli Mungu alikuwa ametenda miujiza katika maisha yake.

********

Siku ziwaka zinakwenda, sekunde, dakika, masaa! Mara usiku, mara mchana… mawio na machweo. Kumbukumbu ya kuwapoteza wazazi mzee Shamsi na mkewe taratibu ikaanza kupotea vichwani kwa Khalfan na mkewe Miriam. Khalfan akawa anajitahidi kwa kadri ya uwezo wake wote kumliwaza mkewe na kumfaya asahau yote yaliyotokea. Yeye ndiyo akawa baba na kichwa cha familia.

Mwanzoni ilimuwia vigumu kuweza kusimamia mali zote zilizoachwa na mzee Shamsi lakini kila alipokuwa akikumbuka mawaidha aliyokuwa anapewa na mzee Shamsi, akawa anajipa moyo kuwa hakuna lisilowezekana. Taratibu akawa anapata uzoefu kila siku mpya ilipokuwa ikianza. Hali hiyo ilionekana kumfariji sana mkewe, ambaye sasa akawa na uhakika kuwa kila kitu kitaendelea vizuri na kushamiri japokuwa alikuwa amepoteza wazazi wake.

Khalfan akawa anajituma kwa bidii kuhakikisha kuwa hakuna kinachomshinda.
Baada ya miezi saba tangu mzee Shamsi na mkewe wapoteze maisha katika ajali mbaya ya ndege, Miriam akiwa anarudi kutoka hospitali alikuja na habari njema kwa mumewe!

“Mume wangu, nafurahi kukuambia kuwa baada ya siku si nyingi nitakuzalia mtoto!”
“Unasema kweli mke wangu? Safi sana!” Khalfan akiwa haamini, alimkumbatia mkewe kwa nguvu… na hapo ndipo naye alipoelewa mkewe alikuwa anamaanisha nini. Mkewe alikuwa mjamzito, furaha iliyoje! Maisha yakawa kama ndio yameanza upya, muda wote wakawa wakicheza kama watoto, wakishinda kutwa nzima katika bustani za maua zilizokuwepo hapo nyumbani.

Muda ukawa unazidi kwenda, huku Khalfan akiwa anampeleka mkewe Clinic mara kwa mara, kuhakikisha anajifungua salama. Miezi ikawa inakatika, hatimaye miezi tisa ikawa imetimia. Bi Miriam akajifungua salama mtoto wa kiume, mzuri kama mama yake. Furaha katika ndoa yao ikawa imeongezeka mara dufu, na ikawa inazidi kuongezeka kila uchao.

Wakampa mtoto wao jina la Khaleed . “Mume wangu yaani furaha unayonipa maishani, sikuwahi kutegemea hata siku moja! Nakupenda sana mume wangu na Mungu azidi kuibariki ndoa yetu tudumu mpaka kifo kitakapo tutenganisha” Bi Miriam alikuwa akiongea kwa hisia nzito za mahaba kwa mumewe wakiwa na kichanga chao Khaleed, wakipunga upepo wa jioni.

Baada ya miaka miwili wakapata mtoto mwingine wa kiume, tofauti na kaka yake, yeye alifanana mno na baba yake. Watoto wakawa na afya njema, furaha na walipewa malezi bora.

Khalfan sasa akawa baba wa familia, mkewe Miriam naye akawa mama kama alivyokuwa akitamani siku zote. Waliyafurahia sana maisha yao. Muda mwingi walikuwa sambamba wakisaidiana kuwapa malezi bora watoto wao na kuwafundisha maadili mema. Utajiri nao ukawa unazidi kuongezeka kila kukicha, shamba na bustani zao za maua zikawa zinazidi kushamiri na kuwa “Evergreen” huku mazao yakistawi sana.

Wapo watu walioyahusisha mafanikio yale na imani za kishirina wakihisi kuwa huenda Khalfan Mwalukasa alikuwa akitumia nguvu za giza ili kupata mafanikio. Wapo walioanza kummezea mate wakiona kuwa hakustahili kuwa na mafanikio makubwa kama yale. Wala maneno ya walimwengu hayakuwarudisha nyuma. Walikuwa waimwamwini Mungu wao na walijitahidi kuishi vizuri na kila mtu, wakitoa misaada mingi ya kijamii kwa watu wenye shida na wanaoishi katika mazingira magumu.

Waliwasaidia pia watoto wenye shida mbalimbali hasa wale waliokuwa wakiishi kwenye mazingira magumu bada ya kufiwa na wazazi wao ama kutokana na hali duni za wazazi wao. Walijtahidi kwa kadri ya uwezo wao wote kugawana kile walichojaaliwa na Mungu kwa wale ambao hawakuwa nacho. Kadri muda ulivyokuwa unaenda wakazidi kujijengea jina na umaarufu huku kila mwenye shida akikimbilia kwao kuomba msaada.

Walifanikiwa pia kuanzisha kituo cha kulelea watoto yatima na wale wa mitaani, na wakaamua kukipa jina la “Shamsi Memorium Orphanage” ikiwa kama kumbukumbu ya mzee wao Shamsi na mkewe waliokuwa wameshatangulia mbele za haki.

Tukutane next issue!

No comments:

Post a Comment

THE DARKEST HOURS (SAA ZA GIZA TOTORO)- 1

Mtunzi: Hashim Aziz (Hashpower) 0719401968 “Ngo! Ngo! Ngo! Fungua!” “Nanii?” “Fungua!” “Jitambulishe kwanza, wewe nani?” “Nimese...