Tuesday, October 13, 2009

MY HEART IS BLEEDING (MOYO WANGU UNAVUJA DAMU)-2

Kijana mdogo anapandishwa kizimbani akishtakiwa kwa kosa la kuua watu wengi kwa mikono yake. Ushahidi ulishakamilika siku nyingi zilizopita kwani mshtakiwa aljisalimisha mwenyewe mikononi mwa Polisi wa kimataifa (Interpol) akiwa na vithibitisho vyote vya namna alivyoendesha mauaji yale makubwa na ya kutisha yaliyoifanya nchi nzima kuzizima kwa hofu.

Pamoja na kukutwa na hatia, mahakimu wote waliokuwa wakipangiwa kusikiliza kesi yake, walikuwa wakijitoa katika hatua za mwisho kila mmoja akitoa sababu zake binafsi. Mwishoni jaji mkuu, Profesa Kadir Mudhihir Simba anaamua kuingilia kati na kuisikiliza mwenyewe kesi ile. Hapo ndipo anapogundua kuwa kesi ile ni ngumu kupita kawaida. Ni kweli kwamba kuua ni kosa kubwa kisheria(murder), lakini sababu zilizomfanya kijana huyu mdogo kuua ndio swala lililoleta utata.

Kila mtu sasa anaanza kuwa na shauku ya kutaka kujua nini chanzo cha mauaji yale. Je ni sababu gani zilizomfanya kijana huyu mdogo kuua? Nini hatma yake? Atahukumiwa kunyongwa, kifungo cha maisha au ataachiwa huru?
Twende pamoja katika safari ndefu ya kuutafuta ukweli.
***************************
Profesa Kadir Mudhihir Simba ni hakimu mwenye uzoefu wa siku nyingi katika medani ya siasa. Alikuwa na ujuzi na utaalamu wa kutosha katika kutoa hukumu za kesi ngumu, kesi zilizoonekana kushindikana au zenye utata. Watu wote walimwamini kwani mara zote hukumu alizokuwa anazitoa zilikuwa ni zenye kuzingatia sheria na haki. Uwezo wake mkubwa wa kuchambua mambo kwa kina na busara alizokuwa nazo, vilimfanya ateuliwe kuwa jaji mkuu miaka kumi na mbili iliyopita.

Pamoja na sifa hizo zote alizokuwa nazo, kesi hii ilionekana kumchanganya sana kichwa chake na kumkosesha sana raha kiasi cha kumfanya asite kutoa hukumu. Upelelezi ulishakamilika muda mrefu kwani mshtakiwa alijisalimisha mwenyewe mikononi mwa polisi akiwa na vithibitisho vyote vya namna alivyofanya mauaji hayo makubwa na ya kutisha.

Hakukuwa na sababu yoyote ambayo ingezuia hukumu kutolewa siku hiyo, Lakini bado jaji mkuu alionekana kupoteza mwelekeo. Alitamani aiahirishe kesi ile mpaka siku nyingine, lakini alihofia kupoteza heshima ambayo alijijengea kwa raia. Sasa aligundua ni kwa nini mahakimu wote saba walioteuliwa kuisikiliza kesi ile walikuwa wakijitoa katika hatua za mwisho.

Aligeuza shingo kumtazama mshtakiwa, kisha wazee wa mahakama na mwisho umati uliokuwa umeijaza mahakama ile. Kwa mara ya kwanza tangu aanze kazi miaka mingi iliyopita, aliuhisi ugumu uliokuwa mbele yake. Japokuwa alikuwa amevaa miwani, macho yake yalionyesha dhahiri jinsi alivyokuwa akibabaika. Usingeweza kuamini kuwa huyu ndio yule jaji mkuu, Profesa Kadir Mudhihir Simba wa siku zote.

Ni kweli kabisa kwamba kuua, kwa kukusudia au bila kukusudia ni kosa kubwa mbele ya sheria, lakini sababu zilizomfanya kijana huyu mdogo kufanya mauaji makubwa kiasi kile ndilo swala lililoleta ugumu.

Jasho lilianza kumtoka kiasi cha kuamuru madirisha yote yafunguliwe na viyoyozi vyote vya mle mahakamani viwashwe. Baada ya kubabaika kwa muda mrefu, hatimaye alipiga moyo konde na kuanza kutoa hukumu.
“Kwa mujibu wa sheria na katiba ya nchi ya mwaka 1962, ibara ya kwanza ya makosa dhidi ya ubinadamu, kifungu kidogo cha kwanza,umepatikana na hatia ya kuua idadi kubwa ya watu kwa kukusudia. Baada ya mahakama kuridhishwa na ushahidi uliowasilishwa dhidi yako, Una..unahukum… unahu……ku……mi……w……”

Hakuna aliyeamini kilichotokea! Jaji mkuu alianza kubabaika na kushikwa na kigugumizi kikali huku jasho jingi likimtoka kama maji. Mwili wote ulikuwa umeloanishwa kwa jasho na sasa akawa anatetemeka mwili mzima. Alijitahidi kujikaza ili aendelee kusoma hukumu lakini alishindwa. Watu walikuwa wamepigwa na butwaa wakiwa wanashangaa kilichomsibu jaji yule. Alizidi kutetemeka mwili mzima na kuazna kuzitupa hovyo karatasi za jalada la hukumu na mara akadondoka kutoka kwenye kiti alichokuwa amekaa mpaka chini, kisha akawa anaporomoka kwenye ngazi. Hakika hii ilikuwa kali ya kufunga mwaka.

Ungeweza kudhani kama yanayotokea mle mahakamani ni viini macho au miujiza, lakini haikuwa hivyo. Akiwa pale chini alianza kutupa mikono na miguu huku povu lililochanganyikana na damu likimtoka puani na mdomoni. Ungeweza kuhisi anataka kukata roho. Umati wote wa watu waliokuwa mle mahakani , ulipigwa na bumbuwazi kwa mshtuko mkubwa walioupata. Ilibidi makarani wa mahakama wafanye kazi ya ziada kwa kusaidiana na watu wa huduma ya kwanza.

Waliwahi kumuinua pale chini na kumkimbiza nje akiwa juu ya machela, na muda mfupi baadae gari la wagonjwa likawa linakimbia kwa mwendo wa kasi kumuwahisha Hospitali. Mtuhumiwa bado alikuwa ametulia kizimbani na yeye akiwa amepigwa na bumbuwazi kwa yale yaliyokuwa yametokea.

Watu wakaanza kukanyagana kila mmoja akitaka ashuhudie kinachoendelea nje ya mahakama. Askari waliokuwa wamejaa mle mahakamani walifanya kazi ya ziada kuhakikisha mtuhumiwa anarudishwa gerezani. Eneo lote likazingirwa na taharuki huku hali ikiwa tete na ya kuogopesha. Polisi walifanya kazi yao kikakamavu na kuhakikisha hakuna madhara makubwa yanayotokea pale mahakamani.

Muda mfupi baadae habari kutoka Hospitali kuu ya Blaziniar zilieleza kuwa hali ya afya ya jaji Mkuu Profesa Kadir Simba ilikuwa ikizidi kuwa mbaya kadri muda ulivyokuwa ukienda. Kwa mujibu wa Daktari mkuu Shyroze Mahiza aliyoitoa kwa vyombo vya habari, jaji mkuu alikuwa amepatwa na mshtuko wa moyo na kusababisha mishipa ya damu iliyoko kichwani kupasuka na kuvujisha damu kwenye ubongo.

Kitaalamu hali hii iliitwa “Venule Rapture due to Hypertension Bp”, na husababisha mtu kupoteza fahamu kwa muda mrefu. Hayo ndiyo yaliyokuwa yamemtokea jaji Simba kwani aliendelea kuwa katika hali ya kupoteza fahamu kwa muda mrefu sana.

Kila aliyemfahamu alimuonea huruma kwa yaliyompata na kila mtu akawa anajiuliza nini kimesababisha hali kama ile itokee. Kila mtu aliongea lake kwani jambo kama hilo halikuwahi kutokea hata mara moja katika historia ya nchi. Wengine waliliona kama muujiza huku wengine wakilihusisha na imani kali za kishirikina. Hali hiyo ilizua hamu na shauku ya watu kutaka kufahamu yule kijana mdogo ni nani na alikuwa ameendesha mauaji yake kwa sababu gani na katika mazingira gani. Uchunguzi wa kina ukaanza kufanywa ili kuupata uhalisia wa kesi ile.

MANY YEARS AGO-MIAKA MINGI ILIYOPITA
Khalfan Mwalukasa alikuwa ni mzaliwa wa mkoa wa Nyanda, uliopo kusini mwa nchi ya Blazinia. Alikuwa ni mtoto wa kipekee katika familia yao, na akiwa bado kijana aliamua kuondoka nyumbani kwa wazazi wake na kwenda kujaribu kutafuta maisha katika nchi jirani ya Tanzania. Hata hivyo alipofika Tanzania aligundua kuwa maisha yalikuwa magumu zaidi kuliko kwao Blazinia.

Alichokifanya aliamua kwenda kwenye visiwa vya jirani vilivyokuwa vikipakana na nchi yake, visiwa vya Banaland vilivyokuwa katika bahari ya Hindi. Visiwa hivi vilikuwa ni sehemu ya nchi yake hivyo hakukuwa na haja ya kuwa na Passport au viza ya kusafiria. Ilimgharimu kiasi kidogo tu cha pesa kupanda meli na siku chache baadae akawa tayari ndani ya visiwa vya Banaland.

Kwa kuwa kilichomtoa kwao na kukimbilia ugenini ilikuwa ni kutafuta ahueni ya maisha , hakutaka kuchagua kazi kwani hata hivyo hakuwa amejaaliwa kusoma kutokana na wazazi wake kuwa na hali duni ya kimaisha. Alijiwekea dhamira ya kufanya kazi yoyote ambayo ingepatikana ilimradi tu imuingizie kipato. Bahati nzuri alipata kazi ya kuuza genge la mbogamboga na matunda.

Moyo wa kujituma, heshima kwa wakubwa na wadogo na busara alizokuwa nazo vilimfanya aweze kuishi kwa amani japokuwa alikuwa mbali na wazazi wake. Muda mfupi baadae alifanikiwa kufungua biashara yake mwenyewe na akaanza rasmi kujitegemea. Alifanikiwa kupanga chumba kimoja mitaa ya uswahili na taratibu akaanza kutengamaa kimaisha.

Mara zote alikuwa akijikumbusha kuwa kilichompeleka pale ilikuwa ni kutafuta maisha, aliahidi kufanya kila alichoweza ili afanikiwe maishani ikiwa ni pamoja na kujiepusha na mambo ambayo alihisi yangezuia ndoto zake.

Baada ya takribani mwaka mmoja kupita, alikuwa ameshajijengea jina miongoni mwa wafanyabiashara wa mbogamboga na matunda. Aliipenda kazi yake, na faida ndogo aliyokuwa akiipata alikuwa akitumia vizuri na kujiwekea akiba. Wateja wake wengi walikuwa ni wanawake lakini kwa kuwa alikuwa akifahamu alichokuwa anakifanya, hakujihusisha nao zaidi ya uteja wa kawaida.

Miongoni mwa wateja wake, alikuwepo binti mmoja aliyekuwa na asili kama ya mchanganyiko wa damu mbili tofauti. Alionekana kuwa na mchanganyiko wa kibantu na watu wa visiwa vya ushelisheli. Mchanganyiko huu ulimfanya awe na mvuto wa kimahaba kuliko wasichana wengine wa rika lake.

Miriam, tofauti na wateja wengine, alikuwa akipenda sana kupiga stori na Khalfan Mwalukasa. Hata baada ya kuhudumiwa kila alichokuwa akihitaji, bado alikuwa akifurahia kuendelea kuongea na Khalfani bila kujali kama alikuwa akichelewa nyumbani kwao.

Japokuwa alishindwa tu kueleza wazi hisia zake, Miriam alitokea kumpenda Khalfani Mwalukasa lakini alishindwa kumwambia bayana kwa hofu ya kueleweka vibaya. Akawa anaendelea kuumia mtimani siku hadi siku huku akijitahidi kumuonyeshea kwa vitendo kuwa alimhitaji awe baba wa watoto wake. Khalfani Mwalukasa alishaelewa kilichokuwa mawazoni mwa mteja wake Miriam, lakini hakutaka kuwa na papara hasa ukizingatia kilichompeleka kule ilikuwa ni kutafuta maisha na sio mapenzi.

Pamoja na kujifanya mgumu, Khalfani naye alijikuta taratibu akianza kuvutiwa na urembo wa binti Miriam aliyekuwa na haiba ya kike haswaa…mrefu kama twiga, uso wake wa duara ukiwa umepambwa na macho madogo ambayo muda wote yalikuwa kama yana usingizi, huku sura yake ikiwa imejawa na tabasamu tamu muda wote. Taratibu alijikuta uzalendo ukimshinda na mara wakajikuta tayari wamezama kwenye dimbwi la mahaba.

“Khalfani hivi kweli utanioa? Au ndio unataka kunitumia mwisho uniache niteseke?”
Miriam alikuwa akimuuliza huku sauti yake ikwa imejawa na huba.
“Ningependa uwe wangu wa maisha Miriam, lakini hali yangu nadhani we mwenyewe unaiona…itakuwa ni maajabu kwa muuza mboga kumuoa mtoto wa milionea kama wewe, haitawezekana”

Khalfani alikuwa akijitetea mbele ya Miriam, lakini baada ya mazungumzo marefu, Miriam alimtoa wasiwasi kuwa yeye hakuhitaji chochote kutoka kwake, zaidi ya kumhitaji awe baba watoto wake bila kuzingatia hali yake ya kimaisha wala kipato.

Moto wa mapenzi ukaanza kukolea kwenye mioyo ya wawili hawa na baada ya kuwa kwenye uhusiano kwa muda mrefu, hatimaye Miriam alimpeleka “mumewe mtarajiwa” kumtanbulisha kwa wazazi wake. Miriam alikuwa akiishi na wazazi wake wote wawili, Mzee Nurdin Shamsi na mkewe. Walibarikiwa kuwa na maisha mazuri ya kitajiri, utajiri ambao ulitokana na biashara aliyokuwa anaifanya mzee Nurdin Shamsi ya madini ya Ruby. Alikuwa akinunua Ruby kutoka kwa wachimbaji wadogo wadogo na kuisafirisha mpaka nchi za uarabuni (U.A.E). Biashara hiyo ilimuingizia pesa nyingi sana zlizomuwezesha yeye na familia yake kuwa na maisha ya juu.

Alifanikiwa kujenga nyumba nzuri ya kifahari pembezoni mwa fukwe za bahari ya Hindi alikokuwa akiishi na familia yake. Alinunua pia eneo kubwa kuzunguka nyumba yake, alilolipendezesha kwa bustani nzuri za maua, viunga vya minazi na karafuu. Eneo zima lilikuwa likipendeza mithili ya Edeni ndogo.

Baada ya kutambulishwa kwa wazazi wa Miriam, Khalfani Mwalukasa aliendelea kuonyesha nidhamu na heshima ya hali ya juu kwa kila mtu, hali ambayo iliwavutia sana wazazi wa Miriam na kuwafanya wamkubalie kwa moyo mkunjufu kumposa binti yao.

Baada ya kutoa posa, taratibu za ndoa zilianza kuandaliwa na siku chache baadae Khalfan Mwalukasa akawa mume halali wa Miriam Shamsi. Wakayaanza maisha mapya ya ndoa. Kwa kuwa umri wa mzee Shamsi na mkewe ulikuwa umekwenda, na Miriam ndio alikuwa mtoto wao pekee, kitendo cha yeye kuolewa na kwenda kuishi kwa mumewe kiliwafanya wawe wapweke sana. Ikabidi mzee Shamsi amshawishi Khalfan Mwalukasa na mkewe wahamie katika jumba lao la kifahari ili waendelee kuishi wote pamoja. Khalfani alijadiliana na mkewe na wakakubaliana kuhamia nyumbani kwa kina Miriam (Ukweni).

Khalfani akayaanza maisha mapya ndani ya jumba la kifahari, maisha ambayo hakuwahi kuyaota. Alikuwa amebadili sana mazingira, kutoka kuwa muuza mboga na matunda akiishi uswahilini, mpaka kuwa mume wa binti tajiri akiishi ndani ya paradiso ndogo. Alimshukuru Mungu wake na kuahidi kuwa atampenda mkewe kwa moyo wake wote.

“Daima nitakuenzi mke wangu, na kamwe sitakufanya utoe machozi ya uchungu, bali utatoa machozi ya furaha”
Khalfan alikuwa akimpa maneno matamu ya huba mkewe jioni moja wakiwa wameketi kwenye moja ya bustani nzuri zilizokuwa ndani ya kasri la mzee Shamsi. Ndoa yao changa ikatawaliwa na upendo na mahaba ya dhati.

No comments:

Post a Comment

THE DARKEST HOURS (SAA ZA GIZA TOTORO)- 1

Mtunzi: Hashim Aziz (Hashpower) 0719401968 “Ngo! Ngo! Ngo! Fungua!” “Nanii?” “Fungua!” “Jitambulishe kwanza, wewe nani?” “Nimese...